0%

https://uongofu.com/wp-content/uploads/2021/06/services-head-1.png

MWEZI WA RAJAB

MWEZI WA RAJAB

Mwezi wa Rajab ni mwezi wa saba katika kalenda ya kiislamu na ni katika miezi mitakatifu ambayo Mwenyezi Mungu Mtukufu ameusia waja wake wasijidhulumu katika Miezi hiyo,

Amesema Mwenyezi Mungu Mtukfu:

إِنَّ عِدَّةَ الشُّهُورِ عِندَ اللَّهِ اثْنَا عَشَرَ شَهْرًا فِي كِتَابِ اللَّهِ يَوْمَ خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ مِنْهَا أَرْبَعَةٌ حُرُمٌ ۚ ذَٰلِكَ الدِّينُ الْقَيِّمُ ۚ فَلَا تَظْلِمُوا فِيهِنَّ أَنفُسَكُمْ   التوبة:36

[Hakika idadi ya miezi kwa Mwenyezi Mungu ni miezi kumi na mbili katika hukumu ya Mwenyezi Mungu tangu alipo umba mbingu na ardhi. Katika hiyo iko mine mitakatifu. Hiyo ndiyo Dini iliyo sawa. Basi msidhulumu nafsi zenu humo]     [Tawba:36]

Na Allah subhanahu Wata’ala kwa hikma yake amefadhilisha baadhi ya siku kuliko siku nyingine, kama alivyo ifadhilisha siku ya ijumaa katika Wiki,na ameifadhilisha baadhi ya Miezi kuliko miezi mengine kama alivyo ifadhilisha miezi hii minne mitakatifu ,Dhulqa’ada, Dhul hijja, Muharram,na Rajab kuliko miezi mengine katika Mwaka,na kadhalika Mitume kwa Hikma yake Subhanah.
Na Waarabu kabla ya Uislamu walikuwa wakiutukuza mwezi huu wa Rajab na wakiuhishimu wakiacha kupigana vita na uhasama, na wameupatia majina tofauti kwa sababu ya kuutukuza kwao, miongi mwa majina hayo;
1 Al’aswam (Kiziwi) kwa sababu walikuwa wakiacha kupigana na kuwa haisikiki milio ya silaha
2. Al’Aswab (wenye kumiminwa) Maqureshi walikuwa wakitakidi kuwa Mwezi wa Rajab Mwenyezi Mungu humimina kheri yake kwa Wingi.
3. Rajm (kufukuzwa) kwa sababu Mashetani hufukuzwa katika Mwezi huu.
Na walikuwa na majina mengi lakini tutosheke na hayo, na majina yote hayo ni kuwa mwezi huu wa Rajab ulikuwa ukihishimiwa na kutukuzwa na waarabu kabla ya kuja Uislamu .
Na Mtume ﷺ asema katika hadithi iliyopokelewa na Abi bakara radhi za Allah ziwe juu yake kwamba Mtume ﷺ alikhutubu katika hija yake akasema:

إن الزمان قد استدار كهيئته يوم خلق الله السموات والأرض، السنة اثنا عشر شهرًا منها أربعة حُرُم، ثلاثة متواليات ذو القعدة وذو الحجة والمحرم، ورجب مُضر الذي بين جمادى وشعبان.   متفق عليه

[Hakika zama zimezunguka kama siku alivyo umba Mwenyezi Mungu mbingu na Ardhi, Mwaka una miezi kumi na mbili, katika hiyo (Miezi ) kuna minne mitakatifu, mitatu imefuatana Dhulqaada, dhulhijja, Muharram na Rajab Mudhwar ulioko kati ya Jumada na Shabani.]    [Imepokewa na Bukhari na Muslim]
Na Mtume ﷺ ameuita Rajab Mudhwar kwa sababu kabla ya Uislamu kulikuwa na Ikhtilafu kuhusu mwezi huu wa Rajab kabila la Rabii’a walikuwa wakisema Rajab ni mwezi wa Ramadhani kwa sababu hiyo wao walikuwa hawau hesabu mwezi huu wa rajab kuwa ni katika miezi mitakatifu na kabila la Mudhwar walikuwa wakiuhishimu Mwezi Huu, ulipokuja Mtume akabainisha kuwa Mwezi mtukufu ni Mwezi huu wa rajab Mudhwar yaani unaotukuzwa na kabila la Mudhwar na akutaka kuweka wazi akabainisha kuwa ni Mwezi ulioko kati ya Jumad na Shabani,na kumesemwa kuwa kabila hili la Mudhwar walikuwa wakiuhishimu mwazi huu wa Rajab zaidi kuliko makabila mengine.

JE KATIKA MWEZI HUU KUNA IBADA MAALUM.

Pamoja na kuwa Mwezi wa Rajab ni katika Miezi Mitakatifu lakini Mwezi Mungu Mtukufu,na Mtume wake ﷺ hawakuhusisha Mwezi huu na ibada Makhsusi, wala hakupokelewa kwa bwana Mtume ﷺ kuwa alikuwa akiuhusisha Mwezi huu wa Rajab kwa ibada, linalo takikana kwa kila muislamu ni kufuata mafundisho tulio fundishwa na Mwenyezi Mungu na Mtume wake, nao ni kujiepusha na kufanya Madhambi katika Mwezi huu,na tusiwe ni wenye kujidhulumu nafsi zetu kama alivyo sema Menyezi Mungu:

{فَلَا تَظْلِمُوا فِيهِنَّ أَنفُسَكُمْ}

[Basi msidhulumu nafsi zenu humo]

Na wala tusifanye lolote lile ambalo hatukufunzwa na dini yetu.

