0%

https://uongofu.com/wp-content/uploads/2021/06/services-head-1.png

MAMBO MAKUBWA YALIYOTOKEA KABLA YA KUZALIWA MTUME ﷺ

AR-RAHEEQ AL- MAKHTUUM


 Mambo Adhimu Yaliyotokea Kabla Ya Kuja Kwa Muhammad ﷺ.
Bila shaka jambo lolote adhimu hutanguliwa na matukio, dalili na bishara mbali mbali adhimu yakiwa kama ni ishara ya kulikaribisha jambo hilo. Na wanadamu hawajapata kutokewa na jambo adhimu kuliko hili la kuzaliwa kwa Al-Habiyb Al-Mustwafaa Muhammad .

KUFUKULIWA KISIMA CHA ZAMZAM 

Anasema Ibn Kathiyr katika ‘Al-Bidaayah wan-Nihaayah’:

“Amesema Ibn Is-haaq; nimehadithiwa na Yaziyd bin Abi Habib Al-Masri kutoka kwa Murthad bin ‘Abdillaah Al-Yazni kutoka kwa ‘Abdullaah bin Zarir al-Ghafiqiy kuwa alimsikia ‘Aliy bin Abi Twaalib (Radhiya Allaahu ‘anhu) akihadithia hadithi ya Zamzam alipoamrishwa ‘Abdul-Muttwallib kukichimba. Anasema: “Alisema ‘Abdul-Muttwallib:

“Nilipokuwa nimelala chumbani kwangu nikasikia sauti usingizini ikiniambia: “Chimba At-Tiyba”.

Akasema:

“Nikauliza: “Nini At-Tiyba ?” lakini mtu huyo akatoweka.

Ulipoingia usiku wa pili yake nikaenda kitandani pangu kulala na mtu yule akanijia tena usingizini, akaniambia:

“Chimba Barrah” nikamuuliza:

“Ni nini hii Barrah?” kisha akatoweka tena.

Na usiku uliofuata nikaenda kitandani pangu kulala, akanijia akaniambia:

“Chimba Al-Madhnuwnah,” nikamuuliza:

“Nini Al-Madhnuwnah?” akatoweka. Usiku uliofuata nikaenda kitandani kulala, akanijia tena akaniambia:

“Chimba Zamzam”  nikamuuliza:

“Nini Zamzam?”

Akaniambia:

لا تنزف أبداً ولا تذم ، تـسقي الحجيج الأعـظم وهي بين الفرث والدم عند نقرة الغراب الأعصم ، عند قرية النمل

“Hakikauki abadan, wala hayapunguwi maji yake. Kitawanywisha mahujaji watukufu,na kipo baina ya mavi na damu, karibu na mahali atakapodokowa kunguru mwenye miguu meusi, penye kichungu cha sisimizi.”

Anasema Ibn Is-haaq:

“Alipojulisha utukufu wake na kufahamishwa mahali kilipo na alipojua kuwa aliyoyasikia ni ya kweli, asubuhi ilipoiniga akachukua jembe lake na kuondoka pamoja na mwanawe Al-Haarith, na wakati huo hakuwa na mtoto mwengine isipokuwa huyo, akaanza kuchimba na alipoyafikia maji akapiga takbir, na Maquraysh watu wa kabila la Bani Umayyah wanaotokana na Bani Abdu Manaf wakajua kuwa keshapata alichokitaka wakamwendea na kumwambia:

“Ewe ‘Abdul-Muttwallib! Hiki ni kisima cha baba yetu Ismaail, na sisi tuna haki yetu ndani yake kwa hivyo utushirikishe na sisi pia.”

Akasema:

“Sitofanya hivyo, jambo hili nimehusishwa nalo peke yangu na nyinyi hamumo na nimechaguliwa mimi kati yenu nyote.”

Wakamwambia:

“Tupe haki yetu kwani sisi hatutokuacha mpaka tumtafute atakayehukumu baina yetu.”

Akasema:

“Mchagueni mnayemtaka ahukumu baina yetu.”

Wakasema:

“Mpiga ramli mwanamke wa kabila la Bani Sa’ad Hudhaym.”

Akasema:

“Nimekubali.”

Anasema Ibnu Is-haaq:

“Mpiga ramli huyo alikuwa akiishi karibu na nchi ya Shaam, na ‘Abdul-Muttwallib akapanda farasi wake, nao wakapanda farasi wao pia, na kutoka katika kila kabila akatoka mtu mmoja, wakafuatana na kuianza safari ndefu kuelekea Sham., na ardhi yote wakati huo ilikuwa jangwa, walipofika katika sehemu mojawapo ya jangwa hilo iliyopo baina ya Hijjahz na Sham maji ya ‘Abdul-Muttwallib na ya wenzake yakamalizika, wakashikwa na kiu na walipotambua kuwa watakuja kufa kiu, wakawaomba Maquraysh waliofuatana nao, wakakataa wakasema:

“Na sisi tuko jangwani pia, tunajiogopea nafsi zetu yasije yakatukuta yalokukuteni.”

‘Abdul-Muttwallib akawauliza wenzake:

“Mnaonaje?”

Wakasema:

“Tupe rai yako na sisi tuko tayari kukufuata.”

Akasema:

“Mimi naona kwa vile bado tuna nguvu zetu, bora kila mmoja wenu ajichimbie shimo lake na kila atakapokufa mmoja, basi wenzake wamsukume ndani ya shimo lake kisha wamfukie mpaka atakapobaki mmoja tu kati yenu, na akipotea mtu mmoja bora kuliko kupotea kundi zima.”

Wakasema:

“Rai yako ni nzuri sana.”

Wakashuka, na kila mmoja wao akaanza kujichimbia shimo lake kisha wakakaa kila mmoja akisubiri kifo chake.

‘Abdul-Muttwallib akawaambia wenzake”

“WaLlaahi huku kukaa kwetu tukiyangoja mauti ni uvivu, kwa nini tusiendelee na safari, huenda tukabahatika kuufikia mji tukapata maji? Inukeni tuendelee na safari.”

Wakainuka na kumsubiri ‘Abdul-Muttwallib apande farasi wake, na alipokuwa akimpanda farasi wake, pakatokea mpasuko chini ya farasi wake na maji matamu yakaanza kutoka, akawaita makabila yote ya Kiquraysh aliofuatana nao akawaambia:

“Njooni mpate kunywa maji, kwani Allaah ndiye aliyetuletea maji haya, kwa hivyo kunyweni, jazeni viriba vyenu na wapeni farasi wenu pia.”

Wenzake wakasema:

“WaLlaahi Allaah keshatoa uamuzi wake juu ya kisima cha maji ya Zamzam, kwa hivyo hatutoshindana na wewe abadan. Bali yule aliyekuletea maji katika jangwa hili ndiye aliyekuletea kisima cha Zamzam, kwa hivyo rudi katika kisima chako ukiwa mshindi.”

Wakarudi wote pamoja na hawakumuendea tena mpiga ramli.[1]


[1] Muhammad ﷺ Rahma Kwa Walimwengu.


Toa maoni yako

Begin typing your search above and press return to search.