0%

https://uongofu.com/wp-content/uploads/2021/06/services-head-1.png

MIONGONI MWA ADABU ZA KUSWALI

SOMO LA FIQHI

Swala ni ibada kuu Muhimu, Muislamu katika ibada hiyo anaelelekea kwa moyo wake na mwili wake kwa Mwenyezi Mungu Aliyetukuka. Hivyo basi inatakikana itanguliwe na matayarisho ya kiroho na ya kimwili, ili aingie katika swala akiwa hana kitu cha kumshughulisha na aitekeleze kwa njia sahihi, na kwa hivyo imewekewa mambo yafuatayo:

1. IKHLAAS (kumtakasia Mwenyezi Mungu)

Mwenyezi Mungu Mtukufu Anasema:

{وَمَا أُمِرُوا إِلَّا لِيَعْبُدُوا اللَّهَ مُخْلِصِينَ لَهُ الدِّينَ حُنَفَاءَ وَيُقِيمُوا الصَّلَاةَ وَيُؤْتُوا الزَّكَاةَ ۚ وَذَٰلِكَ دِينُ الْقَيِّمَةِ}   البينة:5

[Nao hawakuamrishwa kitu ila wamuabudu Mwenyezi Mungu kwa kumtakasia Dini, wawe waongofu, na washike Sala, na watoe Zaka. Na hiyo ndiyo Dini madhubuti.]    [Al-Bayinah: 5].

Na Mwenyezi Mungu hakubali amali njema yoyote isipokuwa ibada ya kutakasiwa Yeye, isiyokua na kujionyesha wala kutaka sifa wala aina yoyote ya kumshirikisha Mwenyezi Mungu.

2. KUENEZA MAJI KWENYE VIONGO VYA KUTAWADHA

Nako ni kutawadha vizuri kwa njia kamilifu.

Abu Huraira Radhi za Allah ziwe juu yake alipokewa akisema kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu ﷺ alisema:

أَلاَ أَدُلُّكُمْ عَلَى مَا يَمْحُو الله بِهِ الْخَطَايَا وَيَرْفَعُ بِهِ الدَّرَجَاتِ؟” قَالُوا: بَلَى. يَا رَسُولَ اللّهِ! قَالَ: “إِسْبَاغُ الْوُضُوءِ علَى الْمَكَارِهِ. وَكَثْرَةُ الْخُطَا إِلَى الْمَسْاجِدِ. وَانْتِظَارُ الصَّلاَةِ بَعْدَ الصَّلاَةِ. فَذلِكُمُ الرِّبَاطُ      رواه مسلم

[Je, siwajulishi nyinyi kitu ambacho kwacho Mwenyezi Mungu hufuta dhambi na hupandisha daraja? Wakasema: “ kwani? Tujulishe, ewe Mtume wa Mwenyezi mungu!” Akasema: Ni kueneza maji kwenye viungo vile itakikanavyo katika kutawadha, kukithirisha hatua za kwenda misikitini, na kungojea Swala baada ya Swala, kwani huko ndiko kujifunga kwenye utiifu wa Mwenyezi Mungu]   [Imepokewa na Muslim.]

3. KUTOKA MAPEMA KWA AJILI YA SWALA

Nako ni kutoka mapema ili kupata fadhila za kungojea Swala. Abu Huraira  amepokewa akisema kwamba Mtume wa Mwenyezi mungu  amsema:

[لَا يَزَالُ أَحَدُكُمْ فِي صَلَاةٍ مَا دَامَتْ الصَّلَاةُ تَحْبِسُهُ لَا يَمْنَعُهُ أَنْ يَنْقَلِبَ إِلَى أَهْلِهِ إِلَّا الصَّلَاةُ]    رواه مسلم

[Mmoja wenu huzingatiwa anaendelea kuwa kwenye Swala kwa mda ambao anasubiri swala haimzui yeye kwenda kwa jamaa zake ila Swala]    [ Imepokewa na Bukhari.].

