KUUNGA KIZAZI
Amesema Mtume Muhammad ﷺ aliyesema [Hatoingia peponi anayewakata jamaa zake].
Na jamaa ya mtu ni mamake, babake, watoto wake na kila ambaye karibu naye kinasaba.
Aya na hadithi zinazozungumzia jambo hili ni nyingi hebu niwatajie baadhi. Mola (Subhaanahu wa Taala) Amesema:
فَهَلْ عَسَيْتُمْ إِن تَوَلَّيْتُمْ أَن تُفْسِدُوا فِي الْأَرْضِ وَتُقَطِّعُوا أَرْحَامَكُمْ} محمد:22
[Basi yanayo tarajiwa kwenu mkitawala ndio mfisidi katika nchi na mwatupe jamaa zenu?] [Muhammad:22]
Mtume ﷺ miongoni mwa mambo aliyoyalingania mwanzo ni kumuabudu Mwenyezi Mungu na kuacha ibada za mababu, kuswali, kutoa sadaka, kujihifadhi na uchafu na kuunga jamaa. Na kuunga jamaa ni kuwafanyia wema na kutowaudhi. Pia ni katika kuwafanyia wema kuwapa nasaha, kuwapa ushauri, kuwapenda na kuwapendelea kheri, kuwafanyia uadilifu, kuwaelekeza, kuwafundisha, kuwapa haki zao za lazima na kuvumilia na kusubiri katika maudhi yao.
FADHLA ZA KUUNGA KIZAZI
Kuunga jamaa kuna fadhila nyingi na katika fadhila hizo ni kuzidishiwa mtu umri wake na vile vile kukunjuliwa mali yake. Amesema Mtume ﷺ :
مَنْ سَرَّهُ أَنْ يُبْسَطَ لَهُ فِي رِزْقِهِ أَوْ يُنْسَأَ لَهُ فِي أَثَرِهِ فَلْيَصِلْ رَحِمَهُ] رواه البخاري ومسلم]
[Anayependa kukunjuliwa riziki yake na kurefushiwa umri wake basi aunge jamaa zake]. [Imepokewa na Bukhari na Muslim]
Na kuunga jamaa kuna daraja kubwa katika Uislamu.
Je tumesimama katika mipaka ya Mwenyezi Mungu? Je tumetekeleza amri zake? Je makemeo yake na makatazo umeyaepuka? Je twawafanyia wema jamaa zetu na tunawatembelea ?
Tunapo taka kheri duniani na kesho akhera tuungeni jamaa zetu na tukaeni nao vizuri.
FAIDA YA KUUNGA KIZAZI
1. Kuunga jamaa ni alama kubwa za ukamilifu wa imani.
2. Kuunga jamaa ni sababu ya kukunjuliwa mtu katika riziki.
3. Kuunga jamaa ni sababu ya kupata radhi za Mwenyezi Mungu.
NASWAHA ZA WATU WEMA JUU YA KUUNGA KIZAZI
Wema waliotangulia wametoa wasia unaoonesha umuhimu wa kuunga jamaa. Amesema ‘Umar ibn Khattwab, Radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake: “Jifundisheni nasaba kisha muwafanyie wema jamaa zenu.” Amesema ‘Atwaa ibn Abi Rabaa: “Kutoa dirham kumpa jamaa yangu inapendeza zaidi kuliko kutoa dirhamu elfu kumpa maskini, mtu akamuuliza: Hata kama jamaa yako ni tajiri? Akasema ‘Atwaa : Ndio, hata kama jamaa yangu ni tajiri”
Vile vile amesema Said ibn Musayyab Mwenyezi Mungu amrehemu hakika aliwacha Dinari kadhaa: “Ewe Mwenyezi Mungu hakika wewe wajua sikuyakusanya mali zangu isipokuwa kwa ajili ya kuhifadhi Dini yangu,. Hana kheri asiyekusanya mali yake kulipa deni lake na kuwafanyia wema jamaa zake”.
Ndugu katika Imani zama tunzao ishi tumeona namna Waislamu namna wanvyo katana na jamaa zao utapata ndugu hawaseshani wala hawajuni, nah ii ni hatari kubwa sana.
Niwajibu wa kila Muislamu kusimama na jukumu hili la kuunga kizazi chake ili awe ni mwenye kutekeleza Mamrisho ya Mwenzi Mungu na Mafundisho ya Bwana Mtume ﷺ na apate radhi za Mwenzi Mungu na fadhla zake.
