0%

https://uongofu.com/wp-content/uploads/2021/06/services-head-1.png

ZAKA NA FAIDA YAKE KATIKA JAMII

ZAKA NA FAIDA YAKE KATIKA JAMII

Je, waijua ibada ya kutoa mali yako wewe Muislamu? Je, wajua kwamba ibada hii ukiifanya Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala) Atakuzidishia baraka katika mali yako hapa duniani na malipo makubwa kesho Akhera? Je, hujui kwamba mali uliyonayo ni mali ya Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala) na Amekupa mtihani katika mali hayo? Je, watarajia kufaulu mtihani huo?.
Mtu akitioa mali yake kwa ajili ya Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala), mali yake huzidi na kupata malipo makubwa kwa Mwenyezi Mungu(Subhaanahu wa Taala) na ni nguzo ya tatu katika Uislamu si nyingine nayo ni zaka. Ni wajibu wa kila Muislamu mwenye mali yaliyofika kiwango kutoa fungu maalum. Mola (Subhaanahu wa Taala) amesema ndani ya Qur’an tukufu:

{وَأَقِيمُوا الصَّلَاةَ وَآتُوا الزَّكَاةَ وَأَطِيعُوا الرَّسُولَ لَعَلَّكُمْ تُرْحَمُونَ}     النور:56

[Na simamisheni Swala na mtoe Zaka na mumtii mtume huenda mukarehemewa]    [Al-Nnuur:56]
Na katika hadithi za Bwana Mtume ﷺ amesema:

بني الإسلام على خمس : شهادة أن لا إله إلا الله ، وأن محمدا رسول الله ، وإقام الصلاة ، وإيتاء الزكاة ، وحج البيت ، وصوم رمضان .    رواه البخاري ومسلم

[Uislamu umejengwa na mambo matano; kupwekeshwa Mwenyezi Mungu, kusimamisha Swala, kutoa Zaka, na kufanya hija na kufunga mwezi wa Ramadhani.]    [Imepokewa na Bukhari na Muslim]

Yamekuja maonyo mbali mbali na tahadhari kwa Muislamu katika suala nzima la kuikwepa Zaka na kufanya ubakhili wa kutekeleza ibada hiyo. Mwenyezi Mungu Mtukufu ameahidi adhabu kali kwa kila ambaye haitekelezi ibada hii tukufu. Amesema Mola Subhaanahu wa Taala:

وَلَا يَحْسَبَنَّ الَّذِينَ يَبْخَلُونَ بِمَا آتَاهُمُ اللَّهُ مِن فَضْلِهِ هُوَ خَيْرًا لَّهُم ۖ بَلْ هُوَ شَرٌّ لَّهُمْ ۖ سَيُطَوَّقُونَ مَا بَخِلُوا بِهِ يَوْمَ الْقِيَامَةِ ۗ وَلِلَّهِ مِيرَاثُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ ۗ وَاللَّهُ بِمَا تَعْمَلُونَ خَبِيرٌ     آل عمران:180

[Na wala wasidhani wale ambao wanafanya ubakhili katika yale aliyowapa Mwenyezi Mungu katika fadhila zake kuwa ni bora kwao. La ni vibaya kwao. Watafungwafungwa kwa yale waliyofanyia ubakhili Siku ya Kiama, na urithi wa mbingu na ardhi ni wa Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu ana khabari za yote mnayoyafanya]      [Al-Imraan:180] .

Vile vile Amesema Mwenyezi Mungu Subhaanahu wa Taala:

وَالَّذِينَ يَكْنِزُونَ الذَّهَبَ وَالْفِضَّةَ وَلَا يُنفِقُونَهَا فِي سَبِيلِ اللَّهِ فَبَشِّرْهُم بِعَذَابٍ أَلِيمٍ يَوْمَ يُحْمَىٰ عَلَيْهَا فِي نَارِ جَهَنَّمَ فَتُكْوَىٰ بِهَا جِبَاهُهُمْ وَجُنُوبُهُمْ وَظُهُورُهُمْ ۖ هَٰذَا مَا كَنَزْتُمْ لِأَنفُسِكُمْ فَذُوقُوا مَا كُنتُمْ تَكْنِزُونَ     التوبة:34-35

[Na wanao kusanya dhahabu na fedha, wala hawazitumii katika Njia ya Mwenyezi Mungu, wabashirie khabari ya adhabu iliyo chungu.Siku zitapo tiwa moto katika Moto wa Jahannamu, na kwazo vikachomwa vipaji vya nyuso zao na mbavu zao na migongo yao, wakaambiwa: Haya ndiyo mlio jilimbikia nafsi zenu, basi onjeni mliyo kuwa mkilimbika]      [Al-Ttawba:34-35]

FAIDA ZA ZAKA KWA UPANDE WA TABIA

Zaka ina faida nyingi sana, nyingine za kidini, za kitabia na pia faida za kijamii.

