0%

https://uongofu.com/wp-content/uploads/2021/06/services-head-1.png

UMUHIMU WA DUA

UMUHIMU WA DUA

Viumbe vyote vinamuhitaji Mola wao katika kupata manufaa yao au kuzuia madhara yasiwafikie, kwa lengo la maisha yao hapa Duniani na kesho siku ya mwisho. Na kila mja anapojikurubisha kwa Allah, basi Allah anamuinua daraja na kumfanya mtukufu mbele ya viumbe vyake.
Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala) Anawapa mitihani viumbe vyake kwa misukosuko mbalimbali ili waweze kurudi kwa Mola wao na kuomba msaada kwake katika kupambana na mitihani hiyo.
Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala) anapenda kuombwa msaada na waja wake na anapenda waja wake kurudi kwake pindi wanapofikwa na shida na misukosuko ya ulimwengu. Kufanya hivyo, ndio msingi wa ibada. Na makusudio makubwa ya sharia kuamrisha na kunyeyekea kwa Allah na kutaraji pamoja na kumtegemea Yeye peke yake kwa mambo yote.Imepokewa na Abi Dharri katika hadithi Qudsi:

[يا عبادي كلكم ضال إلا من هديته ، فاستهدوني أهدكم]

[Amesema Mwenyezi Mungu: Enyi waja wangu nyinyi wote ni wapotevu ila Yule niliye muongoza, basi niombeni uongofu wangu].
Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala) Amepanga kila kitu, na Akaweka sababu ya kila kitu. Ameweka sababu za kufaulu Mwanadamu na sababu za kufeli Mwanadamu. Ameumba sababu zote na athari ya hizo sababu, na hakuna kitu kitakua bila ya kutaka Allah (Subhaanahu wa Taala). Na lau angetaka Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala) kuumba kitu bila sababu angefanya. Amesema Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala)

{وهو الغفور الودود ذو العرش المجيد فعال لما يريد }   البروج:16

[Naye ni Mwenye kusamehe, Mwenye mapenzi,Mwenye Kiti cha Enzi, Mtukufu, Atendaye ayatakayo.]    [Al-Buruuj: 16]
Na Amesema Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala)

{ألا له الخلق والأمر تبارك الله رب العالمين}   الأعراف/54}

[Fahamuni, kuumba ni kwake tu Mwenyezi Mungu, na amri zote ni zake. Ametukuka kabisa Mwenyezi Mungu, Mola wa walimwengu wote]    [Al-Araaf:54]

HUKMU YA KUAMRISHWA KUOMBA DUA

Dua ni ibada bora mbele ya Mwenyezi Mungu. Ameamrisha kwa lengo la la kupata kheri na kuzuia shari. Dua ni sababu kubwa ya kupata kheri na Baraka za Mwenyezi Mungu. Na ni sababu kubwa ya kukinga madhara na shari zote. Na hakika Mwenyezi Mungu ameamrisha waja wake kumuomba Dua katika Aya nyingi. Amesema Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala):

{وَقَالَ رَبُّكُمُ ادْعُونِي أَسْتَجِبْ لَكُمْ ۚ إِنَّ الَّذِينَ يَسْتَكْبِرُونَ عَنْ عِبَادَتِي سَيَدْخُلُونَ جَهَنَّمَ دَاخِرِينَ }    غافر: 60

[Na Mola wenu anasema; Niombeni nitakujibuni. Kwa hakika wale wajivunao kufanya ibada yangu, bila shaka wataingia Jahannam wadhalilike]    [Al-Ghafir :60]

UHAKIKA WA DUA

1. Kutukuza mapenzi ya mja kwa mola wake katika kuomba msaada wakutatuliwa matatizo ya ulimwenguni na matatizo ya Akhera.

2. Kuhakikisha ukweli wa kumuabudu Mola wa walimwengu wote. Kufanya hivyo, ni kufungamanisha moyo wa mja na Mola wake na kumtakasia ibada zote Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala), na kutotegemea mtu au kitu kingine pamoja na Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala).

