0%

https://uongofu.com/wp-content/uploads/2021/06/services-head-1.png

MAANA YA FIDIA NA HUKMU ZAKE

SOMO LA FIQHI


Maana ya fidia
Ni kitu kinachomlazimu mwnye kuhiji au mwenye kufanya Umra kwa sababu ya kuacha tendo la wajibu au kufanya tendo lililokatazwa

Kwanza: Fidia ya kuacha tendo la wajibu
Mwenye kuacha wajibu miongoni mwa wajibu za Hija au Umra, kama aliyeacha kulala Muzdalifa au kunyoa au nyinginezo, itamlazimu fidia, nayo ni kuchinja mnyama.

Na mnyama anayekusudiwa ni fungu moja kati ya mafungu saba ya ngamia au ng›ombe au ni mbuzi aliyemaliza mwaka mmoja au kondoo aliyepita miezi sita. Atachinja katika Haramu ya Makka na nyama yake atagawia mafukara wa Makka.

Akikosa mnyama wa kuchinja, atafunga siku kumi: siku tatu akiwa Hija ikiwezekana, na siku saba arudipo kwa watu wake. Mwenyezi Mungu Mtukufu Anasema:

فَمَن لَّمۡ يَجِدۡ فَصِيَامُ ثَلَٰثَةِ أَيَّامٖ فِي ٱلۡحَجِّ وَسَبۡعَةٍ إِذَا رَجَعۡتُمۡۗ تِلۡكَ عَشَرَةٞ كَامِلَةٞۗ ذَٰلِكَ لِمَن لَّمۡ يَكُنۡ أَهۡلُهُۥ حَاضِرِي ٱلۡمَسۡجِدِ ٱلۡحَرَامِۚ وَٱتَّقُواْ ٱللَّهَ وَٱعۡلَمُوٓاْ أَنَّ ٱللَّهَ شَدِيدُ ٱلۡعِقَابِ     البقرة: 196

[Asiyepata (cha kuchinja) atafunga siku tatu huko Hija na siku saba mtakaporudi. Hizo siku kumi kamili. Hukumu hiyo ni kwa yule watu wake si wakazi wa eneo la Msikiti wa Haram. Na mcheni Mwenyezi Mungu, hakika Mwenyezi Mungu ni Mkali wa kutesa]        [2: 196].

Pili: Fidia ya kufanya tendo lililokatazwa
1. Fidia ya kuvaa nguo ya mzunguko, kufinika kichwa, kujitia manukato, kunyoa nywele na kukata kucha.
Mwenye kufanya mojawapo ya matendo haya atachaguzwa baina ya mambo matatu:

A. Kufunga siku tatu.

B. Kuwalisha masikini sita, kila masikini nusu ya pishi ya chakula kama mchele na mfano wake.

C. Kuchinja mbuzi.

Dalili ni neno la Mwenyezi Mungu Aliyetukuka:

وَلَا تَحۡلِقُواْ رُءُوسَكُمۡ حَتَّىٰ يَبۡلُغَ ٱلۡهَدۡيُ مَحِلَّهُۥۚ فَمَن كَانَ مِنكُم مَّرِيضًا أَوۡ بِهِۦٓ أَذٗى مِّن رَّأۡسِهِۦ فَفِدۡيَةٞ مِّن صِيَامٍ أَوۡ صَدَقَةٍ أَوۡ نُسُكٖۚ}  البقرة: 196}

[Na msinyoe vichwa vyenu mpaka wanyama waliotunukiwa kwa ibada ya Hija wafike mahali pa kuchinjwa. Basi mtu atakayekuwa mgonjwa, au ana vitu vya kumkera kichwani mwake, atatoa fidia ya kufunga, kutoa sadaka au kuchinja]    [2: 196].

Na neno la Mtume ﷺ kumwambia Ka’b bin ‘Ujrah Radhi za Allah ziwe juu yake na yeye yuko kwenye ihramu: (Je, hao niwadudu wa kichwani mwako?). Akasema: “Ndio”. Mtume (saw) akamwambia: (Nyoa kichwa chako kisha uchinje mbuzi ikiwa ni ibada au funga siku tatu au lisha masikini sita pishi tatu za tende).

Mwenye kufanya katazo miongoni mwa makatazo matano yaliyotajwa kwa kukusudia, au akahitaji kulifanya na akalifanya, kama ilivyotokea kwa Ka’b radhi za Allah ziwe juu yake, basi atatoa fidia ya kero.

Na mwenye kufanya lolote miongoni mwa haya yaliyokatazwa kwa kusahau, basi hana makosa

Kunyoa nyweleKukata kuchaKujipaka manukatoKuvaa nguo ya kushonwaKufunika kichwa kwa kitu cha kushika
2. Fidia ya kustarehe sehemu isiyokuwa tupu ya mbele na kuundama katika Hija baada ya tahaluli ya kwanza (kujitoa ka kwanza kwenye vikwazo vya kuhirimi)
Hii fidia yake ni kama ile ya kero iliyotangulia

3. Fidia ya mtu kuundama akiwa Hija kabla ya tahaluli ya kwanza.
Nayo ni kuchinja ngamia. Akikosa atafunga siku tatu katika Hija na siku saba anaporudi kwa watu wake, na hija yake itakuwa imeharibika, na itamlazimu aikamilishe na ailipe mwaka unaokuja.

4. Fidia ya mtu kuundama katika Umra
Nayo ni mbuzi au kondoo, na Umra yake itakuwa imeharibika. Na itamlazimu ailipe.

5. Fidia ya kuua kiwindwa:
Kikiwa kiwindwa kina mfano, Aliyewinda atachaguzwa baina ya kutoa mfano, au kukitia kima (thamani) na kununua kwa kima hicho chakula na kukigawanya kwa mifuto (vibaba): kila masikini mifuto miwili  Nusu ya pishi nikipimo 1020 grm], au afunge kwa kila mifuto miwili siku moja.

Makusudio ya kiwindwa ni kile chenye mfano. Yaani: kuna mnyama mwenye kufanana nacho kiasi fulani, na sio kufanana kikamilifu, kwani kufanana namna hiyo haimkiniki.

Mfano wa hilo: Lau mtu aliwinda mbuni, basi itampasa achinje ngamia mmoja, sababu mbuni anafanana na ngamia, au amtie thamani ngamia na anunue kwa thamani yake chakula kama vile mchele au mahindi, na amlishe kila masikini mifuto miwili ya hiko chakula, au afunge kwa kila mifuto miwili siku moja. Na lau aliwinda pundamilia, basi itamlazimu ng’ombe na namna hiyo.

Na iwapo kiwindwa hakina mfano miongoni mwa wanyama hoa, kama vile nzige na kisigi (ndege mdogo), basi atapewa hiari baina ya kununua chakula kwa thamani ya kile kiwindwa na kuwalisha masikini au afunge kwa kila mifuto miwili siku moja. Na wenye kukitia thamani ni watu wawili waadilifu.

Haifai kufungisha ndoa kwa mwenye kuhiji na mwenye kufanya umra wala hana fidiya mwenye kufanya hivyo


Toa maoni yako

Begin typing your search above and press return to search.