SOMO LA FIQHI
Sharti tunazozikusudia hapa ni zile sharti za kusihi Swala.
Kwanza kabisa tufahamishe Maana ya sharti :
Sharti ya kitu ni lile jambo au tendo ambalo upatikanaji wa kitu husika unalitegemea jambo/tendo hilo lakini lenyewe si sehemu ya kitu hicho.
Mfano:
Mmea ili upatikane/uwepo juu ya uso wa ardhi unahitaji maji pamoja na kuwa maji sio sehemu ya mmea huo.
Kwa hivyo basi maji ni sharti katika upatikanaji na kuwepo kwa mmea kwani bila ya maji hakuna mmea lakini bado mvua haiwi ni sehemu ya mmea huo.
Baada ya kujua ainisho la sharti, hebu sasa tuziangalie sharti za kusihi kwa swala moja baada ya jingine :
Suali: Ni yapi Mashrti ya kusihi Swala?
Jawabu: Masharti ya kusihi Swala ni haya yafuatayo:
1. KUINGIA WAKATI
Swala ya faradhi ina wakati ambao haiswihi kabla yake, wala baada yake isipokuwa kwa dharura. Asema Mwenyezi Mungu aliyetukuka:
{إِنَّ الصَّلَاةَ كَانَتْ عَلَى الْمُؤْمِنِينَ كِتَابًا مَّوْقُوتًا} النساء:103
[Hakika Swala kwa Waumini ni faradhi iliyo wekewa nyakati maalum.] [4: 103]
yaani imefaradhiwa katika vipindi maalumu.
2. KUTWAHIRIKA NA HADATHI
A. Kutwahirika na hadathi ndogo (tukio la kutokuwa na udhu)
Nako kunapatikana kwa kutawadha. Mtume ﷺ anasema:
[لا يقبل الله صلاة أحدكم إذا أحدث حتى يتوضأ] رواه البخاي
[Mwenyezi Mungu hatakubali Swala ya mmoja wenu akitokewa na tukio la kutokuwa na udhu mpaka atawadhe.] [ Imepokewa na Bukhari.]
B. Kutwahirika na hadathi kubwa:
nako ni kunapatikana kwa kuoga, kwa neno la mwenyezi Mungu Aliyetukuka:
{وَإِن كُنتُمْ جُنُبًا فَاطَّهَّرُوا} النساء:6
[Na mkiwa na janaba jitwahirisheni.] [5: 6]
Na yoyote atakayekumbuka akiwa katika Swala kuwa hana udhu au ametokewa na jambo la kuharibu udhu katikati ya Swala, basi Swala yake itatanguka Na itamlazimu ajitoe Swalani ili ajitwahirishe na bila ya kutoa Salamu, kwa kuwa swala ishatanguka na bado haijamalizika, na utoaji salamu ndio mwisho wa Swala.
3. UTWAHARA WA NGOO, MWILI NA MAHALI.
A. Utwahara wa nguo,
kwa neno lake Mwenyezoi Mungu aliyetukuka:
{وَثِيَابَكَ فَطَهِّرْ} المدثر:4
[Na nguo zako twahirisha] [74: 4]
B. Utwahara wa mwili
kwa ilivyothubutu kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu ﷺ aliipita kwenye kaburi mbili akasema:
[إنهما ليعذبان ، وما يعذبان في كبير ؛ أما أحدهما فكان لا يستتر من البول] رواه البخاري
[Hakika wawili hawa wanaadhibiwa, Na hawaadhibiwi kwa jambo kubwa, Ama huyu alikuwa hajiepushi na hajikingi na mkojo.] (na mkojo usimuingie) [Imepokewa na Bukhari.]
C. Utwahara wa mahali.
kwa hadithi ya mbedui aliyekojoa msikitini, Mtume ﷺ alisema:
[دعوه وأهريقوا على بوله ذنوباً من ماء – أو سجلا من ماء ] رواه البخاري ومسلم
[Muacheni na umwagieni mkojo wake ndoo ya Maji.] [Imepokewa na Bukhari na Muslim.]
Suali: Mtu anapokosa sehemu ya kuswali atafanya nini?
Jawabu: Ardhi yote ni msikiti, kwa kuwa kuswali hapo inafaa. Mtume ﷺ amesema:
[وجعلت لي الأرض مسجدا وطهورا، وأيما رجل من أمتي أدركته الصلاة فليصل] رواه البخاري ومسلم
[Nimefanyiwa ardhi kuwa ni mahali pa kuswali na mahali pakujitwahirishia. Basi mtu yoyote miongoni mwa umma wangu aliyeingiliwa na kipindi cha Swala na aswali.]
[Imepokewa na Bukhari na Muslim.]
Suali: Ni sehemu gani zinazo katazwa mtu kuswali?
