SIKU AMBAZO NI SUNNA KUFUNGA
Siku ambazo kwamba ni sunna kufunga.
1. SIKU SITA ZA MWEZI WA SHAWWAAL. (Mfungo mosi)
Kwa kauli ya Mtume ﷺ:
[مَن صام رمضان ثم أتبَعَه ستًّا من شوَّال، كان كصيام الدهر] رواه مسلم
[Atakayefunga Ramadhani, kisha akafuatiliza kwa kufunga siku sita za Shawwaal, itakuwa ni kama aliyefunga mwaka mzima] [Imepokewa na Muslim.].
Sawasawa awe amezifunga siku sita hizi kwa pamoja kufuatana au siku mbalimbali zisizofuatana.
2. KUFUNGA SIKU TISA ZA MWANZO WA MWEZI WA DHULHIJJA. (Mfungo tatu)
Kwa kauli ya Mtume ﷺ:
ما من أيام العمل الصالح فيها أحب إلى الله من هذه الأيام ـ يعني أيام العشر ـ قالوا يا رسول الله ولا الجهاد في سبيل الله ؟ قال ولا الجهاد في سبيل الله إلا رجل خرج بنفسه وماله ثم لم يرجع من ذلك بشيء رواه البخاري
[Hakuna masiku ambayo matendo mema ni bora zaidi mbele ya Mwenyezi Mungu kuliko masiku haya (yaani masiku kumi ya Dhulhijjah) ] wakasema (maswahaba): hata jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu? Akema (Mtume ﷺ): [Hata jihadi kwa njia ya Mwenyezi Mungu, isipokuwa mtu aliyetoka (kwenda jihadi) yeye mwenyewe na mali yake, wala asirudi na chochote (yaani akafa vitani)] [Imepokewa na Bukhari.].
Na masiku haya yakatiliwa nguvu zaidi na siku ya A’rafa kando na hajj – nayo ni siku ya tisa ya mwezi wa Dhulhijjah; kwa kauli ya Mtume ﷺ:
[صِيَامُ يَوْمِ عَرَفَةَ أَحْتَسِبُ عَلَى اللَّهِ أَنْ يُكَفِّرَ السَّنَةَ الَّتِي قَبْلَهُ وَالسَّنَةَ الَّتِي بَعْدَهُ] رواه مسلم
[Kufunga siku ya A’rafa nataraji kwa Mwenyezi Mungu kusamehewa mtu madhambi ya mwaka kabla yake, na mwaka uliyo baada yake] [Imepokewa na Muslim.].
3. KUFUNGA SIKU YA A’SHURAA NA SIKU KABL YAKE.
A’shuura: Ni siku ya kumi katika mwezi wa Muharam (Mfungo nne).
Kwa kauli ya Mtume ﷺ:
[وَصِيَامُ يَوْمِ عَاشُورَاءَ أَحْتَسِبُ عَلَى اللَّهِ أَنْ يُكَفِّرَ السَّنَةَ الَّتِي قَبْلَهُ] رواه مسلم
[Na kufunga siku ya A’shuura nataraji kwa Mwenyezi Mungu kusamehewa kwa mtu madhambi ya mwaka uliyo kabla yake] [Imepokewa na Muslim.].
Na sababu ya kufunga siku hii ni kama ilivyothibiti kutoka kwa Abdillahi ibn Abbas anasema: (Aliingia Madina Mtume ﷺ akawaona Mayahudi wamefunga siku ya A’shuura, akasema Mtume: Ni nini hiki (mnachofanya)? Wakasema: Hii ni siku njema, siku hii ndiyo siku Mwenyezi Mungu aliyowaokoa wana israili kutokamana na maadui zao, basi akaifunga siku hii Nabii Musa. Akasema Mtume:
[فَأَنَا أَحَقُّ بِمُوسَى مِنْكُمْ فَصَامَهُ وَأَمَرَ بِصِيَامِهِ]
[Basi mimi nina haki zaidi kwa Musa kuliko nyinyi, akaifunga Mtume siku hiyo na akaamrisha watu kuifunga] [Imepokewa na Bukhari.].
Na inapendekezwa vile vile kufunga siku ya tisa, kwa ilivyo pokelewa kutoka kwa Mtume ﷺ Alisema
[لَئِنْ عِشْتُ إلَى قَابِلٍ لأَصُومَنَّ التَّاسِعَ] رواه مسلم
[Lau nitaishi mpaka Mwaka ujao nitafunga siku ya tisa] [Imepokewa na Muslim.]
