0%

https://uongofu.com/wp-content/uploads/2021/06/services-head-1.png

UFAHAMU WA IBAADA KATIKA UISLAMU

UFAHAMU WA IBAADA KATIKA UISLAMU

Kumuabudu Mwenyezi Mungu ndio hikma kubwa ya kuumbwa kwa binaadamu. Na ibada ni kuelekea kwa Mungu katika hali zako zote hata ukiwa unafanya mambo ya kawaida na huku watarajia thawabu utalipwa na Allah.

HIKMA YA KUUBWA KWA BINAADAMU NA MAJINI.

Ndugu Muislamu kuumbwa kwa binaadam sio kwa mchezo, bali ni kwa hikma kubwa ndio Allah akawa anatueleza katika Aya nyingi kuhusu kuumbwa kwa binaadamu akatuambia:

{وَمَا خَلَقْنَا السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ وَمَا بَيْنَهُمَا لَاعِبِينَ  مَا خَلَقْنَاهُمَا إِلَّا بِالْحَقِّ وَلَٰكِنَّ أَكْثَرَهُمْ لَا يَعْلَمُونَ }   الدخان 38-39

[Na hatukuziumba mbingu na ardhi na vilivyomo baina yake kwa mchezo. Hatukuviumba hivyo ila kwa Haki, lakini wengi wao hawajui.]     [Al-Dukhaan:38-39]

Na Amesema tena Mwenyezi Mungu Subhanahu wa Ta’aala)

{وَمَا خَلَقْتُ الْجِنَّ وَالْإِنسَ إِلَّا لِيَعْبُدُونِ}    الذريات :56

[Nami sikuwaumba majini na watu ila waniabudu Mimi]   [ Al-Dhariyaat:56]

Yote haya ni kueleza hikma ya kuumbwa kwa binaadamu.

UFAHAMU WA IBAADA

Hakika ya ibada ni kila jambo la kheri katika mambo ya dini na mambo ya dunia na inakusanya maneno na vitendo vyenye kumridhisha Allah. Na utukufu wa Muislamu ni kuwa mnyenyekevu na kwenda mbio kuhakikisha kuwa mja wa Mwenyezi Mungu kisawa sawa kwa kufuata maamrisho na kuepukana na makatazo.

SAMPULI ZA IBAADA

Kwa fadhila zake Mwenyezi Mungu ameweka ibada nyingi tofauti tofauti, kuna ibada ya moyo kama ikhlas na ibada za mwili kama vile swala tano na kuna ibada za mali kama kutoa zaka. Kutoa mali hali ya kuwa na imani na radhi kwa ajili ya kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu. Kuna ibada ambazo zinakusanya baina ya mali na mwili kama hija na jihadi. Kisha Mwenyezi Mungu(Subhaanahu wa Taala)ametutukuza kwa kutuwekea sunna za swala na Sadaka na swaumu na hajj na ‘umra ili zipate kutuinua daraja.

SHARTI ZA KUKUBALIWA IBAADA

Ibada haikubaliwi ila kwa masharti mawili:-
1. Amali iwe ni kwa ajili ya Mwenyezi Mungu na haina riyaa.
2. Ifanyike kulingana na alivyoiweka Mwenyezi Mungu na kuelezewa na Mtume ﷺ.
Kwani dini imekamilika haitaki kuzidishwa wala kupunguzwa Mwenyezi Mungu (Subhanahu wa Ta’aala) anatuambia:

الْيَوْمَ أَكْمَلْتُ لَكُمْ دِينَكُمْ وَأَتْمَمْتُ عَلَيْكُمْ نِعْمَتِي وَرَضِيتُ لَكُمُ الْإِسْلَامَ دِينًا}   المائدة :3}

[Leo nimekukamiliishieni Dini yenu, na nimekutimizieni neema yangu, na nimekupendeleeni UISLAMU uwe ndiyo Dini.]      [Al-Maaida:3]
Na Mtume ﷺ ameifikisha kama ilivyo na hakuna mtu mpotevu kuliko mwenye kufuata hawaa yake.
Ukitaka malipo kwa mambo ya kawaida huwa ni ibada yenye kukukurubisha.
Ewe Muislamu vitendo vyako vyote, ukikusudia kupata radhi za Mola utapata.
Kuwatii wazazi wako ni ibada.

[جَاءَ رَجُلٌ إِلَى النَّبِيِّ-صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ-يَسْتَأْذِنُهُ فِي الْجِهَادِ فَقَالَ أَحَيٌّ وَالِدَاكَ قَالَ: نَعَمْ قَالَ: فَفِيهِمَا فَجَاهِدْ]   رواه البخاري

Alikuja mtu kwa Mtume ﷺ akitaka ruhusa kwenda jihadi. Akaulizwa: [Je wazazi wako hai? Akasema Mtume ﷺ: [Nenda ukapigane jihadi kwa kuwatii]     [Imepokewa na Bukhari]
Utakuta kuwatendea wema wazazi ni kama kwenda katika uwanja wa jihadi. Kuunga kizazi ni kutekeleza wajibu.
Kama vile alivyosema Allah (Subhaanahu wa Taala)

{اتَّقُوا اللَّهَ الَّذِي تَسَاءَلُونَ بِهِ وَالْأَرْحَامَ ۚ إِنَّ اللَّهَ كَانَ عَلَيْكُمْ رَقِيبًا}    النساء:1

[Na tahadharini na Mwenyezi Mungu ambaye kwaye mnaombana, na jamaa zenu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuwaangalieni.]     [Al-Nnisaa:1]

Ndugu Muislamu hata chakula unacholisha watoto wako unapata thawabu. Mtume ﷺ Amemwambia Sa’ad:

[حتى ما تجعل في فم امرأتك]

[Hata unacho kiweka katika kinywa cha mke wako]. Yaani utapata thawabu. [Imepokewa na Bukhari na Muslim.]

