0%

https://uongofu.com/wp-content/uploads/2021/06/services-head-1.png

MTAZAMO WA UISLAMU JUU YA UTUMWA. (1)

MTAZAMO WA UISLAMU JUU YA UTUMWA.

MAANA YA UTUMWA NA UHURU

Kwanza tujifunze ufafanuzi kuhusu neno utumwa na uhuru, nini tofauti yake.

Maana halisi ya neno “UTUMWA” ni: “Kumilikiwa na mtu jumla na kutokuwa na uhuru wa kujiendesha kwa maamuzi yako, yaani kuwa chini ya miliki ya mtu jumla jumla”.

Na neno “UHURU” ni : “ Kuwa huru katika maamuzi na kutokumilikiwa na mtu”.

Ama neno “UHURU” kwa mujibu wa uislamu ni : “Kitendo cha mtu kuitakasa shingo yake na kuitoa katika utumwa na kuwa mtu huru anaejimiliki mwenyewe”.

Na suala zima la mtu kuwa huru au kuachwa huru ni jambo ambalo limetolewa maelekezo katika Kitabu na Sunna na makubaliano ya Wanachuoni
Ama katika Kitabu cha Allah amesema:

{فَتَحْرِيرُ رَقَبَةٍ مُؤْمِنَةٍ }   النساء 92}

[Ni kuacha huru shingo ya mtu Muumini]    4/92.

Na hadithi zinazo elezea umuhimu wa kuacha huru mtu ni nyingi sana miongoni mwa hadithi hizo ni :

عن أبي هُرَيْرَةَ رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُ, قَالَ النَّبِيُّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ : [ أَيُّمَا رَجُلٍ أَعْتَقَ امْرَأً مُسْلِمًا اسْتَنْقَذَ اللَّهُ بِكُلِّ عُضْوٍ مِنْهُ عُضْوًا مِنْهُ مِنْ النَّارِ]      رواه البخاري

Kutoka kwa abii hurairah allah amridhie anasema: amesema mtume Muhammad rehema na amani zimfikie: [Mtu yeyote akiacha huru mtumwa muislamu, allah atamuokoa mtu huyo kutokana na moto kwa kila kiungo cha mtumwa Yule].   [Imepokewa na Bukhari].

pia wanachuoni wa kiislamu wamekubaliana kuwa mtu akilimiliki mtumwa anatakiwa amuache huru.

Na miongoni mwa wanachuoni wa kiislamu walioandika katika vitabu vyao umuhimu wa jambo hili ni mwanachuoni aitwaye Ibn Hajar. Ambae ameandika katika kitabu chake bubughul-marami somo maalumu linaloelezea umuhimu wa mtu kuwa huru tena somo hili ameliweka mwishoni mwa kitabu chake kwa matarajio ya kutaka Allah amwache huru kutokana na moto.

Kama ambavyo kuna baadhi ya wanachuoni wengine wa kiislamu wanafanya hivyo katika vitabu vyao na waka taja somo hili baada tu ya kuelezea mambo ya mirathi kwa sababu mtu akimwacha huru Mtumwa sheria inampa cheo cha uwalii wa kumrithi huyo aliye mwacha huru kama atakuwa hana watu wa kurithi mali zake katika wanae au jamaa zake wanaostahiki kisheria kumrithi.

Hivyo kila mwanachuoni huandika kitabu chake na kuweka somo moja baada ya jingine kwa kuchunga vitu maalumu anavyoviona katika taaluma yake.

Tunamwomba Allah atuache huru sisi pamoja na wao kutokana na moto wa Jahanam.

SABABU ZINAZOPELEKEA KUMILIKI MTUMWA KATIKA DINI YA KIISLAMU

Sababu za kumiliki Mtumwa katika Dini ya Kiislamu ni mbili tu:

Sababu ya kwanza: Ni mtu kuwa kafiri au (Ukafiri), Yaani endapo pata tokea vita kati ya waislamu na wasiokuwa waislamu na wakafanikiwa waislamu kuwashinda maadui zao na waka wateka wapiganaji na familia zao na wake zao, basi hizi familia na hawa wanawake wote wanakuwa ni watumwa papo hapo kwa kitendo cha kutekwa kwao.

Hivyo mwanzo walikuwa ni watu huru ila baada tu ya kutekwa kwa sababu ya vita ya kisheria ya jihadi wakawa ni watumwa wenye kumilikiwa na waislamu.

Sababu ya pili ya utumwa: Ni matokeo ya kupitia chimbuko la utumwa, yaani endapo kijakazi atakuwa na mmiliki halisi kisha akaja mwanamume mwingine akamuoa mwanamke huyo mtumwa basi inakuwa kila mtoto anaezaliwa na mwanamke huyu anakuwa nae ni mtumwa.

Lakini kama mwanamke huyo mtumwa atazaa na mmiliki wake halisi aliye mnunua au aliyepewa na kiongozi wa kiislamu baada ya kupatikana mateka hao, basi mtoto atakaye zaliwa anakuwa ni mtu huru na sio mtumwa na kwa sababu hii Allah mtukufu amewakataza wanaume wa kiislamu kuwaowa wanawake watumwa ili kutozidisha jamii nyingi ya utumwa, ila tu ameruhusiwa kwa dharura maalumu mtu kuowa mtumwa kama ataogopea kuingia katika uzinifu na pia hana mahari ya kuweza kuowa mwanamke huru.