Asema Ibnu Hajar Mwanachuni maarufu Mungu amrahamu:

 لم يرد في فضل شهر رجب، ولا في صيامه، ولا في صيام شيء منه معين، ولا في قيام ليلة مخصوصة فيه حديث صحيح يصلح للحجة.    تبيين العجب  ص:6

“Haikupokelewa katika kufadhilsha Mwezi wa rajab,wala katika kufunga kwake, wala katika kufunga siku Fulani katika mwezi huu wala kuhusisha usiku kwa kisimamo hadithi sahihi ambao inaweza kuitolea hoja.”    [Tabyinul Ujab uk 6]

MAMBO YALIOZUSHWA KATIKA MWEZI WA RAJAB

Katika mwezi huu wa rajab kuna baadhi ya waislamu wanaitakidi mambo mengi ambayo yamezuliwa katika dini na mambo ambayo hayakujulikana wakati wa Bwana Mtume ﷺ wala zama za Makhalifa waongofu, wala karne tatu zilizo bora,na baadhi ya mambo hayo watu wamemzulia Mtume ﷺ hadithi za urongo na waislamu wengi wakaitakidi kuwa ni katika mambo ya kheri kwa sababu ya kutoijuwa dini yao,katika baadhi ya mambo ya uzushi ni kama yafuatavyo:

1. Kusherehekea usiku wa Israa na Miraaj

Baadhi ya waislamu wanasherehekea usiku wa ishrini na saba wa mwezi huu wa Rajab kwa kuwa ndio usiku wa Israai na Miraaji (usiku aliopelekwa Mtume kutoka Makkah hadi Masjidul Aqswaa na kutoka Masjidul Aqswa mpaka uwingu wa saba) na jambo hili si sahihi bali wanazuoni wa tarekhe wamekhitalifiana juu ya hilo,kuna wanaosema kuwa ilikuwa ni 27 mwezi wa mfungo sita na kuna wanaosema ni mwezi wa mfungo saba.Na hata kama tarehe hiyo ya mwezi wa Rajab ni sawa lakini haijapokelewa kutoka kwa Mtume wetu ﷺ wala kwa Maswahaba wa tukufu kuwa walikuwa wakisherehekea siku hiyo, na bila shaka kama ingelikuwa ni Sunna au ni katika jambo la dini wao wangelikuwa wa kwanza kulifanya hilo.

2. Kukhusisha Mwezi wa Rajab na Kufunga

Kuna baadhi ya wailsamu wanaitakidi kuwa ni Sunna kufunga mwezi huu wa Rajab na Shaban na Ramadhan yani kufululiza kufunga miezi mitatu hii kwa pamoja, na kuna Hadithi za kuhimiza waislamu kufunga mwezi huu lakini hadithi hizo karibu zote ni Hadithi Dhaifu na nyingine ni hadithi Maudhui za kupangwa kama walivyosema wanachuoni wa Hadithi.
Asema Ibnul Jawziyah katika kuelezea muongozo wa Mtume ﷺ katika kufunga saumu za Sunna

لم يصم الثلاثة الأشهر سردًا ـ رجب وشعبان ورمضان ـ كما يفعله بعض الناس، ولا صام رجبًا قط، ولا استحب صيامه، بل روي عنه النهي عن صيامه ذكره ابن ماجه . زاد المعاد (2/64

“Hakufunga miezi mitatu kwa mfululizo Rajab na Shaban na Ramadhani kama wanavyo fanya baadhi ya watu,wala hakufunga mwezi wa Rajab kabisa,wala hakusunisha kufunga,bali imepokewa kukataza kufunga kama alivyo taja Ibnu Maajah.”    [Zaadul Ma’aad 2/64]

3. Swalatu Raghaib

Baadhi ya waislamu wanaitakidi kuwa ni Sunna muislamu kuswali Al hamisi ya kwanza katika Mwezi wa Rajab au usiku wa kuamkia ijumaa rakaa kumi na mbili,na imekuja hadithi Maudhui kuhusu swala hii ikielezea namna ya kuswaliwa kwake haina haja ya kuelezea hadithi kama hiyo,la muhimu ni kujuwa kuwa haikuthubutu kutoka kwa mtume Swala Maluum katika Mwezi huu wa Rajab

Asema Imamu Annawawiy Mwanachuoni Marufu wa Madhehebu ya Imamu shafiy Mungu amrahamu

هي بدعة قبيحة منكرة أشد إنكار، مشتملة على منكرات، فيتعين تركها والإعراض عنها، وإنكارها على فاعلها”     فتاوى الإمام النووي  ص:57″

“Hiyo ni Bid’a mbaya yenye kupingwa sana, na imekusanya mambo ya munkar,ni lazima kuiwacha na kuipuuza na kumpinga anae ifanya”     [Fatawal Imamu Annawawiy uk 57]
Hizi ni baadhi ya mambo ya uzushi yaliozushwa katika Mwezi huu wa Rajab,na ni wajibu kwa kila Muislamu ambae alikuwa hajui na akiitakidi mambo kama haya basi akomeke na kuachana na Bid’a kama hizi
Twamuomba allah atujalie tuwe ni wenye kufuata Sunna za bwana Mtume na atuepushe na mambo ya Bid’aa na uzushi.

Toa maoni yako

Begin typing your search above and press return to search.