Kuwalea watoto wako Malezi bora pia ni ibada, Allah anatuambia:

{يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا قُوا أَنفُسَكُمْ وَأَهْلِيكُمْ نَارًا}    التحريم :6}

[Ziokoeni nafsi zenu na ahli zenu kutokana na moto”]    [Al-Tahrim:6]

Biashara zako, kuoa kwako kwa ajili ya kujihifadhi ni ibada, kila jambo unalolifanya kwa ajili ya Mwenyezi Mungu unaandikiwa thawabu. Mtume ﷺ ametuambia:

[مَا مِن مُسلم يَغرِسُ غَرْسًا أو يَزرَعُ زَرْعًا فيأكُلُ مِنه طَيرٌ أو إنسَانٌ أو بهيْمَةٌ إلا كان لهُ بهِ صَدقَةٌٌ]     رواه النسائي]

[Hakuna Muislamu yoyote atakayepanda mmea, au atakayelima kisha akala mmea huo binaadamu au ndege ila yule aliyeupanda mti ule mara ya kwanza hupata malipo] [Imepokewa na Al-Nnasai]
Kuondosha udhia katika barabara ni Sadaka na ni ibada, hata ilimu yoyote anayojifundisha mja huwa anapata thawabu iwapo atataka kunufaisha umma ili wafaidike na kwa Manufaa ya Waislamu na Uislamu bora iwe nia yake ni kwa ajili ya Mwenyezi Mungu (Subhanahu wa Ta’aala)

NAMNA YA KUITENGENEZA IBADA NA KUIFANYA KWA YAKINI.

Ewe Muislamu, kuwa na msimamo na udumu katika ibada na usichoke kwani Allah(Subhaanahu wa Taala) Amesema:

{وَاعْبُدْ رَبَّكَ حَتَّىٰ يَأْتِيَكَ الْيَقِينُ} الحجر:99

[Muabudu Mola wako mpaka yakufikie mauti ]    [Al-Hijr:99]

Isiwe hamu yako ni kumaliza ibada au kumalizika, bali hamu iwe ni kuifanya ibada. Mtume ﷺ alikuwa akimwambia Bilali:

[يا بِلاَلُ أَرِحنا بِالصَّلاَةِ]        رواه أحمد

[Ewe Bilal Tupumzishe kwa swalah].   [Imepokewa na Ahmad.]

Na alikuwa akisema:

{وَجعلت قُرَّة عَيْني فِي الصَّلَاة]    رواه النسائي

[Kutulia jicho langu ni katika swala]. [Imepokewa na An-Nasai kutoka kwa Anas. Hata kumuingilia mke wako ni ibada, hii ni neema ya Mola kwa waja wake.]

KUKATAZWA KUTIA UZITO NA KUVUNJA MIPAKA KATIKA IBADA.

Kwani ukiwa na mikazo utashindwa mwishowe, Mtume ﷺ. alipofikiwa na khabari ya “Abdullah bin Umar” ya kuwa usiku anasimama kuswali na mchana anafunga, mkewe akamshitaki. Amesema Mtume ﷺ:
[Hakika Mola wako ana haki juu yako, na Nafsi yako ina haki juu yako, na hakika ahli yako ana haki juu yako, ewe ‘Abdullahi, funga kila mwezi siku tatu, akakataa akasema naweza zaidi ya hizo, akakazana naye Mtume ﷺ mpaka akamfanya kuwa akifunga siku moja na anafungua siku moja, hivi hivi ndio akamueleza kuswali usiku na kusoma Qur-aani]
Na vile vile, kuongeza mambo katika dini ni mja kujisumbua na wala hafikii lengo, kwani amali ndogo yenye kudumu ni bora kuliko amali nyingi ambayo utaifanya siku na siku nyingine utaacha, na Muislamu kuwa na ibada tofauti tofauti ni bora kwani hufanya uhusiano wake na Mola wake uwe na nguvu. Na Mungu atuafikie kila jambo la kheri.

KUMNYENYEKEA MWENYEZI MUNGU NI CHEO NA UTUKUFU

Kwa utukufu wa kunyenyekea kwa Allah ndio Mtume ﷺ akawa ni mtukufu zaidi wa viumbe wa Mwenyezi Mungu na akalingania mlinganio mtukufu nao ni kuwa mja wa Mungu mwenye kunyenyekea. Allah amesema:

{سُبْحَانَ الَّذِي أَسْرَىٰ بِعَبْدِهِ لَيْلًا مِّنَ الْمَسْجِدِ الْحَرَامِ إِلَى الْمَسْجِدِ الْأَقْصَى الَّذِي بَارَكْنَا حَوْلَهُ }    الإسراء:1

[SUBHANA, Ametakasika aliye mchukua mja wake usiku mmoja kutoka Msikiti Mtukufu mpaka Msikiti wa Mbali,]    [Al-Israa:1]
Na Akasema tena:

{تبَارَكَ الَّذِي نَزَّلَ الْفُرْقَانَ عَلَىٰ عَبْدِهِ لِيَكُونَ لِلْعَالَمِينَ نَذِيرا} القرقان :1

[Ametukuka ambaye kwamba amemteremshia Qur-aani mja wake ili apate kuwakhofisha walimwengu”]    [Al-Furqaan:1]

Na ndio alama kubwa ambayo inatakikana ili apate utukufu wa kuwa mja wa Allah mwenye kunyenyekea. Kwa Mtume mwito mtukufu alioitiwa nao ni kuitwa mja wa Allah.

KWA FAIDA ZAIDI SIKILIZA MADA HII NA SHEIKH YUSUF ABDI


Toa maoni yako

Begin typing your search above and press return to search.