VYOMBO VYA HABARI NA ATHARI YAKE
Shukrani zote ni za Mwenyezi Mungu, Mola wa viumbe vyote na rehma na amani zmfikie Mtume Muhammad. Napenda kuitanguliza mada hii ya vyombo vya utangazaji, kuwatajia umuhimu wake. Na pia nitawabainishia vipi vyombo vya utangazaji vinaweza kuitumikia Dini na matatizo yanayo vikabili vyombo hivyo.
Mwenyezi Mungu Subhaanahu wa Taala Ametupa neema ya ulimi ili tumshukuru kwa neema hiyo kwa kuitumia vilivyo kwa mujibu wa mafunzo mema ya kiislamu. Ametuamrisha Mwenyezi Mungu Subhaanahu wa Taala kuutumia ulimi vizuri tunapozungumza.
Amesema Mwenyezi Mungu Subhaanahu wa Taala:
{يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اتَّقُوا اللَّهَ وَقُولُوا قَوْلًا سَدِيدًا}
[Enyi mlio amini! Mcheni Mwenyezi Mungu na semeni maneno ya sawasawa.] [Al-Ahzaab:70]
Na Mtume ﷺ asema:
[من كان يؤمن بالله واليوم الآخر، فليقل خيرًا أو ليصمت] رواه البخاري ومسلم
[Aliyemuamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho, basi aseme maneno mazuri au anyamaze]. [Imepokewa na Bukahri na Muslim]
Na Ametilia nguvu mshairi akisema: ‘Zungumza vizuri uwezavyo kwani maneno yako ni yako na kunyamaza ni vizuri na ikiwa hutapata maneno mazuri ya kuzungumza basi kunyamaza bila ya kufanya vizuri ni vizuri’. Asema mshairi mwengine: ‘Kuzungumza ni vizuri na kunyamaza ni usalama basi unapozungumza usiwe na maneno mengi kwani sijajuta kwa kunyamaza hata mara moja lakini nimejuta juu ya maneno yangu mara nyingi’.
Kwa mujibu wa Aya na hadithi na mashairi tuliyoyataja inaonesha wazi kuwa Muislamu hafai kabisa kuutumia ulimi wake kinyume na maagizo ya Allah (Subhaanahu wa Taala), huku tukijua ya kwamba kila siku watu wanawasilina kupitia njia tofauti tofauti kama kutumia simu, barua, na vyombo vingine vya mawasiliano, bali wengine kupitia vyombo vya utangazaji. Na kwa kweli watu wamevielekea mno vyombo hivyo ili kupata habari mbali mbali.
Kwa kweli vyombo vya utangazaji vina faida zake na hasara zake. Kwa hivyo hatusemi kwamba haifai kutumia vyombo hivyo, lakini isiyofaa ni kuvitumia katika njia mbaya isiyokubalika kiislamu. Kwani makafiri wakiwemo Waamerika na Wamagharibi wame vitumia vyombo hivi katika kuwapotosha wanaadamu na njia ya sawa, vikiwemo vyombo vya kusikiliza kama redio na vyombo vya kuonesha kama runinga na vya kusoma kama magazeti, majarida na vyenginevvyo.
Kwa kweli vyombo vya utangazaji vimechukua nafasi kubwa kabisa katika kuwaathiri na kuwapotosha watu kimaadili. Sasa wajibu wetu ni mambo gani ya upotofu yanayoenezwa na makafiri katika vyombo vya utangazaji?. Bila shaka wajibu wetu ni kuwatahadharisha watu na uovu unaoenezwa na vyombo hivyo, kwa kuwalingania katika Uislamu na kuacha upotofu. Napenda kuchukua fursa hii kukuliza maswali yafuatayo:
Ulinganizi ni nini ndugu zangu katika imani?
Ni upi umuhimu na ubora wa ulinganizi?
Ni lipi lengo na hukumu ya ulinganizi?
Ni ipi misingi ya ulinganizi ?
Ni zipi nguzo za ulinganizi?
Ni zipi njia na aina za ulinganizi?
Umuhimu wa Ulinganizi
Ulinganizi ni kuwaita watu na kuwafundisha uislamu na kuutekeleza kimatendo kwa ajili ya kuwatakia kheri katika maisha yao hapa duniani na kesho akhera.
Umuhimu wa kulingania watu ni kwamba mlinganizi ana daraja kubwa sana mbele ya Mwenyezi Mungu kwa sababu anawaita watu kuwacha ibada zote mbaya na kushikamana na ibada ya Mwenyezi Mungu peke yake. Amesema Mola (Subhaanahu wa Taala): “ Na hakuna mwenye maneno mazuri kuliko yule anayewalingania watu kwa Mwenyezi Mungu na akafanya vitendo vizuri na akasema Mimi ni katika Waislamu”.
