SOMO LA FIQHI
Suali: Ni yapi masharti ya mtu kuwajibika kutoa zaka za mali ya biashara?
Jawabu: Masharti ya kulazimika mtu kutoa zaka ya Mali ya biashara.
1. Kiwango chake kifikie nisabu, na nisabu inakadiriwa kwa kipimo cha dhahabu na fedha.
2. Ikamilishe mzunguko wa mwaka mzima.
3. Iwe imekusudiwa kwa lengo la biashara; na hii ni kwamba iwe imekusudiwa kama kuchuma; kwa kauli ya Mtume ﷺ:
[إنما الأعمال بالنيات] رواه البخاري ومسلم
[Hakika ya matendo ni kwa niya ya mtu] [Imepokewa na Bukhari na Muslim.].
Mtu atakapobadilisha niya yake kutoka kwa biashara na kutumia bidhaa hizo basi hukatika hisabu ya mzunguko (mwaka), na akirudia niya ya biashara ataanza tena upya kuhisabu mzunguko mpya, ila akiwa amekusudia kufanya udanganyifu kwa lengo la kuondosha jukumu la kutoa zaka, basi hapa mzunguko haukatiki.
– Mfano: mtu anunue ardhi mwezi wa mfungo nne kwa nia ya kufanya biashara kisha alipofika shabani akageuza nia na akakusudia kujenga nyumba ya kukaa, hapa mwaka utakatika, kisha mfungo mosi akamua kuifanyia biashara mwaka wake utahisabiwa mfungo mosi ila kama alifanya hivyo kwa njia ya hila na kukimbia asitoe zaka basi mwaka hautakatika.
FAIDA
ZAKA YA RASLIMALI
Kinachotolewa zaka katika mali za biashara ni raslimali ambayo kwamba imekusudiwa kwa lengo la kununua na kuuza ili mtu apate faida, ama raslimali ambayo kwamba ni ya mali za kukaa hazizunguki katika biashara yaani si za kununuliwa ili ziuzwe, basi raslimali kama hii haihisabiwi wakati wa kuhisabu bidhaa za biashara wala haitolewi zaka, mfano wake ni kama makabati, na jokofu/firiji ambazo zinahifadhi bidhaa za kuuzwa, na magari yanayobeba bidhaa, na vyombo vya kubebea bidhaa, na mfano wake.