SOMO LA FIQHI
Wajibu za Hijja
1. Kuhirimia kwenye sehemu zilizowekwa kuhirimia:
kwa neno lake ﷺ baada ya kuzitaja sehemu za kuhirimia:
[هُنَّ لَهُنَّ، وَلِمَنْ أَتَى عَلَيْهِنَّ مِنْ غَيْرِهِنَّ مِمَّنْ أَرَادَ الْحَجَّ وَالْعُمْرَةَ] رواه البخاري
[Hizo ni za watu wa sehemu hizo na wale wanaokuja hapo kati ya watu wa sehemu nyingine miongoni mwa wale wanataka kuhiji au kufanya Umrah] [Imepokewa na Bukhari].
2. Kusimama Arafa mpaka jua kuzama kwa aliyesimama mchana:
Kwa kuwa Mtume ﷺ alisimama mpaka jua likazama.
3. Kulala hapo Muzdalifa:
kwa sababu Mtume ﷺ alilala hapo na akasema:
[لِتَأْخُذْ أُمَّتِي نُسُكَهَا، فَإِنِّي لَا أَدْرِي لَعَلِّي لَا أَلْقَاهُمْ بَعْدَ عَامِي هَذَا] رواه ابن ماجه
[Umma wangu wachukue ibada yao ya Hija kutoka kwangu, kwani mimi sijui pengine huenda nisikutane nao baada ya mwaka wangu huu] [Imepokewa na Ibnu Maja.]
Na kwamba yeye ﷺ aliwaruhusu Waislamu madhaifu baada ya nusu ya usiku. Hilo linaonyesha kwamba kulala hapo Muzdalifa ni lazima. Na Mwenyezi Mungu Ameamrisha atajwe katika Mash’ar al-Haraam.
4. Kulala Mina masiku ya siku za Tashriiq:
kwa ilivyothubutu kwamba Mtume ﷺ aliwaruhusu wachungaji kulala kando ya Mina [Imepokewa na Abu Yalaa katika Musnad yake.].
Hii inaonyesha kwamba asili ni kuwa kulala Mina ni wajibu.
5. Kuvirushia viguzo vijiwe,
kwa kauli Yake Aliyetukuka:
{ وَٱذۡكُرُواْ ٱللَّهَ فِيٓ أَيَّامٖ مَّعۡدُودَٰتٖۚ } البقرة: 203
[Na mtajeni Mwenyezi Mungu katika siku zinazohesabika] [2: 203].
Na siku zinazohesabika: ni siku za ashriiq.
Na kurusha vijiwe ni miongoni mwa kumtaja Mwenyezi Mungu, kwa neno la Mtume (saw):
[إِنَّمَا جُعِلَ الطَّوَافُ بِالْبَيْتِ وَبَيْنَ الصَّفَا والْمَرْوَةِ وَرَمْيُ الْجِمَارِ لِإِقَامَةِ ذِكْرِ اللهِ] رواه أبو داود
[Hakika kutufu Alkaba, kusai baina ya Swafaa na Marwah na kuvirushia viguzo vijiwe ni miongoni mwa kusimamisha utajo wa Mwenyezi Mungu] [Imepokewa na Abu Daud.].
6. Kunyoa au kupunguza,
kwa neno la Mwenyezi Mungu Aliyetukuka:
{لَتَدۡخُلُنَّ ٱلۡمَسۡجِدَ ٱلۡحَرَامَ إِن شَآءَ ٱللَّهُ ءَامِنِينَ مُحَلِّقِينَ رُءُوسَكُمۡ وَمُقَصِّرِينَ} الفتح: 27
[Mtaingia Msikiti wa Haram mkiwa kwenye amani, Mwenyezi Mungu Atakapo, hali ya kunyoa vichwa vyenu na kupunguza] [48: 27].
7. Kutufu twawafu ya kuaga:
kwa haditi iliyothubutu kutoka kwa Ibnu ‘Abbas Radhi za Allah zimfikie yeye kuwa alisema:
[أُمِرَ النَّاسُ أَنْ يَكُونَ آخِرُ عَهْدِهِمْ بالبيت، إِلَّا أَنَّهُ خُفِّفَ عَنِ الْحَائِضِ] رواه مسلم
[Wameamrishwa watu kuwe kule kutufu twawafu ya kuaga iwe shughuli yao ya mwisho kwenye Alkaba, isipokuwa mwenye hedhi alirahisishiwa] [Imepokewa na Muslim].
Tanbihi
Wajibu wa Hajji
Mwenye kuacha wajibu itamlazimu kuchinja mnyama ili kuunga upungufu huu.