Jawabu: Sehemu zilizokatazwa, mtu kuswali ni kama vile kuswali makaburini na chooni, na sehemu ya malazi ya ngamia,kwa kuwa Mtume ﷺ alisema:
[الأرض كلها مسجد إلا المقبرة والحمام] رواه الترمذي
[Ardhi yote ni mahali pa kuswali, isipokuwa makaburini na chooni.] [Imepokewa na Tirmidhi.]
Na dalili ya sehemu ya malazi ya ngamia ni kauli yake Mtume ﷺ:
[ولا تصلوا في أعطان الإبل] رواه الترمذي
[Musiswali katika malazi ya ngamia] [Imepokewa na Tirmidhi.]
4. KUSITIRI TUPU.
Na tupu ya mwanamume: ni kuanzia kitovuni hadi gotini.
Ama tupu ya mwanamke: ni mwili wake wote isipokuwa uso na vitanga vya mikono.
na dalili ni neno lake Mwenyezi Mungu aliyetukuka:
{خُذُوا زِينَتَكُمْ عِنْدَ كُل مَسْجِدٍ} الأعراف:31
[Enyi wanaadamu! Chukueni pambo lenu kwenye kila pahala wakati wa ibada,] [Al-A’araaf:31]
قَال ابْنُ عَبَّاسٍ رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُمَا : الْمُرَادُ بِالزِّينَةِ فِي الآْيَةِ : الثِّيَابُ فِي الصَّلاَةِ
Asema Ibnu Abbas radhi za Allah ziwe juu yake “Makusudio ya pambo katika aya hii,ni kuvaa nguo katika Swala.”
Na kwa neno lake Mtume:
[لاَ يَقْبَل اللَّهُ صَلاَةَ حَائِضٍ إِلاَّ بِخِمَارٍ] رواه أبوداود والترمذي
[Hakubali Mwenyezi Mungu swala ya Mwanamke alieingia hedheni (alie baleghe) ila kwa mtandio] [Imepokewa na Abuu Daud na Al-Ttirmidhiy]
FAIDA
Kufinika mabega
Inamlazimu mwenye kuswali avae nguo yenye kufinika mabega yake na shingo yake, kwa kuwa Mtume alisema:
[لَا يُصَلِّي أَحَدُكُمْ فِي الثَّوْبِ الْوَاحِدِ لَيْسَ عَلَى عَاتِقَيْهِ شَيْءٌ] رواه مسلم
[Asiswali mmoja wenu kwa nguo moja bila ya kuwa kwenye mabega yake kitu chochote.] [Imepokewa na Muslim.]
Na kufanya hivyo ni Sunna kwa kauli ya jamhuri ya wanachuoni,na ni kuhishimu ibada ya Swala,isipokuwa Madh’habu ya imamu Ahmad anaona ni wajibu kufanya hivyo katika Swala ya Faradhi.
5. KULELEKEA KIBLA.
Kwa neno lake Mwenyezi Mungu Aliyetukuka:
{فَوَلِّ وَجْهَكَ شَطْرَ الْمَسْجِدِ الْحَرَامِ ۚ وَحَيْثُ مَا كُنتُمْ فَوَلُّوا وُجُوهَكُمْ شَطْرَهُ] البقرة:144
[Basi elekeza uso wako upande wa Msikiti Mtakatifu; na popote mnapokuwa zielekezeni nyuso zenu upande huo.] [Al-Baqara:144]
MAELEZO KUHUSU KUELEKEA KIBLA
A. La wajibu kwa mwenye kuswali ndani ya msikiti wa Haram aielekee alkaba yenyewe. Ama yule anayeswali akiwa mbali na Alkaaba, basi ataelekea upande wa hiyo Alkaba na sio kuielekea yenyewe, kwa kuwa hawezi kuielekea yenyewe. Kwa hivyo, Mtume ﷺ alisema:
[ما بين المشرق والمغرب قبلة] رواه الترمذي
[baina ya mashariki na magharibi ni kibla.] [Imepokewa na Tirmidhi]
2. Swala ya Sunna kwa aliyepanda mnyama, kibla chake ni ule upande ambao kile kipando kinaelekea, kwa kuwa ilithubutu kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu alikuwa akiswali juu ya kipando chake akielekea popote pale kile kipando kinapoelekea, na alikiswali witri juu yake, isipokuwa yeye hakuwa akiswali juu yake Swala za faradhi] [Imepokewa na Abu Dawud.]
Suali: Asiyejua Kibla Atafanya Nini?
Jawabu: Asiyejua kibla akiwa kwenye jengo au mahali penye watu walio karibu, atauliza au atajijulisha kibla kwa vibla vya misikiti au dira au jua au mwezi au vinginevyo. Akitoweza kujua basi atajitahidi na atafuata lile lenye nguvu katika dhana yake, kwa neno lake Mwenyezi Mungu:
{فَاتَّقُوا اللَّهَ مَا اسْتَطَعْتُمْ} التغابن:16
[Muogopeni Mwenyezi Mungu vile mnavyoweza] [64: 16]