HASARA YA KUWAFANYIA UBAYA JAMAA ZAKO
1. Kuwakata jamaa ni miongoni mwa sababu za mtu kutoingia peponi. Mtume ﷺ Amesema ya kwamba:
[لا يدخل الجنة قاطع] رواه مسلم
[Hatoingia peponi mtu anayewakata jamaa zake]. [Imepokewa na Muslim]
2. Kupata laana ya Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala) Amesema kwenye Kitabu chake kitukufu:
فَهَلْ عَسَيْتُمْ إِن تَوَلَّيْتُمْ أَن تُفْسِدُوا فِي الْأَرْضِ وَتُقَطِّعُوا أَرْحَامَكُمْ أُولَٰئِكَ الَّذِينَ لَعَنَهُمُ اللَّهُ فَأَصَمَّهُمْ وَأَعْمَىٰ أَبْصَارَهُمْ} محمد:22-23}
[Ndiyo yanayotarajiwa kwenu kuleta uharibifu katika ardhi na kuwakata jamaa zenu wakati mukipata ukubwa. Hao ndio waliolaaniwa na Mwenyezi Mungu Akawatia uziwi masikio yao na akayapofua macho yao.] [Muhammad:22-23]
Na kosa kubwa kabisa ni mtu kuwakata wazazi wake wawili kisha akawakata walio karibu zaidi naye. Mtume ﷺ Amesema:
[ألا أخبركم بأكبر الكبائر قالوا بلى يا رسول الله قال الإشراك بالله وعقوق الوالدين] رواه البخاري
[Je siwajulishi dhambi ambalo ni miongoni mwa madhambi makubwa kabisa? Wakasema maswahaba: Tujulishe ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu. Akasema Mtume ﷺ: [Kumshirikisha Mwenyezi Mungu na kuwakata wazazi wawili]. [Imepokewa na Bukhari]
3. Kufanyiwa haraka mtu kuadhibiwa hapa duniani kabla kuadhibiwa kesho akhera. Amesema Mtume ﷺ:
ما من ذنب أجدر أن يعجل الله لصاحبه العقوبة في الدنيا مع ما يدخره له في الآخرة من البغي وقطيعة الرحم] رواه الترمذي وأبوداود]
[Hakuna kosa ambalo Mwenyezi Mungu analiharakisha zaidi adhabu yake kwa mwenye kulifanya duniani pamoja na kuwekewa adhabu nyingine akhera kuliko kuwakata jamaa na kufanya maasia]. [Imepokewa na Al Tirmidhiy na Abuu Daud]
DARAJA ZA JAMAA YAKO
Hakika jamaa wana daraja tofauti tofauti katika kuishi nao:
Jamaa wenye kushikamana na Dini na jamaa aina hii hufanyiwa wema kwa kule kushikamana kwao na Dini.
Jamaa ambao wazushi ni katika Dini na wenye kufanya maovu. Na hawa wamegawanyika vigawanyo viwili:-
Wanaotangaza bidaa na uzushi wao na maovu yao tena wanalingania kwenye uovu huo. Jamaa hao hupigwa vita kabisa kwa ajili ya kushikamana kwao na uovu. Inafaa kuwaonesha uso wa bashasha, lakini haifai kuwa nyoyo zetu haziko radhi nao moyoni kwa ule uovu wao. Ushahidi wa hilo ni kwamba Mtume ﷺ: [Alimwonesha bashasha ‘Uyaina ibn Hiswhiy aliyekuwa mtu muovu kabisa. Alipokuwa akibisha kwake huku akisema : Ni ndugu muovu katika jamii. Alipoingia Mtume alizungumza naye vizuri akasema: [Hakika tunawaonesha uso wa bashasha watu (waovu) na huku nyoyo zetu zawalaani].
Jamaa wafichao bidaa na vitendo vyao viovu, jamaa aina hii hufanyiwa muamala wa Waislamu wasiojulikana maovu yao.
Jamaa walio makafiri na wanafiki na jamaa aina hii wamegawanyika mara mbili:
Jamaa wanaoupiga vita Uislamu jamaa aina hii hukatwa na hauwaungwi kwa ajili ya kuogopwa shari lao.
Jamaa wasiopiga vita Dini yetu ya uislamu jamaa aina hii hufanyiwa wema kwa njia zifuatazo:
Kuwalingania katika Uislamu kwa njia nzuri.
Kuwaombea dua Mwenyezi Mungu Awaongoze katika Uislamu.
Kuwasaidia wanapokuwa na shida na kuwafanyia wema kuwavutia katika Uislamu.
Mwisho
Tufahamu ya kuwa Jamaa ni msingi wa jamii ya kiislamu, na jamaa ikishikamana, jamii itashikamana. Tukifanya hivyo, tutaweza kujenga umma mmoja wa kiislamu, na kuanzishwa kwa serikali ya kiislamu. Bila ya kujenga msingi wa jamaa moja, hatuwezi kufikia lengo la kurejesha Ukhalifa katika ardhi. Ni jukumu la kila Muislamu kufanya bidii kuunga jamaa yake na kujenga jamii ya kiislamu iliyoshikamana. Tunamuomba Allah atuwezeshe kurejesha umoja wa kiislamu na Atujaalie ni wenye kuwatendea wema jamaa zetu na tufaulu kuipata pepo yake.
Sikiliza Mada hii na Sheikh Uthman Shee (Mungu amrahamu)