1. Kwanza Kutoa Zaka ni kusimamisha nguzo, katika nguzo za Uislamu ambayo ni sababu ya utukufu duniani na kesho akhera.
2. Zaka zinamkurubisha mja kwa Mola wake na zinamzidishia mtu imani.
Mtu atoapo zaka hupata ujira na malipo makubwa mbele ya Mwenyezi Mungu. Asema Mola Subhaanahu wa Taala:

{يَمْحَقُ اللَّهُ الرِّبَا وَيُرْبِي الصَّدَقَاتِ ۗ وَاللَّهُ لَا يُحِبُّ كُلَّ كَفَّارٍ أَثِيمٍ}   البقرة:276

[Mwenyezi Mungu huiondolea baraka riba, na huzibariki sadaka. Na Mwenyezi Mungu hampendi kila mwenye kukanya na afanyae dhambi.]      [Al-Baqara:276]
3. Mwenyezi Mungu Subhaanahu wa Taala humfutia madhambi Muislamu atoapo zaka. Mtume ﷺ Amesema:

[والصدقة تطفئ الخطيئة كما يطفئ الماء النار]    رواه الترمذي

[Na sadaka(zaka)inaondosha maovu kama maji yanavyozima moto]    [Imepokewa na Tirmidhiy]

FAIDA ZA ZAKA KWA UPANDE WA TABIA

Na miongoni mwa faida za kitabia:
1. Kutoa zaka inamuweka mtu katika kundi la watu wakarimu na wenye kujali maslahi ya watu,
2. Kutoa zaka kunamfanya mtu kusifika na sifa ya huruma na upole kwa ndugu zake.Kwani Waislamu wenye huruma Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala) pia huwahurumia.
3. Kutoa zaka kunasafisha vifua vya watu wenye kupewa mali ile na watampenda mtoaji kwa kule kuwajali ndugu zake na kuwasaidia.
4. Kutoa zaka kunamsafisha mtoaji na sifa ya ubakhili na uchoyo. Na tabia mbaya hii ya ubakhili ni miongoni mwa tabia mbaya ambazo haitakiwi Muislamu kujipamba nayo. Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala) Amesema katika kitabu chake kitukufu:

{خُذْ مِنْ أَمْوَالِهِمْ صَدَقَةً تُطَهِّرُهُمْ وَتُزَكِّيهِم بِهَا وَصَلِّ عَلَيْهِمْ ۖ إِنَّ صَلَاتَكَ سَكَنٌ لَّهُمْ ۗ وَاللَّهُ سَمِيعٌ عَلِيمٌ}   التوبة:103

[Chukua sadaka katika mali zao, uwasafishe na uwatakase kwazo, na uwaombee rehema. Hakika maombi yako ni utulivu kwao. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia Mwenye kujua.]    [Al-Ttwaba:103]

FAIDA ZA ZAKA KWA UPANDE WA JAMII

Na miongoni mwa faida za kijamii katika kutoa zaka:
Kutoa zaka huwaondolea watu matatizo ya kiuchumi waliyonayo na kama illvyo ni kwamba wanaohitajia ni wengi.
Kutoa zaka hutilia nguvu mambo ya Waislamu wanayotaka kuyafanya kwa mfano kupigana kwa ajili ya Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala).
1. Zaka huondoa chuki baina ya maskini na matajiri na kuleta mapenzi baina yao.
2. Zaka hukuza mali na kuyazidisha na kuwa na baraka. Amesema Mtume ﷺ: [Haipungui mali inayotolewa zaka].
3. Kutoa zaka hueneza mali baina ya watu na haibaki kwa matajiri bali huzunguka kati yao.
Na hizi faida tulizozitajaza ziwe ni za kijamii au za kidini au za kitabia zinaonesha kwamba kutoa zaka ni jambo muhimu sana na dharura Ili kutengeneza nafsi ya mtu na jamii kwa ujumla.
Kutoa zaka kuna athari katika nafsi ya mtu na jamii kwa ujumla. Kwani kutoa zaka ndio nidhamu ya kwanza waliyoijua watu katika kuwasaidia wanaohitaji na uadilifu katika jamii nzima ya kiislamu. Kwani mali inatoka katika tabaka ya matajiri na kwenda katika tabaka ya maskini na wanaohitajia. Ukweli ni kwamba zaka inasafisha mali ya mtoaji na kuikuza kama ambavyo inamtakasa moyo wa mtoaji zaka kutokana na tabia ya ubakhili, tamaa na kutojali wanaohitajia. Vilevile inasafisha moyo wa anayepewa zaka kutokana na tabia mbovu ya uhasidi na chuki kwa mwenye mali.
Tukiangalia vyema pia kutoa zaka kunazidisha mshikamano kati ya jamii inayoishi pamoja na kuondoa umaskini na pia kuangamiza matatizo ya kijamii, kiuchumi na ya kitabia endapo itatolewa na kupewa wanaostahili.