Umuhimu wa ulinganizi ni kwamba anapata anayelingania ujira mkubwa. Mtume ﷺ amesema:
[مَنْ دَعَا إِلَى هُدًى كَانَ لَهُ مِنْ الْأَجْرِ مِثْلُ أُجُورِ مَنْ تَبِعَهُ لَا يَنْقُصُ ذَلِكَ مِنْ أُجُورِهِمْ شَيْئًا] رواه مسلم
[Anayelingania katika uongofu atapata ujira sawa na atakayeufuata uongofu huo na hatapunguziwa katika ujira wake kitu chcchote]. [Imepokewa na Muslim]
Umuhimu wa kulingania vile vile ni kutii na kutekeleza amri ya Mtume ﷺ aliposema:
[بلِّغوا عني ولو آية] رواه البخاري
[Nifikishieni hata kama ni Aya moja]. [Imepokewa na Bukhari]
Kulingania hupatikana ndani yake ukamilifu wa kumfuata Mtume ﷺ katika ulinganizi wake wa busara. Mwenyezi Mungu Subhaanahu wa Taala Aasema:
{قُلْ هَٰذِهِ سَبِيلِي أَدْعُو إِلَى اللَّهِ ۚ عَلَىٰ بَصِيرَةٍ أَنَا وَمَنِ اتَّبَعَنِي ۖ وَسُبْحَانَ اللَّهِ وَمَا أَنَا مِنَ الْمُشْرِكِينَ} يوسف:108
[Sema: Hii ndiyo Njia yangu – ninalingania kwa Mwenyezi Mungu kwa kujua – mimi na wanao nifuata. Na ametakasika Mwenyezi Mungu! Wala mimi si katika washirikina.] [Yusuf:108]
Wametofautiana wanavyuoni katika hukumu ya ulinganizi, je ni lazima kwa kila mtu au wakifanya baadhi huwatosheleza wengine?. Wanavyuoni wengine wamesema kwamba ni lazima kwa kila Muislamu na wengine wamesema kwamba wakifanya baadhi ya Waislamu huwatosheleza waliobakia. Lakini ilivyo ni kwamba ulinganizi ni lazima kwa kila Muislamu kulingana na uwezo wake. Amesema Mola Subhaanahu wa Taala:
كُنتُمْ خَيْرَ أُمَّةٍ أُخْرِجَتْ لِلنَّاسِ تَأْمُرُونَ بِالْمَعْرُوفِ وَتَنْهَوْنَ عَنِ الْمُنكَرِ وَتُؤْمِنُونَ بِاللَّهِ ۗ وَلَوْ آمَنَ أَهْلُ الْكِتَابِ لَكَانَ خَيْرًا لَّهُم ۚ مِّنْهُمُ الْمُؤْمِنُونَ وَأَكْثَرُهُمُ الْفَاسِقُونَ
[Nyinyi mmekuwa bora ya umma walio tolewa watu, kwa kuwa mnaamrisha mema na mnakataza maovu, na mnamuamini Mwenyezi Mungu.] [Al-Imraan:110]
Amesema Mtume ﷺ:
[من رأى منكم منكرًا، فليغيره بيده، فإن لم يستطع فبلسانه، فإن لم يستطع فبقلبه، وذلك أضعف الإيمان] رواه مسلم
[Atakayeona jambo baya katika nyinyi basi aliondoshe kwa mkono wake na ikwa hawezi basi aliondoshe kwa ulimi wake(kwa kusema)na ikiwa hawezi basi achukie kwa moyo wake na huo ni udhaifu wa Imani]. [Imepokewa na Muslim]
Nachukua tena fursa hii kuitaja misingi inayotegemewa katika kulingania, nayo ni:
Qur’an Tukufu,
Hadithi za bwana Mtume rehma na amani zimfikie yeye
Sira ya Mtume ﷺ na
Historia ya makhalifa wema waongofu. Misingi tuliyoitaja ndiyo ambayo anayelingania huitumia kuwaita watu katika kheri.
Nguzo za Ulinganizi
Nguzo ambazo ni lazima zipatikane ndio upatikane ulinganizi na nguzo hizo ni kama
zifuatazo:
Mlinganizi
Anayelinganiwa
Kinacholinganiwa
Njia na aina za ulinganizi.
Yatakiwa mlinganizi asifike na apambike na sifa njema alizokuwa nazo Mtume rehma amani zimfikie sifa hizo ni ukweli, uaminifu, kumtakasia Mwenyezi Mungu ulinganizi, ushujaa, upole, maneno mazuri, subira, uadilifu, na sifa nyingine nzuri.
Wanaolinganiwa ni aina tofauti za watu. Kuna Waislamu, wanafiki, makafiri, viongozi, raia, wakubwa na wadogo. Na kila mmoja katika hawa kuna njia na namna yake ya kumlingania.
