SHARTI ZA KUSIHI ADHANA
Ili adhana iweze kusihi na kuzingatiwa kisheria kuwa ni adhana kumeshurutizwa kupatikana sharti zifuatazo:-
1. Muadhini awe ni Muislamu, mwanamume, mwenye akili.
Haisihi Adhana ya Kafiri na wala haikubaliwi Adhana yake,na vile vile haisihi Adhana ya Mwanamke na Mtoto ndogo asiefikisha miaka ya kuweza kupambanuwa.
2. Adhana ilingane na mpango uliowekwa.
Ni sharti matamko ya adhana yaletwe kwa mtungo na utaratibu wake kama yalivyopokewa kutoka kwa Bwana Mtume ﷺ.
Hii ni kwa sababu kuacha utaratibu kunatuhumisha kufanya mchezo na kupunguza uzito wa tangazo hili la kuingia kwa wakati wa swala.
3. Iwe ni yenye kufuatanishwa, kusiwe na mwanya mrefu baina ya maneno yake.
Ni sharti upatikane mfululizo baina ya matamko ya adhana, kiasi cha kutopatikana mwanya mkubwa baina ya tamko la kwanza na lile la linalofuatia.
4. Iwe ni pale unapoingia wakati wa Swala.
Na hili linatokana na kauli ya Bwana Mtume ﷺ:
[وإذا حضرت الصلاة فليؤذن لكم أحدكم] متفق عليه
[Itakapohudhuria swala, basi na akuadhinieni mmoja wenu]. [Imepokewa na Bukhari na Muslim]
5. Iwe ni kwa Lugha ya Kiarabu
Ni sharti matamko yote ya adhana yaletwe kwa lugha ya Kiarabu kama yalivyopokelewa kutoka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu ﷺ.
Haijuzu kutolewa adhana kwa lugha nyingine yo yote isiyo Kiarabu, kwani hiyo haitakuwa adhana bali tarjamah (tafsiri ya neno kwa neno) ya adhana
TANBIHI:
Haikusuniwa adhana kwa jamaa ya wanawake, kwa sababu ya fitina inayoweza kupatikana kutokana na kusikilizika sauti zao na wanamume.
Iliyosuniwa kwao ni Iqaama tu, kwa sababu hekima yake ni kuwainua waliohudhuria swala kuswali. Na haina kuinua sauti kama ilivyo kwa adhana.