MALI YANAYOTOLEWA ZAKA

Miongoni mwa mali ambayo hutolewa zaka ni dhahabu, fedha kwa sharti ifike kiwango na wajibu ni robo ya kumi ya dhahabu au fedha.Na katika mali ambayo ni lazima kutolewa zaka ni bidhaa za biashara nazo ni kila kilichofanyiwa biashara kwa mfano:majumba, magari, nafaka, mifugo, vitambaa na vyingenevyo. Na ni wajibu kutoa katika mali tuliyo yataja robo ya kumi.

Ama vitu vilivyoandaliwa kwa matumizi ya kawaida kama Magari ya matumizi, Majumba ya kuishi na vitu mfano wa vitu hivi havitolewi Zaka. Kwa neno la Mtume ﷺ:

[ليس على المسلم في عبده ولا فرسه صدقة]    رواه البخاري

[Halazimiki Muislamu kwa mtumwa wake wala farasi wake zaka].  [Imepokewa na Bukhari]

WANAOSTAHIKI KUPEWA ZAKA

Miongoni mwa watu wanaostahiki Kupewa zaka Mwenyezi Mungu aliyetukuka amewataja watu sampuli nane ndani ya Qur’an Tukufu Aliposema:

{إِنَّمَا الصَّدَقَاتُ لِلْفُقَرَاءِ وَالْمَسَاكِينِ وَالْعَامِلِينَ عَلَيْهَا وَالْمُؤَلَّفَةِ قُلُوبُهُمْ وَفِي الرِّقَابِ وَالْغَارِمِينَ وَفِي سَبِيلِ اللَّهِ وَابْنِ السَّبِيلِ ۖ فَرِيضَةً مِّنَ اللَّهِ ۗ وَاللَّهُ عَلِيمٌ حَكِيمٌ}

[Hakika zaka hupewa mafukara na maskini na wanazikusanya na waliosilimu karibu na watumwa na wenye madeni na katika jihadi na kupewa msafiri zaka hii ni faradhi kutoka kwa Mwenyezi Mungu na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi na Mwenye hikma.]    [Al-Ttwawba:60]

Nachukue tena nafasi hii kuwafafanulia aliyowataja Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala) katika wanaostahiki kupewa zaka.

WANAOSTAHIKI KUPEWA ZAKA

1. Fukara: ni mtu ambaye hapati cha kumtosha isipokuwa kidogo chini ya nusu.Kwa hivyo ikiwa mtu hapati cha kujisimamia yeye na familia yake nusu mwaka basi huyo ni fukara. Kwa hiyo atapewa cha kumtosha yeye na familia yake mwaka mzima.

2. Maskini: ni mtu ambaye anapata cha kumtosha nusu na zaidi lakini hapati cha mwaka mzima kwa hiyo hupewa zaka ili kumkamilishia mahitaji.

3. Wenye kukusanya zaka: ni wale ambao wanamuwakilisha kiongozi kwa kukusanya mali ya zaka kutoka kwa wenye mali na kuwapelekea wanaostahiki na kuyahifadhi.

4. Waliosilimu karibu: hawa hupewa ili kuzitia nguvu imani zao hatimaye wawe walinganizi wa dini ya kiislamu na kuwa mfano mzuri.

5. Mtumwa: anaingia katika tamko hili ni mtumwa ambaye husaidiwa kujikomboa kwa mali ya zaka.

6. Wenye madeni: endapo hawana cha kulipa madeni yao na wenye madeni watapewa kile cha kulipa madeni yawe madeni yao ni mengi au machache.

Hata kama wanao uwezo wa kujitafutia chakula lakini hawezi kulipa.

7. Kutoa zaka katika jihadi: hutolewa katika jihadi kinachowatosha wapiganaji katika vita kununulia silaha na matumizi mengine ya kivita.

8. Msafiri: ni msafiri aliyekatikiwa na safari. Msafiri hupewa mali ya zaka ili ziweze kumfikisha mjini kwake anakokwenda.

Na hawa ndio ambao Mwenyezi Mungu Mtukufu Amewataja kwenye Kitabu Chake, na Akaelezea kwamba ni lazima kutekelezwa ibada hii kwa ajili yake. Wala haifai kutolewa zaka katika sehemu nyingine kwa mfano; kujenga Misikiti, kutengeneza njia, kuchimba visima na mengineyo. Kwa sababu Mwenyezi Mungu Amewataja Mwenyewe wanaostahiki na wasiokuwa wao haifai kabisa kupewa zaka.

Mwisho

Kuitekeleza nguzo hii ni kumsafisha mtoaji kutokana na sifa ya ubakhili na madhambi. Pia ni kutakasa mali yake na kuzidisha baraka kwa kutoa zaka, kuondoa chuki na uhasidi katika nafsi za wenye kupokea zaka, bali kuleta mapenzi kati ya tajiri na maskini.

Mwisho kabisa tunamuomba Mwenyezi Mungu Mtukufu Atujaalie tuwe miongoni mwa wanaotekeleza ibada ya zaka, pia tunamuomba Ayabariki mali zetu, Atupe ujira mkubwa kwa tunachokitoa kesho akhera.

KWA FAIDA ZAIDI SIKILA MADA HII NA DR.MAJID HOBENI

Toa maoni yako

Begin typing your search above and press return to search.