4. KUMTAJA MWENYEZI MUNGU

Amtaje Mwenyezi Mungu anapotoka nyumbani kwa kusema:

بسم اللَّهِ، توكَّلْتُ عَلَى اللَّهِ، اللَّهُمَّ إِنِّي أعوذُ بِكَ أنْ أَضِلَّ أو أُضَلَّ ، أَوْ أَزِلَّ أوْ أُزلَّ ، أوْ أظلِمَ أوْ أُظلَم ، أوْ أَجْهَلَ أو يُجهَلَ عَلَيَّ

[Kwa jina la Mwenyezi Mungu, nimetegemea kwa Mwenyezi Mungu, Hapana hila za kujiepusha na maasia wala nguvu za kufanya mambo ya utiifu isipokuwa ni kwa msaada wa Mwenyezi Mungu Ewe Mola! Mimi najilinda kwako ni sipotee au nipoteze, au niteleze au niwafanye watu wateleze, au nidhulumu au nidhulumiwe, au nikosee au nikosewe]   [Imepokewa na Abu Daud na At Tirmidhi]

Na amtaje Mwenyezi Mungu anapokwenda msikitini kwa kusema:

اللهم اجعل في قلبي نوراً ، وفي لساني نوراً ، وفي سمعي نوراً ، وفي بصري نوراً ، ومن فوقي نوراً ، ومن تحتي نوراً ، وعن يميني نوراً ، وعن شمالي نوراً ، ومن أمامي نوراً ، ومن خلفي نوراً  ، و اجعل في نفسي نوراً ، وأعظم لي نوراً ، وعظم لي نوراً ، واجعل لي نوراً ، واجعلني نوراً ، اللهم أعطني نوراً ، واجعل في عصبي نوراً ، وفي لحمي نوراً ، وفي دمي نوراً ، وفي شعري نوراً ، وفي بشري نوراً

[Ewe Mwenyezi Mungu, weka katika moyo wangu nuru, na katika ulimi wangu nuru, na katika masikio yangu nuru, na katika macho yangu nuru, na juu yangu nuru, na chini yangu nuru, na kuliani kwangu nuru, na kushotoni kwangu nuru, na mbele yangu nuru, na nyuma yangu nuru, na weka katika nafsi yangu nuru, na nifanyie kubwa nuru, na nifanyie nyingi nuru, na uniwekee mimi nuru, na unifanyie mimi nuru, Ewe Mwenyezi Mungu nipe nuru, na uweke  katika  mishipa yangu nuru, na katika  nyama  yangu nuru, na katika damu yangu nuru, na katika nywele zangu nuru, na katika ngozi yangu nuru, (Ewe Mwenyezi Mungu  niwekee nuru katika kaburi langu, na nuru katika mifupa yangu) (Na unizidishie nuru, na unizidishie nuru, na unizidishie nuru) (na unipe nuru juu ya nuru. )]   [Imepokewa na Bukhari na Muslim.].

5. KWENDA MSIKITINI KWA UTULIVU NA UPOLE

Kwa kauli yake Mtume ﷺ:

إِذَا سَمِعْتُمْ الْإِقَامَةَ ، فَامْشُوا إِلَى الصَّلَاةِ ، وَعَلَيْكُمْ بِالسَّكِينَةِ وَالْوَقَارِ ، وَلَا تُسْرِعُوا ، فَمَا أَدْرَكْتُمْ ، فَصَلُّوا ، وَمَا فَاتَكُمْ فَأَتِمُّوا    رواه البخاري ومسلم

[Mkisikia swala inakimiwa, nendeni kuswali, na kuweni na utulivu [ Sakinah: Utulivu na upole katika kwenda. na umakini na msiende haraka, mnachokipata kiswalini na kinachowapita kitimizeni]     [Imepokewa na Bukhari na Muslim.]

6. KUMTAJA MWENYEZI MUGNU WAKATI WA KUINGIA NA KUTOKA MSIKITINI

Atangulize mguu wake wakulia wakati wakuingia msikitini na aseme:

[أعوذ بالله العظيم ،وبوجهه الكريم ،وسلطانه القديم ،من الشيطان الرجيم]

[Najilinda kwa Mwenyezi Mungu Mkubwa, na kwa uso wake mtukufu na mamlaka yake ya tangu na tangu, kutokana na Shetani aliyefukuzwa kwenye rehema ya Mwenyezo Mungu] [Imepokewa na Abu Daud.]

