0%

https://uongofu.com/wp-content/uploads/2021/06/services-head-1.png

SIKU YA IJUMAA NA HUKMU ZAKE

SIKU YA IJUMAA NA HUKMU ZAKE

Hakika Mwenyezi Mungu ﷻ huumba atakavyo na huchagua atakavyo. Amesema Mwenyezi Mungu ﷻ:

{وَرَبُّكَ يَخْلُقُ مَا يَشَاءُ وَيَخْتَارُ ۗ مَا كَانَ لَهُمُ الْخِيَرَةُ ۚ سُبْحَانَ اللَّهِ وَتَعَالَىٰ عَمَّا يُشْرِكُونَ} القصص: ٦٨}

[Na Mola wako Mlezi huumba na huteuwa atakavyo. Viumbe hawana khiari.] [Al-Qaswas: 68]
Na Mwenyezi Mungu ﷻ ndie anaye jua hekima kwa kila kitu anacho kichagua miongoni mwa viumbe vyake. Mwenyezi Mungu ﷻ huchagua Mitume miongoni mwa Malaika na watu. Na Mwenyezi Mungu ﷻ ameufadhilsha Mji wa Makka kushinda sehemu nyingine. Na akauchagua Mji wa Madina kuwa ni mji aliohamia Mtume ﷺ na Masahaba. Kisha akauchagua Baytul Maqdis akajalia ni sehemu ya Mitume wengi ambayo Mwenyezi Mungu ﷻ ametuelezea habari zao katika Qur’an Tukufu.

Na Mwenyezi Mungu ﷻ amefadhilisha baadhi ya Miezi kuliko mingine na Usiku na Mchana. Akachagua Miezi mine Mitukufu (Dhul-qa’ada, Dhul-hijja, Muharam na Rajab). Na bora wa masiku ni siku ya Ijumaa.

HUKMU YA SWALA YA IJUMAA

Swala ya Ijumaa ni miongoni mwa swala muhimu za faradhi. Na ni wajib kwa kila Muislamu mwanamume ,mwenye akili timamu, alie baleghe ambae hana nyudhuru za kisheria za kumzuia kuetekeleza ibada hiyo.
Na sharia imetia mkazo zaidi na kusisitiza kutekelezwa swala ya ijumaa kwa jamaa. Na malipo yake ni makubwa zaidi.

FADHLA ZA SIKU YA IJUMAA

1. Kupata Thawabu na Malipo kwa kila hatua ya kwenda Msikitini sawa na Mtu aliyesimama kuswali na kufunga Mwaka mzima. Amesema Mtume ﷺ:

[مَنْ اغْتَسَلَ يَوْمَ الْجُمُعَةِ وَغَسَّلَ وَبَكَّرَ وَابْتَكَرَ وَدَنَا وَاسْتَمَعَ وَأَنْصَتَ كَانَ لَهُ بِكُلِّ خُطْوَةٍ يَخْطُوهَا أَجْرُ سَنَةٍ صِيَامُهَا وَقِيَامُهَا]       رواه الترمذي وأحمد

[Mwenye kuoga na kujisafisha, kisha akaenda Msikitini na mapema na akamkurubia Khatibu na akasikiliza kwa utulivu. Mwenyezi Mungu ﷻ atamlipa kwa kila hatua malipo sawa na Mtu aliyesimama kuswali na kufunga Mwaka mzima]      [Imepokewa na Al-Ttirmidhiy na Ahmed].
2. Kusamehewa Madhambi yake ya wiki mzima pamoja na siku tatu za ziada. Amesema Mtume ﷺ:

[مَنْ تَوَضَّأَ فَأَحْسَنَ الْوُضُوءَ ثُمَّ أَتَى الْجُمُعَةَ فَاسْتَمَعَ وَأَنْصَتَ غُفِرَ لَهُ مَا بَيْنَهُ وَبَيْنَ الْجُمُعَةِ وَزِيَادَةُ ثَلَاثَةِ أَيَّامٍ]      رواه مسلم

[Mwenye kutawadha vizuri, kisha akaja Msikitini na akamsikiliza Khatibu na kunyamaza. Anasemehewa Madhambi yake ya wiki mzima pamoja na siku tatu].      [Imepokewa na Muslim.]
3. Kukubaliwa dua katika siku hii tukufu. Amesema ﷺ:

[فِي الْجُمُعَةِ سَاعَةٌ لَا يُوَافِقُهَا عَبْدٌ مُسْلِمٌ قَائِمٌ يُصَلِّي فَسَأَلَ اللَّهَ خَيْرًا إِلَّا أَعْطَاهُ]     رواه مسلم

[Hakika katika Siku ya Ijumaa kuna wakati, haafikiwi Muislamu na wakati huo hali akiwa anamuomba Allah Kheri, ila Mwenyezi Mungi humpatia]. [Imepokewa na Muslim]

