0%

https://uongofu.com/wp-content/uploads/2021/06/services-head-1.png

KUTAHADHARI NA UCHAWI NA UGANGA

KUTAHADHARI NA UCHAWI NA UGANGA

Ndugu Muislamu katika Makala haya tutaelezea hukumu ya uchawi na uganga katika uislamu pia tutatoa tahadhari kwa watu kwenda kwa waganga na wapiga ramli na pia tuwabainishie hatari za waganga katika umma tutahimiza kuchukua sababu za kisheria.
Ni kweli usiofichika ya kwamba watu wanapitia mitihani mbali mbali, kwa mfano mitihani ya kiuchumi, ya kiafya na pia ya kijamii na mitihani mingineo. Kwa hivyo kukabiliana na mitihani hii ni lazima sheria ichungwe na sababu za kisheria zifuatwe katika kutatua matatizo yoyote yanayomkabili Muislamu popote alipo hafai kwenda kinyume na sheria.
Ndugu Muislamu hakika katika mitihani waliopewa watu leo, waume kwa wake, wakubwa kwa wadogo, isipokuwa walio rehemewa na Mwenyezi Mungu ni kwenda kwa waganga na watu wa ramli wanaokula mali ya watu kwa batili.
Unaweza kumuona kiongozi amefungamanishwa na mganga hafanyi jambo lolote isipokuwa kwa ushauri wake hata kama ushauri huo utaenda kinyume na dini ya kiislamu, na anahisi ndani ya moyo wake ya kwamba huyo mganga ndiye anayempa uongozi na anaweza kuuchukua uongozi huo.na Kusahau kabisa kuwa Mwenyezi Mungu (Subhanahu wa Ta’aala) Ndie mmiliki wa kila kitu,Mwenyezi Mungu Anasema:

قُلِ اللَّهُمَّ مَالِكَ الْمُلْكِ تُؤْتِي الْمُلْكَ مَن تَشَاءُ وَتَنزِعُ الْمُلْكَ مِمَّن تَشَاءُ وَتُعِزُّ مَن تَشَاءُ وَتُذِلُّ مَن تَشَاءُ ۖ بِيَدِكَ الْخَيْرُ ۖ إِنَّكَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ      آل عمران:26

[Sema ewe Mwenyezi Mungu Mfalme wa wafalme Unampa ufalme unaye mtaka na unampokonya ufalme unayemtaka na unamtukuza unayemtaka na Unamdhalilisha unayemtaka katika mkono wako kuna kheri. Hakika yako wewe juu ya kila kitu ni muweza]    [Al-Imraan: 26]

Utaona mfanyabiashara hanunui wala hauzi isipokuwa kwa ushauri wa mganga ambaye amefungamanisha moyo wake na mganga huyo na hufanya lolote atakaloambiwa na mganga namna litakavyokuwa jambo lile.
Utapata mke anaetaka kumtawala mumewe kwa kiasi ambacho mume yule hatatamani mke mwengine isipokuwa yeye ataenda mke yule kwa mganga mchafu na atataka usaidizi, akisahau kuwa Mwenyezi Mungu ndie ambaye amejaalia mapenzi ya dhati baina ya mume na mke hii ndio hali yetu waja wa Mwenyezi Mungu isipokuwa aliyerehemewa na Mwenyezi Mungu.
Ndugu katika imani ni vyema kila Muislamu kujuwa Hukmu ya kufanya hivyo,na kwamba Mwenyezi Mungu Amebainisha wazi katika Qur’an tukufu kwamba kujifundisha uchawi ni ukafiri.
Mwenyezi Mungu (Subhanahu wa Ta’aala)

{وَمَا يُعَلِّمَانِ مِنْ أَحَدٍ حَتَّىٰ يَقُولَا إِنَّمَا نَحْنُ فِتْنَةٌ فَلَا تَكْفُرْ} البقرة:102

[Na hawamfundishi yoyote mpaka waseme hakika yetu sisi ni fitna usikufuru ]  [Al-Baqara: 102]
Na vile vile Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala) Amesema:

{وَلَا يُفْلِحُ السَّاحِرُ حَيْثُ أَتَىٰ}     طه:69

[Na mchawi hafanikiwi popote afikapo.]    [Twaha: 69].