4. KUFUNGA MASIKU MEUPE YA KILA MWEZI.
Nayo ni tarehe kumi na tatu, na kumi na nne, na kumi na tano ya kila mwezi katika miezi ya kiislamu, na yameitwa meupe; kwasababu usiku wa masiku haya hunga’ra kwa mwangaza wa mwezi.
Kama ilivyothibiti kutoka kwa AbdulMalik ibn Minhal kutoka kwa babake: Kwamba (babake) alikuwa pamoja na Mtume ﷺ akasema (kumwambia mwanaye – AbdulMalik): Alikuwa Mtume ﷺ akiwaamrisha kufunga masiku meupe, na akisema: (Masiku) haya ni saumu za mwaka) [Imepokewa na Ibnu Hibbaan.]
5. KUFUNGA SIKU YA JUMATATU NA ALHAMISI KILA WIKI.
Kama ilivyopokewa kutoka kwa Abu Hureira t kwamba Mtume ﷺ amesema:
[تُعْرَضُ الأَعْمَالُ يَوْمَ الاثْنَيْنِ وَالْخَمِيسِ ؛ فَأُحِبُّ أَنْ يُعْرَضَ عَمَلِي وَأَنَا صَائِمٌ] رواه الترمذي
[Hupandishwa matendo (juu kwenda mbinguni) kila jumatatu na alhamisi, basi napenda matendo yangu yapandishwe hali ya kuwa nimefunga] [Imepokewa na Tirmidhi.].
6. KUFUNGA SIKU MOJA NA KULA SIKU NYINGINE
Kutoka kwa Abdillahi ibn A’mru Radhi za Allah ziwe juu yake Anasema: Amesema Mtume ﷺ:
[إن أفضل الصيام صيام داود كان يصوم يوماً ويفطر يوماً] اخرجه البخاري ومسلم
[Hakika saumu ya kupendeza sana mbele ya Mwenyezi Mungu ni saumu ya Daud, na alikuwa akifunga siku moja na kula siku moja] [Imepokewa na Bukhari na Muslim.].
7. KUFUNGA MWEZI WA MUHARAM (Mfungo nne).
Kutoka kwa Abu Hureira t Anasema: Amesema Mtume ﷺ:
[أَفْضَلُ الصِّيَامِ بَعْدَ رَمَضَانَ شَهْرُ اللَّهِ الْمُحَرَّمُ] رواه مسلم
[Saumu ilio bora baada ya Ramadhani ni saumu ya mwezi wa Muharam] [Imepokewa na Muslim.].
8. KUFUNGA MWWEZI WA SHABANI.
Kutoka kwa Usama ibn Zaid Radhi za Allah ziwe juu yake Asema: Nilisema: [Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, sijapata kukuona ukifunga mwezi wowote mfano wa unavyofunga Shabani. Akasema:
[ذَلِكَ شَهْرٌ يَغْفُلُ النَّاس عَنْهُ بَيْنَ رَجَبٍ وَرَمَضَان , وَهُوَ شَهْر تُرْفَعُ فِيهِ الأَعْمَال إِلَى رَبّ الْعَالَمِينَ ، فَأُحِبُّ أَنْ يُرْفَعَ عَمَلِي وَأَنَا صَائِمٌ]
[Kwa sababu huo ndio mwezi ambao watu wanaghafilika kati ya Rajabu na Ramadhani, na ndio mwezi ambao matendo hupandishwa juu kwa Mola wa walimwengu, basi napenda matendo yangu yapandishwe hali ya kuwa nimefunga] [Imepokewa na Nasaai.na Abuu Dawuud].
Ama Katazo lililo kuja katika hadithi ya Mtume ﷺ Inayo sema
[إِذَا انْتَصَفَ شَعْبَانُ فَلا تَصُومُوا] رواه أبو داود والترمذي
[Ifikapo nusu mwezi wa shabani Musifunge] [Imepokewa na Abuu Dawud wa At Tirmidhiy.]
inachukuliwa ni kwa Yule anae khusisha nusu ya mwisho wa shabani kwa kufunga, au kutounganisha shabani na Ramadhani, ama Yule alifunga mwanzo wa shabani, wala asikhusishe mwisho wa shabani wala asiunganisha na ramadhani hapana ubaya kwa mtu huyu kufunga au kwa yule ambae alikuwa na ada ya kufunga siku ya Juma tatu na Al hamisi.