SOMO LA FIQHI
Mwenye kuswali anaruhusiwa kisheria kufanya baadhi ya mambo akiwa ndani ya swala, kwa sharti kwamba kuwe na dharura ya kufanya hivyo.
Anaruhusiwa kuyafanya mambo hayo katika hali hiyo ya dharura bila ya swala yake kubatilika. Mambo hayo ni kama yafuatavyo:-
1. Kutembea katika Swala kwa tukio muhimu kwa sharti ya kutogeuka upande wa kibla kama kufunguwa mlango kama alivyofanya Mtume kwa Hadithi aliyoipokea Bibi Aisha radhi za Allah ziwe juu yake Asema:
كان رسولُ الله صلَّى الله عليه وسلَّم يصلِّي في البيت والبابُ عليه مغلق، فجِئتُ فاستفتحتُ، فمشى ففتح لي، ثم رجعَ إلى مُصلاَّ أخرجه أبوداو والنسائي
[Mtume ﷺ alikuwa akiswali Nyumbani na mlango ulikuwa umefungwa nilikuja kuufungua,(nikashindwa) akaja kunifungulia kisha akarudi kwenye Mswala wake] [Imepokewa na Abuu Daud na An Nasai]
2. Kubeba mtoto katika Swala
Amepokea Abuu Qatada Radhi za Alla ziwe juu yake amesema:
رأيتُ النبِيَّ صلَّى الله عليه وسلَّم يؤمُّ النَّاس، وعلى عاتقِه أمامةُ بنت زينب، فإذا ركَع وضَعها، وإذا رفع من السُّجود أعادَها رواه البخاري ومسلم
[Nilimuona Mtume rehma na amani zimfike yeye akiswalisha watu,na (amembemba) kwenye mabega yake Umaamah bint Zaynab, Alikuwa ikirukuu akimuweka na ikiinika kutoka kwenye Sijda akimrudisha (kumbeba)] [Imepokewa na Bukhari na Muslim]
3. Kuuwa nyoka na n’nge katika Swala.
Mtume ﷺ Ameamrisha kuuwa vyeusi viwili ndani ya Swala nyoka na nge [Imepokewa na Abuu Daud na An Nasaai na Ibnu Maajah]
4. Kuzunguka katika Swala kwa dharura.
Amepokea Jaabir radhi za Allah ziwe juu yake amesema: Mtume ﷺ aliposhikika na Ugonjwa Tuliswali Nyuma yake na yeye alikuwa amekaa akatuzungukia akatuona Tumesimama akatuashiria (kukaa) tukakaa] [Imepkewa na Muslim na Abuu Daud]
Ama kuzunguka bila ya Dharura ni Makruhi kwa sababu ni kinyume na Unyenyekevu katika Swala.
5. Kulia katika Swala
Alikuwa [Mtume ﷺ wa Mwenyezi Mungu akiswali na kwenye kifua chake kuna Sauti kama sauti ya Chungu kwa ajili ya kulia] [Imepokewa na Abuu Daud na An Nasai]
6. Kuleta tasbihi kwa wanaume na kupiga makofi kwa wanawake
Amesema Mtume ﷺ:
[مَن نابَه شيءٌ في صلاته، فلْيُسبِّح؛ فإنَّما التَّصفيق للنِّساء] رواه البخاري ومسلم
[Atakayepatwa na jambo ndani ya swala yake na aseme: Sub-haanallah,ama kupiga makofi ni kwa wanawake] [Imepokewa na Bukhari na Muslim]
7. Kumfunguza Imamu anapo sahau katika kisomo
Amepokea Ibnu Umar radhi za Allah ziwe juu yake Asema Mtume ﷺ aliswali swala na akasoma akachangana (kisomo) alipo maliza akamuliza Ubayyah je uliswali pamoja na sisi?? akasema ndio akamwambia: Ni nini kilikuzuia? (Kunirekebisha nilipo changaya kisomo) [Imepokewa na Abuu Daud na Isnadi yake ni Hasan]
8. Kuashiria kwa Mkono kwa ajili ya kurudisha salamu
Amepokea Ibnu Umar radhi za Allah ziwe juu yake asema nilimuliza Bilal Mtume akirudisha vipi salamu anaposwalimiwa akiwa katika swala? akasema (Bilal) alikuwa akiashiria kwa mkono wake. [Imepokewa na Abuu Daud na At Tirmidhiy]
9. Kutoa ishara ya kufahamisha kwa anae swali wakati akitokewa na haja
10. Kumshukuru Mwenyezi Mungu anapoona linalo kupelekea kufanya hivyo
11. Kutema mate na kohozi katika Swala upande wakushoto
12. Kumzuia anaepita mbele ya mwenye kuswali
Kwa kauli ya Bwana Mtume ﷺ:
إذا كان أحَدُكم يُصلِّي، فلا يدَعْ أحدًا يمرُّ بين يدَيْه، ولْيَدرأه – (يعني ليدفعه) – ما استطاع، فإنْ أبَى فلْيُقاتله؛ فإنَّما هو شيطان
[Atakaposwali mmjoa wenu kuelekea kitu (kinachomsitiri na watu,) asimuachie mtu kupita mbele yake na amzuie kwa kadri ya uwezo wake, Akikataa basi na amzuie kwa nguvu, kwani huyo ni shetani]. [Imepokewa na Bukhari na Muslim]
Kwa ujumla inafaa kufanya kila tendo ambalo halipingani na adabu, suna au unyenyekevu wa swala. Kama vile mtu kujikuna na kadhalika, isipokuwa tu anafaa kufanya haya tulioeleza kwa Dharura anapokuwa na haja ya kufanya hivyo.