0%

https://uongofu.com/wp-content/uploads/2021/06/services-head-1.png

UMUHIMU WA KUTAFUTA ILIMU YA DINI

UMUHIMU WA KUTAFUTA ILIMU YA DINI

Ilimu ni msingi muhimu katika dini ya Kiislamu. Dini ya Kiislamu imejengwa juu ya Ilimu. Kwasababu Ilimu ndio mwangaza wa kuonyesha njia ya sawa na kuonyesha njia ya mbaya. Aya za kwanza alizo teremshiwa Mtume Muhammad Swalla Llahu ‘alayhi wasallam zilikuwa ni za kufundisha ilimu, na kuhimiza Waislamu wafanye bidii kutafuta ilimu. Amesema Mwenyezi Mungu Subhaanahu wa Taala:

{اقْرَأْ بِاسْمِ رَبِّكَ الَّذِي خَلَقَ خَلَقَ الْإِنسَانَ مِنْ عَلَقٍ اقْرَأْ وَرَبُّكَ الْأَكْرَمُ الَّذِي عَلَّمَ بِالْقَلَمِ عَلَّمَ الْإِنسَانَ مَا لَمْ يَعْلَمْ}

[Soma kwa jina la Mola wako Mlezi aliye umba, Amemuumba binaadamu kwa tone la damu, Soma! Na Mola wako Mlezi ni Karimu kushinda wote! Ambaye amefundisha kwa kalamu. Kamfundisha mtu aliyo kuwa hayajui.]   [Al-Alaq”1-5]
Mwenyezi Mungu(Subhaanahu wa Taala)Ametumia katika Aya hizo maneno kama; soma, ilimu, kalamu, kufundisha, yote haya ni kuonyesha umuhimu wa kutafuta ilimu kwa kupitia njia tofauti za kuweza kukufikisha wewe kupata ilimu hio. Katika Aya hizo kuna ishara ya kuonyesha kwanza kabla ya kufanya vitendo vingine ni lazima mwanadamu apate ilimu ili aweze kutekeleza vitendo vyake kwa ujuzi zaidi na maarifa ya kutosha kinyume na mafundisho hayo, basi mwanadamu atafanya mambo kwa ujinga na baada ya kupata faida na mambo hayo, atapata hasara tupu ima kwa kudhuru nafsi yake au jamii kwa jumla.
Wajibu wa kutafuta Ilimu kabla ya kila kitu katika Mafundisho ya Qur’ani na Sunna

KATIKA QUR’ANI TUKUFU:

Mwenyezi Mungu Subhaanahu wa Taala Amesema:

{فَاعْلَمْ أَنَّهُ لَا إِلَٰهَ إِلَّا اللَّهُ وَاسْتَغْفِرْ لِذَنبِكَ وَلِلْمُؤْمِنِينَ وَالْمُؤْمِنَاتِ ۗ وَاللَّهُ يَعْلَمُ مُتَقَلَّبَكُمْ وَمَثْوَاكُمْ}    محمد:19

[Basi jua ya kwamba hapana mungu ila Mwenyezi Mungu, na omba maghufira kwa dhambi zako na za Waumini wanaume na Waumini wanawake.]   [ Mahammad:19]
Amesema Imam Bukhari katika kitabu chake Sahihi Al-Bukhari: “Mlango unaozungumzia kusoma ilimu kabla ya maneno na vitendo” Makusudio ya Imamu Bukhari ni kutafsiri Aya iliyotangulia ya kumaanisha ilimu mwanzo kabla ya vitendo. Ilimu imetangulizwa kwanza kabla ya kusema au kutenda, kwa sababu, ikiwa maneno na vitendo havikujengwa juu ya msingi wa Ilimu, maneno hayo na vitendo hivyo havina faida kwa mwenye kufanya. Khasara yake ni kubwa kuliko faida yake. Ndio Dini ya Kislamu kwanza ikatilia mkazo watu kusoma na kujuwa kabla ya kufanya vitendo.
Amesema Mwenyezi Mungu Subhaanahu wa Taala:

{إِنَّمَا يَخْشَى اللَّهَ مِنْ عِبَادِهِ الْعُلَمَاءُ ۗ إِنَّ اللَّهَ عَزِيزٌ غَفُورٌ}     فاطر:28

