SOMO LA FIQHI
Saumu ya Ramadhani ina nguzo mbili za msingi, ambazo kusihi kwa saumu kunazitegemea.
Nguzo ya kwanza: Ni kutia nia: nao ni kuazimia kufunga mwezi wa Ramadhani. Na nia mahala pake ni moyoni na sio lazima kwa ulimi. Na wala haikupokelewa kwa Mtume kuwa alikuwa akiitemka nia na vile vile haikupokelewa kwa Maswahaba wake watukufu.
Kwa neno lake Mtume ﷺ:
[إِنَّما الأَعْمَالُ بالنِّيَّاتِ وإنَّما لكُلِّ امْرِىءٍ ما نَوَى ] رواه البخاري ومسلم
[Hakika kila jambo analolifanya (mwanadamu) ni kulingamana na nia yake, na hakika kila mtu atalipwa kulingana na alivyonuilia] [Imepokewa na Bukhari na Muslim.]
Na kwa neno lake Mtume ﷺ:
[من لم يبيت الصيام من الليل فلا صيام له] رواه الترمذي
[Asiyeleta nia ya swaumu usiku, hana swaumu]. [Imepokelewa na Tirmidhiy]
Na uwajibu huu wa kutia nia ni kwa upande wa saumu ya fardhi tu. Ama saumu za sunna, nia inatosha hata baada ya kuingia kwa mchana maadamu mtu hajatenda lo lote miongoni mwa yabatilishayo saumu.
عائشة رضي الله عنه : دخل علي رسول الله صلى الله عليه وسلم ذات يوم ، فقال : [هل عندكم شيء ؟ ] قلنا : لا . قال :[ فإني صائم ] . رواه مسلم
Imepokelewa kutoka kwa Bibi Aysha-Allah amuwiye radhi-kwamba Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie aliingia kwake siku moja na kuuliza: [Je, mna cho chote?] Nikamjibu: Hapana, akasema: [Basi hakika mimi nimefunga]. [Imepokewa na Muslim]
Nguzo ya pili: Nikujizuia na yote yenye kuharibu Saumu tokea kuchomoza kwa alfajiri mpaka kuzama kwa jua, kwa ushahidi wa neno lake Allah Mtukufu:
{وَكُلُوا وَاشْرَبُوا حَتَّىٰ يَتَبَيَّنَ لَكُمُ الْخَيْطُ الْأَبْيَضُ مِنَ الْخَيْطِ الْأَسْوَدِ مِنَ الْفَجْرِ ۖ ثُمَّ أَتِمُّوا الصِّيَامَ إِلَى اللَّيْلِ ۚ} البقرة:187
“Na kuleni na kunyweni mpaka ubainike kwenu weupe wa alfajiri katika weusi wa usiku. Kisha timizeni Saumu mpaka usiku. [2:187]