MNASABA WA MWAKA MPYA
Shukrani zote ni za Mwenyezi Mungu, Swala na salamu zimfikie Mtume wetu Muhammad ﷺ. Inapaswa kwa kila mwanadamu kujiuliza maswala haya:
Nimekuja kutoka wapi ?
Naenda wapi ?
Ulimwengu huu ulioko pembezoni mwangu umekuja kutoka wapi ?
Kwa ajili gani nimeumbwa ?
Matamanio ni sababu ya mtu kujisahau, na kumalizika mwaka kwa haraka, amesema Hassan Basri: Tahadharini na matamanio, kwani hapati mtu na tamanio kheri ya duniani na kesho akhera. Mafhumu Neno lake Mwenyezi Mungu Subhaanahu wa Taala:
{أَوَلَا يَرَوْنَ أَنَّهُمْ يُفْتَنُونَ فِي كُلِّ عَامٍ مَّرَّةً أَوْ مَرَّتَيْنِ ثُمَّ لَا يَتُوبُونَ وَلَا هُمْ يَذَّكَّرُونَ} التوبة:126
[Je! Hawaoni ya kwamba wanatiwa mtihanini kila mwaka mara moja au mara mbili? Kisha hawatubu, wala hawakumbuki.] [Al-Twaba:126]
Amesema Mujaahid Mungu Amrahamu: wataonjwa kwa ukame na njaa. Amesema Qatada: wataonjwa kwa kupigana vita mara moja na mara mbili. Amesema Mujaahid: wataonjwa kwa ukame na shida. Amesema ‘Atwiyyah: Wataonjwa kwa maradhi na maumivu.
Maswali muhimu yanapaswa kwa mwanadamu kujibu. Maswali hayo baada ya kumalizika kwa mwaka. Kila mwanadamu anapaswa kujiuliza maswali haya:
Swala ngapi hukuswali ?
Umepuuza jumaa ngapi ?
Saumu ngapi hukufunga ?
Mali ngapi hukuyatolea zaka ?
Hija ngapi zimekupita?
Umefanyia uvivu wema ngapi ?
Uovu kiasi gani uliounyamazia?
Mambo mangapi ya haramu umeyaangalia?
Maneno mangapi machafu umeyazungumza?
Mara ngapi umewaudhi wazazi wako wawili na wala hukuwaridhisha?
Umewavisha madhaifu wangapi?
Wangapi umewadhulumu?
Umuhimu wa Wakati
Amesema Mwenyezi Mungu(Subhaanahu wa Taala):
{يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اتَّقُوا اللَّهَ وَلْتَنظُرْ نَفْسٌ مَّا قَدَّمَتْ لِغَدٍ ۖ وَاتَّقُوا اللَّهَ ۚ إِنَّ اللَّهَ خَبِيرٌ بِمَا تَعْمَلُونَ } الحشر:18
[Enyi mlio amini! Mcheni Mwenyezi Mungu, na kila nafsi iangalie inayo yatanguliza kwa ajili ya Kesho. Na mcheni Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu anazo khabari ya mnayo yatenda.] [Al-Hashr:18]
Amesema tena Mwenyezi Mungu Subhaanahu wa Taala:
{يَوْمَ تَجِدُ كُلُّ نَفْسٍ مَّا عَمِلَتْ مِنْ خَيْرٍ مُّحْضَرًا وَمَا عَمِلَتْ مِن سُوءٍ تَوَدُّ لَوْ أَنَّ بَيْنَهَا وَبَيْنَهُ أَمَدًا بَعِيدًا ۗ وَيُحَذِّرُكُمُ اللَّهُ نَفْسَهُ ۗ وَاللَّهُ رَءُوفٌ بِالْعِبَادِ} آل عمران:30
[Siku ambayo kila nafsi itakuta mema iliyo yafanya yamehudhurishwa, na pia ubaya ilio ufanya. Itapenda nafsi lau kungekuwako masafa marefu baina ya ubaya huo na yeye.] [Al-Imraan:30]
Amesema ‘Umar Ibn Khatwab (Radhi za Allah ziwe juu yake) “Hesabuni nafsi zenu kabla hazijahisabiwa na pimeni nafsi zenu kabla hazijapimwa, kwani itakuwa ni wepesi kwenu nyinyi siku ya Qiyama ikiwa mtahesabu nafsi zenu.”
Ndugu Muislamu, Je tumejiandaa kiasi gani kwenda kujibu maswali mbele ya Allah siku ya kiama?. Kila moja ajiulize suala hilo na aandae jibu la ukweli kabisa. Kwasababu kuokoka mwanadamu siku hiyo, ni kujibu swali atakalo ulizwa na Allah siku ya hesabu.
Mfano Mzuri wa Kuhesabu Nafsi
Abubakar (Radhi za Allah ziwe juu yake ) alikuwa akiuzuia ulimi wake ukitoka nje, na akisema: kiungo hiki kimeniingiza katika maangamivu.
Amesema Ghunaym: Mungu Amrehemu “tulikuwa tukijipatia mawaidha kwa mambo mane:
Fanya amali njema katika ujana wako kabla utu uzima
Unapokuwa na wakati kabla kuwa na shughuli
Unapokuwa na afya kbala kuwa mgonjwa
Unapokuwa hai kabla hujafa.
TANABAHISHO
Hatukuwekewa na sheria kusherehekea Mwaka mpya wa Hijria Unapo ingia kama vile wanavyo fanya wasio kuwa waislamu kusherehekea mwaka mpya wa miladia unapo ingia,na vile vile ni haramu kwa Muislamu kushiriki kwa Mnasaba huo kwa sababu ni sherehe zinzao ambatana na Ibada za wasio kuwa Waislamu na tumeharamishwa kuwaiga wasio kuwa waislamu
Sikiliza Mada hii na Sheikh Muhammad Rajab