0%

https://uongofu.com/wp-content/uploads/2021/06/services-head-1.png

MBINU ZA MALEZI- Sheikh Abuu Hamza

MBINU ZA MALEZI

Malezi  yana mbinu  maalumu  ambazo yataka  tuzifahamu, ili tuweze kuwalea  watoto wetu  kwa njia za kisawa. Mbinu hizi zinabadilika  kulingana  na mabadiliko ya kitaaluma yanavyobadilika kwa kasi sana.Pamoja na  athari ya tamaduni zinazotufikia kupitia mitandao mbalimbali. Kwa hivyo kuna dharura ya kuzifahamu  mbinu hizi haswa ukizingatia kuwa kuna athari  ya utandawazi  katika ulimwengushi  au ulimwengu wa kijiji kimoja.Mambo yafuatayo ni muhimu yazingatiwe:

1. Kwanza mbinu ya kuwa wewe ni kiigizo  chema kwa  namna unavyomlea mtoto au jinsi jamii inavyokutazama  wewe  pamoja na mambo unayoyatenda  kuliko unayoyasema. Kwa hivyo kuwa mfano mwema ni muhimu sana katika malezi.

2. Pili  ni mbinu ya mawaidha mazuri  na kumuelekeza mtoto wako mara kwa mara katika njia iliyonyooka.Kutoa mwongozo wa kimaisha kwa unayemlea ni jambo muhimu sana.Hivi kwamba akue akijua mwelekeo unaoutaka wewe kama mlezi wake.

3. Tatu mbinu ya kumpendezesha  na kumwonesha  uzuri wa lile unalotaka  alifanye, vipi lina athari  na maisha yake na kumwonesha  vipi atafaulu akifuata  yale unayomfahamisha.

4. Nne mbinu ya kumtahadharisha na kumwonesha  madhara na hasara atakazopata katika maisha yake na ubaya wa tabia ile mbaya unayomkataza.Kwa mfano madhara ya kutohifadhi wakati, kukhalifu ahadi, kutokuwa na uaminifu katika maisha yake pamoja na tabia mbaya nyingi.

5. Tano ni mbinu ya kupigia mtoto wako mifano hai  ili aweze kutofautisha baina ya faida na hasara za tabia mbalimbali.Mfano Amati mwalimu mwanachuoni wa kike ambaye mpaka leo yupo katika  uhai na amefundisha  Qur’an miaka 110.Huu ni mfano hai katika nchi ya Kenya mwanamke mshela atumia umri wake wote katika kufundisha dini.Hivi ndivyo jinsi tunavyopaswa kujitolea kwa manufaa ya jamii.

6. Sita ni mbinu ya kutumia  visa vilivyotokea katika kurekebisha tabia fulani. Utoaji wa visa ni mbinu muhimu sana katika kulea mtoto.Kwani waliotangulia walipatikana na mambo mengi ambayo lau watoto wetu watakuwa wakihadithiwa watapata mazingatio mengi sana.Mfano wa kile kisa cha yule mwanamume aliyeuwa watu 99 kisha akarudi kwa ALLAH(S.W.T) kumtaka msamaha.Akakutana na msomi aliyemshauri  atoke katika mji ule anaoishi aende katika mji wa watu wazuri.Kisa ni kirefu lakini faida yake ni kuwa, mwisho ALLAH(S.W.T) akamsamehe.Mazingatio tunayoyapata ni kuwa hatupaswi kukata tamaa na rehma ya ALLAH (S.W.T).

7.  Mbinu ya saba ni ya kumzowezesha mtoto kukariri jambo mpaka akazowea  kama alivyofundisha Mtume ﷺ  Swala juu ya mimbari na kama alivyofundisha Sayyidna Uthman b.Affan (R.A) namna Mtume alivyochukua Udhu.Jambo likirudiwarudiwa linabaki kwenye fahamu ya mtoto.

8. Mbinu ya nane ni ya kufaidika na matokeo fulani kisha ukatumia fursa ile kurekibisha kosa au kutilia nguvu fikra fulani kwa kutumia matokeo fulani.Mfano kumsisitiza mtoto afanye bidii ya kuhifadhi Qur’an baada ya kumwona mwenzake akiswalisha msikitini na mengine mengi.

9. Mbinu ya tisa ni kujaribu  kukuza fikra ya mtoto na kuifungamanisha na utumiaji wa busara katika maisha ya wanadamu.Akue akijua kuwa katika maisha kuna mambo mengi yanayohitaji hekima na busara pasi na kutumia nguvu kukabiliana nayo.

10. Mbinu ya kumi ni kujaribu kukusanya  mazoezi uliyoyapata  kulingana  na tajriba yako katika kutaamaliana  na binadamu wengine.Mtoto wako awe karibu na wewe katika kuona ni jinsi gani unataamaliana na watu.Akiona tabia fulani inajirudiarudia hutakuwa na haja ya kumwambia afanye bali atafanya mwenyewe kwa sababu amekuwa akikuona jinsi gani unavyotaamaliana na watu.

11. Kumi na moja ni mbinu ya kutumia mazungumzo mazuri katika kutafuta usawa wa jambo.Na vilevile kukinaisha watu  katika kutazama mambo na vishawishi tofauti katika maisha.

12. Kumi na mbili ni kujaza nafasi au pengo kwa  kutumia fursa inapojitokeza  au kubuni nafasi ya kurekibisha jambo kwa njia ya hekima na busara.

13. Kumi na tatu ni kuangalia jinsi watu wanavyosuhubiana katika safari na kutazama  vitendo vyao katika safari hizo kwani  mara nyingi watu wanafahamika na kudhirika jinsi walivyo wakati wakiwa kwenye safari.

14. Mbinu ya Kumi na nne ni yakuadhibu  na hii yafaa itumike ya mwisho  baada ya kutofanya kazi mbinu zote kumi na tatu zilizotangulia.Mbinu hii yafaa itumike kwa uwangalifu mno na adhabu iwe ya kipimo na iambatane na kosa mara tu linapofanyika.Kwa mfano ni makosa kwa mzazi kumwadhibu mtoto wake leo kwa kosa alilotenda wiki iliyopita.Changamoto ni kuwa wazazi wengi hawajui mbinu hizi,wao hupindukia katika kutesa na kuadhibu tu.

Hivyo basi ni muhimu sana kuzingatia mbinu hizo ili zirahisishe malezi haswa katika ulimwengu huu wa utandawazi.

Makala yameandikwa na: Sheikh Abu hamza

Kusahihishwa kilugha na: Ustadh Ali Juma

Makala yanaendelea…

Toa maoni yako

Begin typing your search above and press return to search.