0%

https://uongofu.com/wp-content/uploads/2021/06/services-head-1.png

SOMO LA FIQHI

Ni kila kisichokuwa ni miongoni mwa masharti ya Swala, au nguzo za Swala au Wajibati za Swala hiyo basi itakuwa ni Sunna,mtu akiacha kuleta Sunna,Swala yake haibatiliki wala halazimi kuleta sijda ya sahau bali atakuwa amekosa Thawabu kwa kuacha Sunna.

Na sunna za Swala ni aina mbili:

KWANZA: SUNNA ZA MANENO

1. Dua ya ufunguzi wa Swala: Nayo ni dua inayosomwa baada ya kuleta takbiri ya kufungia Swala na kabla ya kusoma suratul Fatiha.Kama kusoma dua hii

[سبحانك اللهم وبحمدك وتبارك اسمُكَ وتعالى جدك ولا إله غيرك]

[Kutakasika ni Kwako ewe Mwenyezi Mungu , na sifa njema zote ni zako, na limetukuka jina lako, na utukufu niwako, na hapana apasae kuabudiwa kwahaki, asie kuwa wewe.]

au kusoma Dua yoyote nyingine iliyothubutu kutoka kwa Mtume ﷺ na atosoma kwa siri.

2. Kusema  A’UDHU BILLAHI MINA SHETWANI RAJIIM

(Najilinda kwa Mwenyezi Mungu kutokana na Shetani aliyefukuzwa kwenye rehema ya mwenyezi Mungu).Kwa neno lake Mwenyezi Mungu mtukfu:

{فَإِذَا قَرَأْتَ الْقُرْآنَ فَاسْتَعِذْ بِاللَّهِ مِنَ الشَّيْطَانِ الرَّجِيمِ}    النحل 98

[Na ukisoma Qur’ani mwombe Mwenyezi Mungu akulinde na Shetani maluuni.]     [Al Nahl:97]

3. Kusema BISMILLAHI RRAHMANI RRAHIM

(Kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa rehema Mwenye kurehemu)

Kwa hadithi iliyopokewa na Nuaym Al mujmir radhi za Allah ziwe juu yake kwamba yeye aliswali nyuma ya Abuu hurayra akasoma Bismillahi Arrahmani Arrahim kisha akasoma Mama wa Qur’ani… (Suratul Fatiha) na mwisho wa Hadithi asema Abuu Hurayra radhi za Allah ziwe juu yake:

[والذي نفسي بيده إني لأشبهكم صلاة برسول اللّه صلى الله عليه وسلم]   رواه النسائي وأخرجه إبن خزيمة إبن حبان

[Naapa kwa yule nafsi yangu iko mikononi mwake hakika yangu mimi nafanana zaidi na mtume katika swala yangu]    [Imepokewa na Al Nasaai na Ibnu Khuzeymah na Ibnu Hibban]

MAELEZO

Sunna ni kusema bismillahi kwa siri wakati wakusoma suratul Fatihi katika Swala, na Hadithi hii ya Abuu Hurayra inaonyesha kufaa mtu kusoma kwa dhahiri mara nyingine,na Hadithi ya kuonyesha kuwa ni Sunna kusoma kwa siri ni hadithi iliyopokelewa na Imamu Muslim katika Sahihi yake hadithi kutoka kwa Anas radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake asema:

[(صليت مع رسول اللّه صلى الله عليه وسلم وأبي بكر وعمر وعثمان فلم أسمع أحداً منهم يقرأ (بسم اللّه الرحمن الرحيم]

[Nimeswali na Mtume ﷺ na Abuubakar na Umar na Uthmani sijamsikia hata katika wao akisoma Bismillahi Arrahamani Arrahim (kwa dhahiri)]

4. Kusema (Ameen). Na maana yake “Ewe mola itikia”, Kwa hadithi iliyopokelewa na Abuu Hurayara radhi za Allah ziwe juu yake kuwa Mtume amesema:

إذا قال الإمام غير المغضوب عليهم ولا الضَّالِّين فقولوا آمين فإن الملائكة تقول آمين وإن الإمام يقول آمين فمن وافق تأمينه تأمين الملائكة غُفر له ما تقدم من ذنبه     رواه أحمد والنسائي

[Anaposema Imamu Gheyril Maghdhubi alayhi wala Dhwaalliin, semeni Amiin, hakika Malaika wanasema amiin, na Imamu ansema amii, basi yule ambae itafikiana taamini yake, na taamini ya malaika atasamehewa madhambi yake yaliyo tangulia.]    [Imepokewa na Ahmad na Al Nnasaai]

5. Kisomo cha ziada baada ya Suratul Faatiha:

Kuthubutu hilo kutoka kwa Bwana Mtume ﷺkwa hadithi Mutawati zilizo pokewa kwa wingi,na miongi mwa Hadithi hizo ni Hadidhi iliyopokelwa na Anas radhi za Allah ziwe juu yake asema:

