VIPI TUTAANZA MALEZI BORA KATIKA JAMII ZETU ?
Hatua zifuatazo ni muhimu sana kila mmoja wetu azizingatie ili malezi yasiwe ni ya kubahatisha bali malezi yawe ya kitaalamu na kuwe na malengo ya wazi.Kwa hivyo ni muhimu wazazi wasome malezi yenyewe yanavyotakikana Kusomwa. Kusoma vitabu vya malezi na kumsoma Mtume ﷺ alivyolea watoto wake na alivyofundisha malezi.
1. Kujua namna ya kuchagua mshirika wako katika maisha.Siku zote yataka utazame na kufikiria kuhusu mke au mume mutakayesaidiana naye katika kulea watoto malezi bora.Mtu ambaye mtakuwa na malengo sawa katika malezi ya kufungamanisha kizazi na misingi imara ya Qur’an na Sunnah.
2. Kiwango cha maarifa cha mume na mke kiweze kukaribiana ili kuepuka matatizo mbeleni katika kutazama mambo na kuyapima.Mfano viwango vyenu vya masomo viwe vinalingana mfano mwenye shahada ya ndaki na mwenzake awe anakaribia hapo.
3. Kuwe na ratiba za malezi na ushirikiano baina ya wanandoa lisiachwe jukumu hili kwa mtu mmoja.Mfano baba akifuatilia masomo basi mama ashughulike kwa kutengeneza mazingira mwafaka ya masomo nyumbani.
4. Wazazi wawe mfano mwema kwa watoto wao kwa tabia na wanavyojiweka.Wasitukanane au kutoleana sauti mbele ya watoto wao.Wazazi wawe kielelezo cha kufanya ibada ndani ya nyumba na baba naye ajibidiishe kuswali swala za sunnah ndani ya nyumba yake.Wazazi wasidhihirishe ubaya wao mbele ya watoto.Mfano baba au mama ana udhaifu wa urongo basi asiseme mbele ya watoto au uraibu wa miraa au sigara asiutumie wala kuwatuma watoto.
5. Kuweka vikao vya mara kwa mara vya kifamilia ili kupeana nasiha baina ya wazazi na watoto.Wawashirikishe watoto katika baadhi ya mambo mepesi ya nyumabani na kuwataka ushauri kwa mambo hayo.Kuwasikiliza shida zao na mambo yanayowakereketa.
6. Wazazi wawe waadilifu katika kuwapenda na kuwahudumia watoto wao.Wasiwabague watoto katika huduma muhimu kiasi cha watoto wenyewe kujua kuwa fulani anapendwa zaidi na wazazi kuliko sisi.Jambo hili hupanda chuki baina ya watoto na linaweza kusababisha maafa makubwa.
7. Kufuatilia tabia za watoto wanapokua katika mabadiliko yanayopatikana katika mwili na hisia.Kuwa karibu nao na kuwapa mwongozo wa sawa kama wazazi.Kuwafanya wajue kuwa lengo si kuwanyima uhuru wao bali ni kuwaonyesha ya sawa ambayo yatajenga mustakabali wao.Mfano kumwamrisha mtoto kuswali anapotimu umri wa miaka saba na kumlazimisha anapofikisha miaka kumi na kumuadhibu anapokataa.Kama alivyo sema Bwana Mtume ﷺ:
[مُرُوا أَوْلادَكُمْ بِالصَّلاةِ وَهُمْ أَبْنَاءُ سَبْعِ سِنِينَ ، وَاضْرِبُوهُمْ عَلَيْهَا وَهُمْ أَبْنَاءُ عَشْرٍ ، وَفَرِّقُوا بَيْنَهُمْ فِي الْمَضَاجِعِ] صححه الألباني في صحيح أبي داود
[Waamrisheni watoto wenu kuswali wanapofika miaka saba,na muwapige wanapoacha Swala wakiwa na umri wa miaka kumi,na muwafarikishe katika malazi] [Imesahihiswa na Al-Baniy katika Sunani Abiy Daud]
8. Kuweka risala ya pamoja katika kutekeleza haki ya:
Mwenyezi Mungu Aliyetukuka.
Mtume ﷺ.
Wazazi wawili.
Nasaba yao.
Majirani.
Ummah.
Nafsi.
Haki zote hizi zataka ziwe katika risala ya pamoja wakubaliane kuwa hizi haki zifahamike na zichungwe.
VIPI TUTAWAELIMISHA WATOTO WETU KISAWA ?
Kuwafundisha tawhid nako ni kumpwekesha ALLAH (SWT) na kujitahdhirisha na shirk.
Kuwahifadhisha kitabu cha ALLAH (SWT) kulingana na uwezo wa akili zao.Baada ya hapo ajue maana yake aweze kuizingatia na kuitumia katika maisha yake.Kwa maana hiyo anafaa kuhifadhi,kufahamu,kuzingatia na kuitumia.
Kujua lugha ya kiarabu ambayo ni lugha ya Qur’an na kujifakhiri nayo.
Kumfanya mtume ﷺ kuwa ndiye kielelezo chema katika maisha ya watoto wetu,kwa kusoma hadithi za mtume na sera yake na kuzifanyia kazi
Kuwaheshimu maswahaba wa mtume wote akiwatanguliza makhalifa wanne Abubakar,Omar,Uthman na Ali radhi za Mungu ziwe juu yao wote.
Kuwafundisha Fiqh ya ibada zake zote,swalaa,Swaum,Zakat na Hajj
kuwafundisha namna ya kufikiria na kupanua uwezo wao wa kutoa masuluhisho.
Baada ya kuweka misingi hii imara unaweza kumpeleka shule yenye nidhamu ili kukuza misingi uliyoijenga.Mfano ni shule za mseto zenye masomo ya dini na kisekula akapate maarifa ya kilimwengu pasi na kusahau akhera yake.
TAHADHARI!!!
UKIWEZA KUJIEPUSHA NA ANASA NYUMBANI KWAKO ITASAIDIA SANA KATIKA MALEZI YA WATOTO WAKO.
JAZAKALLAH KHEIR.
Sheikh Abuu Hamza
Mombasa-Kenya