SOMO LA FIQHI
Aliye kwenye ihramu akisumukwa na Nywele tatu anapopangusa kichwa katika kutawadha au kuoga, hilo halimdhuru. Pia lau baadhi ya nywele za masharubu au ndevu zilisumuka au ukucha wake ukakatika, hilo halitamdhuru, isipokuwa akizisumua kwa kusudi. Na mwanamke analingana na mwanamume katika hilo la kutodhurika na kusumukwa na nywele au kucha.
Inafaa kwa aliye kwenye ihramu kufunga uzi mguuni mwake akihitajia hilo au kukiwa na maslahi ya kufanya hivyo.
UWEKAJI MASHARTI KATIKA NIA
Ambaye ni mgonjwa, au anaogopea kutokewa na jambo lenye kumzuia kukamilisha ibada yake ya Hijja, ni sunna kwake aweke sharti wakati wa kuhirimia na aseme:
[لبيك عمرة، أو لبيك حجاً، “فإن حبسني حابس فمحلي حيث حبستني]
«Tunaitikia mwito wako wa Umra (au Hija) iwapo kutatokea kitu chochote chenye kunifunga mimi (nisimalize ibada yangu,) basi mahali pangu pa kutahalali ni pale uliponifunga».
Bibi Aishah radhi za Allah ziwe juu yake amepokewa akisema kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu ﷺ aliingia kwa Dhuba’ah binti Zubair akamwambia: (Huenda ulitaka kuhiji) Aksema: “Najikuta naumwa. Akamwambia:
[حجي واشترطي وقولي : اللهم محلي حيث حبستني]
[Hiji na ujiwekee sharti na useme ‘ Ewe Mola! Mahali pangu pa kujifungua na ihramu ni pale uliponifunga] [Imepokewa na Bukhari na Muslim.].
Akisema hivyo, kisha akapatikana na jambo la kumzuia, basi itafaa atahalali (ajifungue na ihramu) bila kulazimiwa na kitu.