3. Kuwa na yakini kamili yakuwa Allah ndie Mweza wa kila kitu, hakuna kitu kinacho mshinda, Mjuzi wa kila kitu, hakuna kitu kilicho fichika mbele ya Allah (Subhaanahu wa Taala).

4. Kudhihirisha mja unyonge wake mbele ya Muumba wake. Na kumhitaji Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala) katika mambo yake yote. Na huu ndio Ukweli wa kumuabudu Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala).

FADHILA ZA DUA

1. Dua ni Ibada. Amesema Mtume ﷺ:

[الدعاء هو العبادة]    رواه أحمد

[Dua ndio Ibada]    [Imepokewa na Ahmad]

2. Dua ni ubongo wa ibada, kwa sababu Dua imekusanya ibada zote, kunyenyekea, kutegemea, kutarajia, kuogopa, kuomba msaada, n.k.
3. Dua ni Ibada tukufu kushinda ibada zote. Amesema Mtume ﷺ:

[ليس شيء أكرم على الله تعالى من الدعاء]      رواه أحمد

[Hakuna jambo tukufu mbele ya Allah kushinda Dua]    [Imepokewa na Ahmad]

4.Kuwa pamoja na Mwenyezi Mungu kwa ulinzi wake na hifadhi yake. Amesema Mtume ﷺ katika hadithi Qudsi: [Mola Asema: Mimi niko pamoja na mja wangu pindi anapoelekea kwangu kwa maombi yake]          [ Bukhari na Muslim ]

NYAKATI ZA KUKUBALIWA DUA

1.Wakati wa kusujudu. Amesema Mtume ﷺ:

[أقرب ما يكون العبد من ربه وهو ساجد ، فأكثروا الدعاء]    رواه مسلم

[Mja anakuwa karibu zaidi na Mola wake wakati akiwa katika sijida. Kwa hivyo, ombeni Dua wa wingi]     [Imepokewa na Muslim.]

2. Baada ya Adhana. Amesema Mtume ﷺ:

[الدُّعَاءُ لَا يُرَدُّ بَيْنَ الْأَذَانِ وَالْإِقَامَةِ]     رواه الترمذي

[Dua hairejeshwi baina ya Adhana na Iqaama]    [Imepokewa na At-Tirmidhi]

3. Thuluthi ya mwisho wa usiku. Amesema Mtume ﷺ:

ينزل رَبُّنَا تَبَارَكَ وَتَعَالَى كُلَّ لَيْلَةٍ إِلَى السَّمَاءِ الدُّنْيَا حِينَ يَبْقَى ثُلُثُ اللَّيْلِ الآخِرُ يَقُولُ : مَنْ يَدْعُونِي فَأَسْتَجِيبَ لَهُ مَنْ يَسْأَلُنِي فَأُعْطِيَهُ مَنْ يَسْتَغْفِرُنِي فَأَغْفِرَ لَهُ    رواه البخاري

[Mola wetu anateremka kila usiku mpaka katika uwingu wa dunia wakati wa thuluthu ya mwisho wa usiku. Na Anasema: Nani mwenye kuniomba nimkubalie dua yake]     [Imepokewa na Bukhari]

4. Siku ya Ijumaa. Amesema Mtume ﷺ:

[في يوم الجمعة ساعة لا يوافقها مسلم وهو قائم يصلي يسأل الله خيرًا إلا أعطاه]      متفق عليه

[Katika siku ya Ijumaa kuna Saa, hatoafikiwa muislamu (katika saa hiyo) akawa anaswali na kumupmba Mwenyezi Mungu kheri ila Mwenyezi Mungu huumpa ]        [Imepokewa na Bukhari na Muslim]

 KWA FAIDA ZAIDI SIKILIZA MADA HII NA SHEIKH SHADDAD

Toa maoni yako

Begin typing your search above and press return to search.