0%

https://uongofu.com/wp-content/uploads/2021/06/services-head-1.png

MASHARTI YA KUWAJIBIKA KUSWALI

MASHARTI YA KUWAJIBIKA KUSWALI

Swala imemuwajibikia kila Muislamu aliyebaleghe (mkubwa) mwenye akili timamu. Zitakapopatikana na kutimia kwa mtu sifa tatu hizi:-

1. Uislamu.

2. Kufikia baleghe (ukubwa) 

3. Akili timamu.

Hapo atakuwa amekalifishwa na kuwajibishiwa na sheria kuitekeleza ibada hii ya swala, na si kuitekeleza tu basi, bali kuitekeleza kwa namna aliyoifundisha kwa maneno na matendo Bwana Mtume ﷺ .

Hebu tuangalie kwa ufafanuzi kidogo sifa tatu hizi ambazo ndizo zinamvika mja taji la kuwajibikiwa na swala. Tuanze na

A. UISLAMU.

Hii ndio sifa ya kwanza au tuseme ndio sifa mama.

Kafiri hawajibiki kuswali kwa sababu hajakuwa Muislamu.

Yaani ili mtu awe na sifa ya swala ni lazima kwanza atamke shahada ambayo itamvisha Uislamu, hapo ndipo atawajibikiwa na swala.

Haya ni kwa mujibu wa kauli ya Bwana Mtume ﷺ alipokuwa akimpa maelekezo swahaba wake Muaadh – Allah amuwiye radhi,

فادعهم إلى أن يشهدوا أن لا إله إلا الله وأن محمدا رسول الله، فإن هم أطاعوا لك بذلك فأخبرهم أن الله فرض عليهم خمس صلوات في كل يوم وليلة    رواه البخاري

[Walinganie washuhudie kwamba hapana Mola pasaye kuabudiwa kwahaki ila Allah pekee na kwamba Muhammad ni Mjumbe wa Allah, ikiwa wao watakutii katika hilo, basi waambie kwamba Allah amewafaradhishia swala tano kila siku, mchana na usiku]      [Imepokewa na Bukhariy.]

B. KUFIKILIA BALEGHE (kwa mkubwa),

Hii ndiyo sifa ya pili inayomfanya mtu kuwajibika kuswali. Sifa hii haimaanishi zaidi ya kuwa swala si wajibu kwa mtoto mdogo.

Sifa hii ya pili tunaipata kupitia kauli ya Bwana Mtume ﷺ:

 [رفع القلم عن ثلاثة عن النائم حتى يستيقظ . وعن الصغير حتى يكبر . وعن المجنون حتى يعقل أو يفيق]   رواه أبوداود والحاكم

[Kalamu imeondoshwa kwa aina tatu za watu : kwa mtu aliyelala mpaka atakapoamka, kwa mtoto mapaka atakapobaleghe na kwa mwendawazimu mpaka atakaporudiwa na akili]    [Abuu Daawaid na Al-Haakim.]

Naam, pamoja na kwamba swala haikufaradhishwa na kuwajibishwa kwa mtoto mdogo, lakini ni sunah na imependekezwa na sheria kwa baba, mama au mlezi wa mtoto aanze kumuamrisha mwanae kuswali atakapofikia umri wa miaka saba.

Na amchape akiacha kuswali wakati akiwa na umri wa miaka kumi. Hizi zote ni hatua za kumjengea mtoto hisia na mazoea ya ibada hii ya swala atakapokuwa mkubwa.

Kwa neno lake Bwana Mtume ﷺ:

[مُرُوا أَوْلَادَكُمْ بِالصَّلَاةِ وَهُمْ أَبْنَاءُ سَبْعِ سِنِينَ وَاضْرِبُوهُمْ عَلَيْهَا وَهُمْ أَبْنَاءُ عَشْرٍ وَفَرِّقُوا بَيْنَهُمْ فِي الْمَضَاجِعِ]   رواه أحمد وأبوداود

[Waamrisheni watoto wenu kuswali watakapofikia umei wa miaka saba, na wapigeni kwa kuiacha (swala) wakifikia miaka kumi na watengeni katika malazi]     [Imepokewa na Ahmad na Abuu Daud]

Yaani watoto wa kiume na wale wa kike wasilale pamoja baada ya kufikia umri wa miaka kumi.

C.  AKILI TIMAMU:

Ili mtu awajibikiwe kuswali ni lazima awe na sifa hii ya akili timamu.

Mwendawazimu hawajibiki kuswali kwa sababu hana nguvu ya kujua alitendalo. Hivyo ndivyo tunavyofahamishwa na kauli ya Bwana Mtume tuliyoitaja katika nukta/kipengele cha pili…

[وعن المجنون حتى يعقل أو يفيق…]

[……na kwa mwendawazimu mpaka atakaporudiwa na akili.]

4. Kusipatikane kiziwizi cha Kumkataza kuswali kama Janaba au Damu ya hedhi na Nifasi kwa Mwanamke.


Toa maoni yako

Begin typing your search above and press return to search.