[Kwa hakika wanao mcha Mwenyezi Mungu miongoni mwa waja wake ni wanazuoni.] [Fatir:28]

Mwenyezi Mungu Subhaanahu wa Taala Amesema:

{وَتِلْكَ الْأَمْثَالُ نَضْرِبُهَا لِلنَّاسِ ۖ وَمَا يَعْقِلُهَا إِلَّا الْعَالِمُونَ}    العنكبوت:43

[Na hiyo ni mifano tunawapigia watu, na hawaifahamu ila wenye ilimu.]    [Al-Ankabut:43]

KATIKA SUNNA ZA MTUME ﷺ

Amesema Mtume ﷺ:

[من سلك طريقاً يلتمس فيه علماً سهل الله له به طريقاً إلى الجنة]     رواه مسلم

[Mwenye kufuata njia kwa ajili ya kutafuta Ilimu. Mwenyezi Mungu atafanyia wepesi njia ya kuingia peponi ].   [Imepokewa na Muslim]
Na Amesema Mtume ﷺ katika Hadithi nyingine:

[مَنْ يُرِدِ اللَّهُ بِهِ خَيْرًا يُفَقِّهْهُ فِي الدِّينِ]      رواه البخاري ومسلم

[Mwenyezi Mungu akimtakia kheri mja wake humfundisha ilimu ya dini].   [Imepokewa na Bukhari na Muslim]
Muislamu hawezi Kufahamu Qur’an na Sunna za Mtume ila kwa Ilimu. Ni lazima kwanza ajilazimishe na kusoma ili apate ujuzi wa kufahamu. Bila ya kufanya hivyo, atakuwa ni miongoni mwa waliosifiwa na sifa ya ujinga. Ndugu katika Imani, haya ndio mafundisho ya Allah na Mtume wake, yameweka wazi umuhimu wa kusoma kabla ya vitendo. Kwa hivyo, Allah (Subhaanahu wa Taala) hatokubali kwa mja wake ibada au vitendo vilivyo fanywa bila ya ilimu. Kwa sababu hio, ndio Sheria ya Kiislamu ikaamrisha Waislamu kusoma na ikawa hukumu ya kusoma ni wajibu juu ya kila Muislamu.

MAMBO YANAYO LAZIMU KATIKA KUTAFUTA ILIMU

Kuwa na Ikhlasi, nayo ni kusoma kwa ajili ya Allah Subhaanahu wa Taala. Muislamu lazima awe na lengo kubwa katika kutafuta ilimu nalo ni kusoma kwa ajili ya kutaka raadhi za Allah Subhaanahu wa Taala. Malengo mengine yanakuja baadae. Lakini, la msingi ni kusoma kwa ajili ya Allah Subhaanahu wa Taala.
Kuchunga haki za Mwalimu, kwa kumuheshimu na kumsikiliza vizuri wakati wa kusoma na kuuliza masuali kwa njia ya heshima.
Kupanga mikakati ya kusoma, kwa kutanguliza ilimu ambayo ni muhimu sana,kabla ya nyingine, Mfano wa kusoma ilimu ya faradhi kabla ya ilimu ya sunna.
Kufanyia kazi ilimu, na kuwa na hisia ya jukumu kubwa ulilo libeba. Na kujuwa ya kwamba utaenda kuulizwa ilimu yako mbele ya Allah. Je ulifanyia nini?
Kufundisha watu. Ilimu ni amana kutoka kwa Allah (Subhaanahu wa Taala). Na ili tuweze kutekeleza amana hii kama anavyotaka Mwenyezi Mungu, ni lazima tufanye bidii ya kuwafundisha wengine wasio bahatika kusoma. Amesema Mtume ﷺ:

[خيركم من تعلم القران وعلمه]    أخرجه البخاري

[Mbora wenu, ni Yule aliye jifunza Qur’ani na akafundisha].  [ Imepokewa na Bukhari]

Kwa hakika, ni jukumu kubwa juu ya wasomi kufanya bidii kuifundisha ilimu waliopewa na Mwenyezi Mungu Subhaanahu wa Taala.

KWA FAIDA ZAIDI SIKILIZA MADA NA HII NA SHEIKH HAMMAD QASIM

Toa maoni yako

Begin typing your search above and press return to search.