Kinacholinganiwa ni Uislamu na hii kazi ya Mitume wote. Amesema Mwenyezi Mungu Subhaanahu wa Taala:
{وَلَقَدْ بَعَثْنَا فِي كُلِّ أُمَّةٍ رَّسُولًا أَنِ اعْبُدُوا اللَّهَ وَاجْتَنِبُوا الطَّاغُوتَ}
[Na kwa hakika kwa kila umma tuliutumia Mtume kwamba: Muabuduni Mwenyezi Mungu, na muepukeni Shetani.] [Al-Nnahl:36]
Njia za ulinganizi ni nyingi.
Miongoni mwa njia hizo kuwasiliana na mtu moja kwa moja, kutoa khutba, kuandika vitabu, kufundisha madrasa au vyuo vikuu, kuandika makala gazetini, kutumia vyombo vya utangazaji kufikisha ujumbe kama redio, runinga na vyinginevyo. Kwa hivyo inatakiwa tuwe makini na ufisadi unaopatikana katika vyombo vya habari inatakiwa tuwatahadharishe Waislamu popote waliopo na uovu unaoenezwa na vyombo hivi.
Miongoni mwa aina na sampuli za ulinganizi ni kuwa mfano mzuri wa katika jamii, kujadiliana kwa lengo la kuelimishana, kutumia hikma, pia kutumia mawaidha mazuri, kutumia mifano kwa kutoa visa, na kutumia vitisho na kutia moyo katika mawaidha. Na inatakiwa mlinganizi achague aina ya ulinganizi ambao anaona itakuwa wepesi kukubaliwa ulinganizi wake.
{وَلَا تَقْفُ مَا لَيْسَ لَكَ بِهِ عِلْمٌ ۚ إِنَّ السَّمْعَ وَالْبَصَرَ وَالْفُؤَادَ كُلُّ أُولَٰئِكَ كَانَ عَنْهُ مَسْئُولًا}
[Wala usiyafuate usiyo na ujuzi nayo. Hakika masikio, na macho, na moyo – hivyo vyote vitasailiwa.] [Al-Israa:36]
Pia Amesema Mola Subhaanahu wa Taala:
{وَإِذَا قُلْتُمْ فَاعْدِلُوا وَلَوْ كَانَ ذَا قُرْبَىٰ ۖ وَبِعَهْدِ اللَّهِ أَوْفُوا ۚ ذَٰلِكُمْ وَصَّاكُم بِهِ لَعَلَّكُمْ تَذَكَّرُونَ}
[Na msemapo semeni kwa uadilifu ingawa ni jamaa.] [Al-An’am:152]
Na pia Amesema tena Allah Subhaanahu wa Taala:
{وَقُل لِّعِبَادِي يَقُولُوا الَّتِي هِيَ أَحْسَنُ ۚ إِنَّ الشَّيْطَانَ يَنزَغُ بَيْنَهُمْ ۚ إِنَّ الشَّيْطَانَ كَانَ لِلْإِنسَانِ عَدُوًّا مُّبِينًا}
[Waambie waja wangu waseme maneno mazuri, maana Shet’ani huchochea ugomvi baina yao. Hakika Shet’ani ni adui aliye dhaahiri kwa mwanaadamu.] [Al-Israa:53]
MISINGI YA VYOMBO VYA UTANGAZAJI
Uislamu umeweka misingi kuvifanya vyombo vya utangazaji kuwa imara.
Msingi wa kwanza na muhimu kabisa katika maisha ya watu ni kumuabudu Mwenyezi Mungu peke yake. Amesema Mwenyezi Subhaanahu wa Taala:
{اعْلَمْ أَنَّهُ لَا إِلَٰهَ إِلَّا اللَّهُ }
[Basi jua ya kwamba hapana mungu ila Mwenyezi Mungu] [Muhammad:19]
Mwingine ni kuhisi majukumu wa kuwalingania watu katika njia ya kheri, kuwa mkweli katika maneno na matendo, pia kuwa muadilifu na kuzingatia adabu za mjadala wakati anapojadiliana na kupeana mawaidha mazuri. Amesema Allah Subhaanahu wa Taala:
{ادْعُ إِلَىٰ سَبِيلِ رَبِّكَ بِالْحِكْمَةِ وَالْمَوْعِظَةِ الْحَسَنَةِ ۖ وَجَادِلْهُم بِالَّتِي هِيَ أَحْسَنُ ۚ إِنَّ رَبَّكَ هُوَ أَعْلَمُ بِمَن ضَلَّ عَن سَبِيلِهِ ۖ وَهُوَ أَعْلَمُ بِالْمُهْتَدِينَ}
[Waite waelekee kwenye Njia ya Mola wako Mlezi kwa hikima na mawaidha mema, na ujadiliane nao kwa namna iliyo bora.] [Al-Nnahl:125]