جَوَّز رسولُ اللّه صلى الله عليه وسلم ذات يوم الفجر، فقيل يا رسول اللهِ لمَ جَوَّزْتَ؟ قال سمعت بُكاء صبيّ فظننت أن أمه معنا تصلي، فأردت أن أُفْرِغَ له أمه    رواه أحمد

[Alikhafisha Mtume siku moja Swala ya Al fajiri (yaani akasaoma suratul Fatiha peke yake) akaulizwa kwa nini amekhafisha ewe Mtume wa Mungu? akasema nilisikia kilio cha mtoto ni kadhani kuwa mamake yuwaswali nasisi basi nikataka nimalizie mamake]    [Imepokewa na Ahmad]

6. Kisomo cha ziada baada ya RABBANAA LAKAL HAMDU (Mola wetu! Na sifa njema zote ni zako) baada ya kuinuka kutoka kwenye rukuu. Kwa Hadithi iliyopokelewa na Imam Muslim.

ملء السموات وملء الأرض وما بينهما ، وملء ما شئت من شئ بعد .أهل الثناء والمجد،أحق ما قال العبد، وكلنا لك عبد ، اللهم لا مانع لما أعطيت ولا معطي لما منعت ولا ينفع ذا الجد منك الجد

[Zimejaa mbingu na zimejaa ardhi na vilivyomo ndani yake sifa Zako, na zimejaa (sifa Zako)  kwa ulichokitaka baada yake, Wewe ni mstahiki wa sifa na utukufu, ni kweli aliyoyasema mja Wako, na sote ni waja wako, Ee Allaah hapana  anaeweza kukizuia ulichokitoa, na wala kutoa ulichokizuia, na wala haumnufaishi mwenye utajiri, kwani kwao Wewe ndio utajiri.]

7. Maneno ya ziada baada ya kusema RABBIGH FIRLIY (Mola wangu nighufirie) baina ya sijida mbili.Kwa hadithi iliyopokelea na Abuu Daud na Al Tirmidhiy na wengine.

[ اللهم اغفر لي ، وارحمني ، واهدني ، واجبرني، وعافني، وارزقني ، وارفعني]

[Ewe Mwenyezi Mungu nisamehe, na unirehemu, na uniongoze, na uniungie, na unipe afya, na uniruzuku na uniinue.]

8. Tasbihi iliyo zaidi ya moja katika kurukuu na kusujudu.

Kwa hadithi iliyopokelewa na Said bin Jubeyr kutoka kwa Anas radhi ya Allah ziwe juu yake asema:

ما صليت وراء أحد بعد رسول الله صلى الله عليه وسلم أشبه صلاة به من هذا الفتى- يعني عمر بن عبد العزيز- قال فَحَزَرْنا في ركوعه عشر تَسْبيحات وفي سجوده عشر تسبيحات       رواه أحمد وأبوداود والنسائي

[Sijaswali nyuma ya mtu yoyote baada ya Mtume Swala inayofanana na Swala ya Mtume kuliko Swala ya mtoto huyu (Akimkusududia Umar bin Abdilaziiz) asema tukahisabu katika rukuu yake tasbihi mara kumi na katika Sijada yake tasbihi kumi.]      [Imepokewa na Ahmad na Abuu Daud na Al Nasaai]

PILI: SUNNA ZA VETENDO

Nazo ni nyingi miongoni mwazo ni:

1. kuinua mikono pamoja na takbiri ya kufungia Swala, wakati wa kurukuu, kuinuka kutoka kwenye rukuu wakati wa kuinuka kwenda kwenye rakaa ya tatu.

2. Kuweka mkono wa kulia juu ya wa kushoto wakati wa kusimama kabla ya kurukuu na baada yake.

3. Kuangalia mahali pa kusujudu.

4. Kuiepusha mikono iwe kando na tumbo na mbavu wakati wa kusujudu.

5. Kukaa kikao cha iftiraash: nacho ni kukaa hali ya kuinua nyayo za mguu wa kulia na kuvielekeza vidole vyake kibla, hali ya kuweka mguu wa kushoto chini na kuukalia. Kikao hiki kimesunniwa katika vikao vyote vya Swala isipokuwa kikao cha Atahiyatu ya mwisho ya Swala ambayo rakaa zake zinapita mbili.

6. Kikao cha tawarruk: nacho ni kukaa hali ya kusimamisha nyayo za mguu wa kulia na kuzielekeza vidole vyake kibla, na kuziweka nyayo za mguu wa kushoto chini ya muundi wa mguu wa kulia na kuzitoa nyayo upande wa kulia na kukalia kitako kwa kujitegemeza kalio la upande wa kushoto. Kikao hiki ni sunna kwa Attahiyatu ya mwisho ya Swala inayozidi rakaa mbili


Toa maoni yako

Begin typing your search above and press return to search.