[بسم الله ،والصلاة والسلام على رسول الله اللهم افتح لي أبواب رحمتك]

[Na ingia kwa jina la Mwenyezi Mungu na kumuombea rehema na amani Mtume wa Mwenyezi mungu Ewe Mola! Nifungulie milango ya rehema zako]    [Imepokewa na Muslim.]

Na atangulize mguu wake wakushoto wakati wa kutoka msikitini na aseme:

[بِسمِ الله وَالصّلاةُ وَالسّلامُ عَلى رَسولِ الله، اللّهُـمَّ إِنّـي أَسْأَلُكَ مِـنْ فَضْـلِك، اللّهُـمَّ اعصِمْنـي مِنَ الشَّيْـطانِ الرَّجـيم]

[Natoka kwa jina la Mwenyezi Mungu na kumuombea rehema na amani Mtume wa Mwenyezi Mungu. Ewe Mola! Mimi nakuomba fadhila zako. Ewe Mola! Nilinde mimi kutokana na Shetani]     [Imepokewa na Muslim.]

7. ASIKAE MPAKA ASWALI RAKAA MBILI

Kwa kauli yake Mtume ﷺ:

[إذا دخل أحدكم المسجد، فليركع ركعتين قبل أن يجلس]     متفق عليه

[Anapoingia mmoja wenu msikitini, aswali rakaa mbili kabla hajakaa]    [Imepokewa na Bukhari na Muslim]

8. KUJIEPUSHA NA KUSHIKANISHA VIDOLE

Kwa kauli yake Mtume :

[إِذَا تَوَضَّأَ أَحَدُكُمْ فَأَحْسَنَ وُضُوءَهُ ثُمَّ خَرَجَ عَامِدًا إِلَى الْمَسْجِدِ فَلا يُشَبِّكَنَّ يَدَيْهِ ، فَإِنَّهُ فِي صَلاةٍ]    رواه أبوداود

[Anapotawadha mmoja wenu vizuri kisha akatoka kukusudia msikitini, basi na asivishikanishe vidole vyake kwakuwa yeye yuko katika Swala]   [Imepokewa na Abu Daud.]

9. KUJISHUGHULISHA NA KUMTAJA MWENYEZI MUNGU

Kujishughulisha kumtaja Mwenyezi Mungu, kuomba dua na kusoma Qur’ani wakati wa kungojea Swala bila kuwafanyia fujo wenye kuswali.

10. KUWA MNYENYEKEVU KATIKA SWALA

Unyenyekevu ndio kiini cha Swala na roho yake. Swala bila ya unyenyekevu wala kuhudhurisha moyo ni kama mwili uliokufa. Ibnu Rajab, Mwenyezi Mungu amrehemu, alisema: “Asili ya unyenyekevu ni moyo kulainika na kuwa nyororo, kutulia, kuwa mnyonge, kujivunjavunja na kupishika. Basi moyo ukinyenyekea viungo vyote huufuata moyo, kwa kuwa hivyo vinauandama na kuufuata moyo”   [Al-Khushuu’ cha ibnu Rajab.].

Basi unyenyekevu mahali pake ni moyo, na ulimi wake wenye kueleza ni viungo.

11. KUJILAZIMISHA NA SUNNA YA MTUME ﷺ KATIKA SWALA YAKE YOTE

Swala ni ibada ambayo ni lazima kufuata, kusifanywe chochote wala kusisemwe lolote katika Swala ambalo Mtume ﷺ hakulifanya wala hakulisema, kwa neno lake Mtume ﷺ:

[صلوا كما رأيتموني أصلي]     رواه البخاري 

[Swalini kama vile mlivyoniona nikiswali]   [Imepokewa na Bukhari. ]

Toa maoni yako

Begin typing your search above and press return to search.