Na amesema Mtume ﷺ:

اجتنبوا السبع الموبقات))، قالوا: يا رسول الله، وما هن؟ قال: ((الشرك بالله، والسحر، وقتل النفس التي حرم الله إلا بالحق، وأكل الربا، وأكل مال اليتيم، والتولي يوم الزحف، وقذف المحصنات المؤمنات الغافلات        متفق عليه

[Jiupusheni na mambo saba yanayoangamiza, wakasema maswahaba: Ni yapi, ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu? Akasema Mtume ﷺ: Kumshirikisha Mwenyezi Mungu, na uchawi, na kuuwa nafsi aliyoharamishwa na Mwenyezi Mungu ila kwa haki, na kula Ribaa, na kula mali ya yatima, na kukimbia vitani,(katika jihadi) na kuwasingizia kuwa wamezini wanawake waliojihifadhi walioghafilika tena waumini].  [Imepokewa na Bukhari na Muslim]
Asema Aisha:Watu walimuuliza Mtume ﷺ kuhusu uganga akasema: [Hao si chochote. Wakasema: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu hakika hao wanazungumzia mambo mara nyingine kisha yanatokea kweli. Akasema Mtume ﷺ:

[تِلْكَ الْكَلِمَةُ الْحَقُّ يَخْطَفُهَا الْجِنِّيُّ ، فَيَقْذِفُهَا فِي أُذُنِ وَلِيِّهِ ، وَيَزِيدُ فِيهَا مِائَةَ كَذْبَةٍ]     رواه مسلم

[Hilo ni neno la haki analolichukua jinni kisha akalitia katika sikio la rafiki yake naye kwa upande wake akachanganya neno hilo na maneno mia ya uongo].      [Imepokewa na Muslim]
Na katika hadithi nyingine za kukataza uchawi na uganga. Mtume
ﷺ: amesema:

[مَنْ أَتَى كَاهِنًا، أَوْ عَرَّافًا، فَصَدَّقَهُ بِمَا يَقُولُ، فَقَدْ كَفَرَ بِمَا أُنْزِلَ عَلَى مُحَمَّدٍ صلى الله عليه وسلم]   رواه أحمد

[Atakayeenda kwa mganga au mchawi akamuuliza na akamuamini kwa atakayosema basi amekufuru aliyoteremshiwa Mtume Muhammad rehma na amani zimfikie].      [Imepokewa na Ahmad]
Hadithi hii tukufu inatufundisha kwamba mtu yoyote atakaye kwenda kwa mganga kumuuliza kitu na akamuamini kwa atakayomwambia basi ametoka kabisa katika dini ya Uislamu. Ama hukumu ambayo inatakiwa aichukue kiongozi kwa atakayepatikana anafanya uchawi ni kukatwa shingo yake na kuuwawa kama ilivyothibiti katika maneno ya Maswahaba Mwenyezi Mungu awawie radhi; Tahadhari tunayoitoa ni kwamba haifai kwa Muislamu kuchukua hatua mikononi mwake isije ikaleta balaa na fujo miongoni mwa watu.

MADHARA YA WACHAWI NA WAGANGA KATIKA UMMA

Baadhi ya madhara ya waganga na wachawi katika umma. Madhara hayo ni kama yafuatayo;
1. Kufutika imani za wanaokwenda kwa waganga na kuwaamini kwa watakayo ambiwa kama ilivyo katika hadithi ya Mtume ﷺ tuliyoitaja.
2. Kukithiri vifo na au kuona makaburi yanafukuliwa au kuona baadhi ya viungo vya wanadamu kwa hawa waganga baada ya kuwaamrisha wafuasi wao wawaletee.
3. Kuenea zina na machafu baina ya watu kwani ni wangapi katika waganga hufanya zina na wake za watu na wakaharibu ndoa za watu na wakafungua milango mikubwa ya shari.
4. Kula mali za watu kwa njia ya batili kinyume na haki, kwani kila anachochukua mganga ni kwa kazi yake mbovu na anakula uchafu. Mtume ﷺ amekataza kula thamani ya mbwa na mahari ya mzinifu na chumo la mganga.
5. Kuwapoteza watu na kuwafanya watu kuwa na tabia mbaya na kuwazuia wao kutekeleza maamrisho ya Dini, kwani kuna wengine huacha swala zote au baadhi yake na wengine huzuiliwa kuoga janaba na wengine huzuiliwa kufanya mema bali huamrishwa kufanya mabaya.
6. Kumkasirisha Mwenyezi Mungu na kusababisha adhabu yake. Alisema Zainab binti Jahshi kumwambia Mtume ﷺ:

[أَنَهْلِكُ وَفِينَا الصَّالِحُونَ قَالَ « نَعَمْ إِذَا كَثُرَ الْخَبَثُ]      رواه مسلم

[Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu. Je tunaweza kuangamizwa na kati yetu kuna watu wema? Akasema Mtume ﷺ: Ndio, ukikithiri uchafu].    [Imepokewa na Muslim]

Na je kuna wachafu zaidi kuliko waganga waovu?.
7. Kupata hasara duniani na kesho akhera.Amesema Mwenyezi Mungu (Subhanahu wa Ta’aala)

{وَلَا يُفْلِحُ السَّاحِرُ حَيْثُ أَتَىٰ} طه:69

[Na mchawi hafanikiwi popote afikapo.]   [Twaha: 69].

Asema Sheikhul Islaam Ibn Taimia Mwenyezi Mungu Amrehemu «Hivi ndivyo ilivyo. Hakika ufuatiliaji unaonesha kwamba watu wakitegemea nyota hawafaulu. Si duniani bali vile vile kesho akhera.”
Hayo ndiyo baadhi ya madhara yanayopatikana kutoka kwa waganga waovu.
Kwa hivyo, ni lazima ewe Muislamu kuelekea kwa Mwenyezi Mungu na watu wakumbushane kwamba jambo la kwenda kwa waganga na kuangaliliwa ni jambo baya na halifai. Jueni ya kwamba Mwenyezi Mungu ni Mfalme na Mwenye kumiliki kila kitu, hana wa kumzuwia anapo toa. Ametuamrisha Mola Wetu tutakapo kuwa na tatizo lolote tumuombe Yeye na tumtake Yeye msaada, na yafaa tumtegemee yeye katika kila kitu na tuchukue sababu za kisheria katika kufikia tunayoyakusudia na miongoni mwa sababu hizo ni kumuomba Mwenyezi Mungu dua. Kwa hivyo, atakaemuomba kwa nia njema hakika Mwenyezi Mungu hapotezi ujira wa amali ya anayeomba. Mwenyezi Mungu yuko karibu na hujibu maombi na yeye ndiye anayeruzuku ndege porini na samaki baharini.Amesema Mwenyezi Mungu (Subhanau wa Ta’aala)

اللَّهُ الَّذِي خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ وَأَنزَلَ مِنَ السَّمَاءِ مَاءً فَأَخْرَجَ بِهِ مِنَ الثَّمَرَاتِ رِزْقًا لَّكُمْ ۖ وَسَخَّرَ لَكُمُ الْفُلْكَ لِتَجْرِيَ فِي الْبَحْرِ بِأَمْرِهِ ۖ وَسَخَّرَ لَكُمُ الْأَنْهَارَ وَسَخَّرَ لَكُمُ الشَّمْسَ وَالْقَمَرَ دَائِبَيْنِ ۖ وَسَخَّرَ لَكُمُ اللَّيْلَ وَالنَّهَارَ      إبراهيم:32-34

[Mwenyezi Mungu ambaye ameumba mbingu na ardhi na ameteremsha maji kutoka mbinguni akatoa kutokana na maji hayo matunda hali ya kuwa ni riziki kwenu na Amewadhalilishia meli ili itembee baharini kwa amri Yake na Akawadhalilishia mito na akawadhalilishia jua na mwezi zinazotembea na akawadhalilishia usiku na mchana na akawapa kila mnachoomba na endapo mutazihesabu neema za Mwenyezi Mungu hamuwezi kuzidhibiti hakika mwanadamu ni dhalimu aliye mkufuru Mwenyezi Mungu. ] [Ibrahiim:32-34]

 SIKILIZA MADA HII NA SHEIKH SHADDADI ALI 

Toa maoni yako

Begin typing your search above and press return to search.