VIATHIRI AU PINGAMIZI ZA MALEZI
Jamii yetu tunamoishi inakabiliwa na matatizo chungu nzima,miongoni mwa changamoto tunazozipata ni kama zifuatazo;
1. Udhaifu wa maarifa na uchache wa elimu
Jambo hili limesababishwa na watu kusoma Qur’an kimajaka pasi na kuelewa tafsiri yake. Watu hawana juhudi ya kuelewa wanayoyasoma katika Qur’an hivyo kuleta ugumu wa kuweza kutumia mafunzo yanayopatikana katika Qur’an kwenye maisha yao. Bali hata ilipopatikana tafsiri ya Kiswahili ya Sheikh Abdallah Alfarsy (Allah amrehemu), ni wachache mno wanaofanya hima ya kusoma tafsiri ya Qur’an. Tatizo hili limekuwa sugu katika jamii zetu hivyo kupelekea ugumu wa kupatikana mabadiliko halisi ya malezi bora. Hii ni kwa sababu, malezi na tabia za Mtume ﷺ yanapatikana katika Qur’an kwa mujibu wa hadithi ya Aisha Radhi za Allah ziwe juu yake alipoulizwa tabia ya Mtume ﷺ akajibu:
[فَإِنَّ خُلُقَ نَبِيِّ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيهِ وَسَلَّمَ كَانَ القُرآنَ] رواه مسلم
[Hakika tabia ya Mtume ﷺ ilikuwa ni Qur’an.] [Imepokewa na Muslim].
2. Kukosekana dira, ratiba na malengo kwa jumla katika malezi yetu.
Malezi yetu yapo katika mfumo wa kubahatisha na kuiga tamaduni za watu wengine wa hususan wamagharibi. Tunawaiga hasa katika mitaala iliyofungamana na taasisi za kikanisa. Pasi na kufahamu tumejikuta ni watu tuliokosa mwelekeo kwa sababu ya kuiga na kufuata mila za watu wengine tukawachana na mila ya Uislamu. Matokeo yake ni kupata vizazi ambavyo viko mbali kabisa na mfumo aliotuletea Mtume wetu ﷺ.
3. Athari zilizoletwa na mitaala ya shule zinazoegemea sana maono ya kugawanya baina ya dini na dunia.
Mpasuko huu wa watu wanoamini tofauti ya ki manufaa iliyopo baina ya elimu ya dini na dunia imeregesha watu nyuma. Msimamo wa sawa ni kutotafautisha baina ya elimu ya dini na dunia bali mtu awe na yakini ya kuwa elimu yote inatoka kwa Mungu na inapaswa imuelekeze mtu katika kutafuta radhi za Mungu katika maisha yake. Wasioamini msimamo huu umewafanya wakose mwelekeo wa malezi katika jamii.
4. Kutangamana na watu wasio na maadili.
Katika jamii zetu tunatangamana na kuishi na watu aina nyingi wasio na maadili ya kisawasawa. Jambo hili limesababishwa na kugura kwa watu wa sehemu za bara na kuja sehemu za watu wa kwetu kwa malengo tofauti tofauto. Athari za watu hawa waliokuja katika jamii zetu na wenye malengo fiche ,zimeweza kubadili maadili mengi yetu na kuleta ufisadi katika jamii zetu.
5. Falsafa ya uhuru.
Kuna watu wengi wenye msimamo wa kutaka kujikomboa kwa kutumia neno zuri ‘’tuwe huru katika mambo yetu’’ wanataka wafanye wanavyotaka pasi na kufuatiliwa, wasijue kwamba falsafa hii tegemezi yenye asili ya kimagharibi ni sumu iliyotiwa ndani ya asali na sisi pasi na mazingatio yoyote na fikra za kisawa tumetumia sumu hii kiasi cha kutoweza kujinasua hata tukijaribu vipi. Kwa sababu imeingia katika mishipa ya damu yetu na inaendesha maisha yetu.
TANBIHI
Suluhisho ya maradhi haya tuliyoyataja ni kuwa tunahitaji kuja na mfumo mbadala wa taaluma kutokea msingi wa taasisi za mwanzo mpaka ndaki (chuo kikuu), pamoja na kuja na mtaala wenye kuambatana na lengo halisi la dini yetu na kuweza kwenda sambasamba na malimwengu ya kileo.
Makala yameandikwa na: Sheikh Abu hamza
Kusahihishwa kilugha na: Ustadh Ali Juma
Makala yanaendelea…