{ذَلِكَ لِمَنْ خَشِيَ الْعَنَتَ مِنْكُمْ}    النساء: 25 

[hilo (la kuowa mwanamke mtumwa) ni kwa yule tu anae hofia kuingia katika uzinifu]    [Al Nnisaa:25]

JE UISLAMU NDIYO ULIOTESHA MIZIZI YA UTUMWA NA WATUMWA NA HAUJAKATA AU LAA?

Wanasema baadhi ya watu wa nchi za magharibi kutokana na chuki zao juu ya uislamu kwamba uislamu ndio dini inayo endeleza utumwa na imeruhusu kuendelea kuwepo utumwa na umeamrisha kueneza utumwa ulimwenguni.

Tena umehalalisha kwa waislamu kuwafanya wanawake kuwa ni watumwa. Na umelikubali hilo bila ya kuogopa, na umewadhalilisha mateka wa kivita wanawake. Kwa kitendo cha kuruhusu kwamba anaweza mtu mwanaume mmoja kukaa na wanawake hao zaidi ya wanne bila ya ukomo maalumu tena bila ya idadi maalumu kinyume na wanawake huru uislamu umemruhusu mwanamme wa kiislamu kutozidisha zaidi ya wanawake wanne.

Kabla ya kujibu tujiulize kwanza swali hili muhimu sana. Je uislamu ndio chanzo cha utumwa au laa, Yaani je uislamu ndio umeanzisha utumwa au utumwa ulikuwapo hata kabla ya mtume Muhammad kutangaza uislamu?

Jawabu ni kwamba: Utumwa ulikuwepo kablaya uislamu huu alioshushiwa mtume wetu Mohammadi rahma na amani za allah zimfikie , yaani mtume amepewa utume amekuta utumwa upo tayari duniani.

Hivyo basi uislamu sio chanzo cha utumwa, bali uislamu umekuja umekuta tayari utumwa upo. Pia uislamu hauja anzisha njia za utumwa bali uislamu

umeanzisha njia nyingi za kuachwa huru mtumwa.

Kama tulivyosema kwamba uislamu umekuja hali ya kuwa tayari utumwa upo na vyanzo vya utumwa ni vingi yaani njia za watu kuwa watumwa zilikuwa nyingi na rahisi sana. Na njia za mtu kutoka kwenye utumwa na kuwa huru ni chache yaani havizidi moja nayo ni Yule mmiliki mtumwa akubali tu kwa ridhaa yake kumwacha huru mtumwa wake.

Lakini uislamu ulipo fika ukaziba njia zote za kuzalisha watumwa na ukafungua njia nyingi sana za kuwaacha huru watumwa, hali ambayo kipindi cha nyuma kabla ya uislamu kulikuwa na njia moja tu ya kumtoa mtu katika utumwa kama tutakavyoona katika somo letu hili .

VYANZO VYA UTUMWA KABLA YA UISLAMU:

Vyanzo vya kuwaingiza watu katika utumwa kabla ya kuja uislamu ni hivi vifuatavyo:-

1. Mtu kuwa mateka katika vita anakuwa tayari ni mtumwa.
2. Kabila moja likivamiwa na jingine likashindwa nguvu tayari linakuwa kabila lote ni watumwa wa kabila lililowashinda, utumwa huo utaendelea vizazi na vizazi vyao
3. Mtu akifanya dhambi na akataka kutubia anakwenda kwa kiongozi wa jamii hiyo, ima awe kiongozi wa kimila au kiongozi wa kidini, ili atubie dhambi zake na anajitakasa kwa kuwa mtumwa wa kiongozi huyo.
4. Mzazi akisumbuliwa na mwanae na akakasirika anampa mtu mwingine mtoto huyo kwa njia ya utumwa.
5. Mtu akiwa anadaiwa na akashindwa kulipa deni, mwenye kudai anammiliki na kuwa mtumwa wake baada kushindwa kulipa deni.
6. Mtu kutekwa akiwa katika safari zake, akizidiwa nguvu anakuwa mtumwa wa huyo alomteka, kama ilivowahi kutokea kwa swahaba mtukufu zaidu bun haarithah radhi za allah ziwe juu yake.
7. Utumwa wa kurithi kutoka kwa wazazi.
8. Mtu kufanya kosa kwa mtu na kuambiwa ili ni kusamehe lazima uwe mtumwa wangu ndio nakusamehe akubali anakuwa mtumwa.
9. Mtu kuiuza nafsi yake kwa sababu ya uamsikini (ufakiri) au hali ngumu ya maisha wake kwa kusema nipe chakula nile na unifanya mtumwa wako.
10. Mtu kumuuza mwanae kwa sababu ya hali ngumu ya maisha ili akidhi mahitaji yake ya lazima.
Hivyo basi hizi zote tulizo zitaja hapo nyuma ndizo sababu na njia za kumiliki watumwa kabla ya kuja uislamu.
Na ili mtu atoke kwenye utumwa ni hadi yule anae mmiliki amwache huru tu. Na wala hakukuwa na njia zingine za kumtoa mtu katika utumwa hivyo kila siku hadi siku watu walikuwa wanazidi kuwa wengi utumwani.
Hivyo basi baada tu ya kuja uislamu ukaasisi njia nyingi za kutoa watu utumwani na ukawa umebakisha njia moja tu ya utumwa ambayo inatokana na vita kati ya waislamu na wasio kuwa waislamu. Hivyo wale waliotekwa wanakuwa ni mateka na pia ni watumwa.

MAKALA YAENDELEA

IMEANDIKWA NA SHEIKH: ABDULQADIR AL-AHDAL

TAFSIRI:

BASHIRU SHABANI  & AMRY SHAMBULA.

Toa maoni yako

Begin typing your search above and press return to search.