ADABU NA SUNNA ZA SIKU YA IJUMAA

1.Kuoga na kujisafisha na kupaka manukato mazuri pamoja na kuondosha harufu mbaya mwilini.. Amesema Mtume  ﷺ:

[مَنْ اغْتَسَلَ يَوْمَ الْجُمُعَةِ غُسْلَ الْجَنَابَةِ ثُمَّ رَاحَ فَكَأَنَّمَا قَرَّبَ بَدَنَةً]     رواه البخاري ومسلم

[Mwenye kuoga siku ya Ijumaa, Josho la Janaba kisha akaenda Msikitini (na mapema.) Mfano wake ni kama mtu aliyetowa sadaka ya Ngamia]     [Imepokewa na Bukhari na Muslim]

2. Kwenda Msikitini mapema na kumkurubia khatibu. Amesema Mtume ﷺ:

[احْضُرُوا الذِّكْرَ ، وَادْنُوا مِنَ الْإِمَامِ ]     رواه أبوداود

[Nedeni mkasali sala ya Ijumaa, na mkae karibu na khatibu].     [Imepokewa na Abuu Daud]

3. Kujishughulisha kwa Kumtaja Allah, kusoma Qur’an, kuomba msamaha, kuomba dua kwa wingi na kumsalia Mtume Muhammad ﷺ.

4. Kumsilikiza Khatibu kwa utulivu, bila ya kujishughulisha na mambo mengine. Asema Mtume ﷺ:

[مَنْ تَوَضَّأَ فَأَحْسَنَ الْوُضُوءَ ثُمَّ أَتَى الْجُمُعَةَ فَاسْتَمَعَ وَأَنْصَتَ غُفِرَ لَهُ مَا بَيْنَهُ وَبَيْنَ الْجُمُعَةِ وَزِيَادَةُ ثَلَاثَةِ أَيَّامٍ]    رواه مسلم

[Mwenye kutawadha vizuri, kisha akaja Msikitini na akamsikiliza Khatibu na kunyamaza. Anasemehewa Madhambi yake ya wiki mzima pamoja na siku tatu]. [Imepokewa na Muslim.]

MAMBO YALIO KATAZWA KATIKA SWALA YA IJUMAA

1. Kuja Msikitini kuchelewa na kukata safu kwa kuruka watu, kwa lengo la kutaka kukaa safu ya mbele. Siku moja Mtume ﷺ alimuona mtu akikata safu na kuruka watu; Akamuambia:

[اجلس فقد آذيت وآنيت]   رواه إبن ماجة

[Kaa chini kwa hakika umewaudhi watu na umechelewa.]     [Imepokewa na Ibnu Maajah]

2. Kuwashawishi waja wa Mwenyezi Mungu, kwa kusoma Qur’an kwa sauti kubwa, au kufanya Dhikri kwa sauti ya juu. Mtume ﷺ aliwakataza Masahaba kusoma kwa sauti ya juu, na akawambia; Asisome mmoja wenu Qura’n kwa sauti ya juu kuliko mwingine.

3. Kuzungumza wakati wa Khatibu anatoa khutbah ya Ijumaa. Amesema Mtume ﷺ:

[من قال لصاحبه يوم الجمعة والإمام يخطب أنصت فقد لغا]     رواه النسائي

[Ukimuambia mwenzako nyamaza na Khatibu akiwa anazungumza, amefanya upuzi].   [Imepokewa na Al-Nnasaai]

KHATARI YA KUACHA SWALA YA UJUMAA

Mtume Muhammad ﷺ Amesisitiza na kutilia mkazo juu la suala la kutekeleza swala ya Ijumaa. Na akawatahadharisha Waislamu wanaoacha kutekeleza swala hii. Adhabu kubwa watakayo pata watu hao hapa duniani ni nyoyo zao kuwa ngumu na kupigwa muhuri wa kughafilika. Amesema Mtume ﷺ:

[لينتهين أقوام عن ودعهم الجمعات، أو ليختمن الله على قلوبهم، ثم ليكونن من الغافلين]   رواه مسلم وأحمد والنسائي

[Hawataendelea watu kuacha swala ya Ijumaa, mpaka Mwenyezi Mungu apige muhuri nyoyo zao, kisha watakuwa niwenye kuishi katika mughafala].  [Imepokewa na Muslim na Ahmad na Al-Nnasaai]
Ndugu Muislamu, tujihadhari sana na kuacha swala ya Ijumaa, kwasababu adhabu yake ni nzito sana. Moyo ukiwa mgumu, basi mwanadamu anakuwa sawa na myama, hajali lolote wala chochote. Utamuona hamuogopi Mwenyezi Mungu, kwa kufanya maasi usiku na mchana.
Tunamuomba Allah Subhaanahu wa Taala athibitishe nyoyo zetu juu ya twaa yake, na atulinde na machafu yote.

 KWA FAIDA SIKILIZA MADA HII NA SHEIKH HASSAN SUGO

Toa maoni yako

Begin typing your search above and press return to search.