AR-RAHEEQ AL-MAKHTUM
Aya zenyewe zimekusanya mada za Da’awa na ufikishaji wa ujumbe. Kukhofisha nafsi kuna maana ya kuwa yapo matendo ambayo huwa na mwisho mbaya, ambao watakutana nao wenye matendo hayo. Jambo hili ni kuyaangalia yale yanayojulikana na kila mmoja wetu, nayo ni kuwa duniani si mahala pakulipwa kwa matendo yote yanayofanywa na watu, hali hairuhusu kulipwa kwa matendo yote. Hivyo kukhofisha kunaashiria kuwa ipo siku ya malipo ambayo si katika siku hizi za duniani. Hiyo huitwa siku ya Kiyama. Siku ya Malipo, na hili ni jambo linalolazimisha maisha mengine yasiyokuwa haya tunayoishi hapa duniani.
Aya zilizobakia zinataka waja wampwekeshe Mwenyezi Mungu ﷻ kwa uwazi na kuyategemeza mambo yao yote kwa Mwenyezi Mungu ﷻ Aliye Mtukufu na kuacha matakwa ya nafsi na matakwa ya watu wengine ili kupata radhi za Mwenyezi Mungu (s.w.t). Kwa msingi huo mada hizi zinafupishwa katika mambo yafuatayo:
(1). Kumpwekesha Mwenyezi Mungu ﷻ (Tawhiid)
(2). Kuiamini siku ya mwisho (Kiyama).
(3). Kusimama imara na kuitakasa nafsi kwa kuacha mambo machafu na maovu, ambayo husukuma watu kwenye ubaya wa mwisho, na badala yake kusimama imara na kutenda mambo mazuri, bora na makamilifu na matendo mengine ya kheri.
(4). Kuyategemeza mambo yote kwa Mwenyezi Mungu ﷻ Aliye Mtukufu.
(5). Yote haya yafanywe baada ya kuuamini ujumbe wa Mtume Muhammad (s.a.w) na kuwa chini ya uongozi wake ulio bora na maelekezo yake yaliyo maongofu. Kwa hakika mwanzo wa aya umekusanya wito wa juu- katika sauti ya Aliye Mkubwa, Mtukufu, kwa kumwita Mtume ﷺ kwa ajili ya jambo hili tukufu, alimchagua kutoka katika usingizi na kujifunika na kumuelekeza kwenye Jihadi, mapambano, taabu na mashaka:
{يَا أَيُّهَا الْمُدَّثِّرُ قُمْ فَأَنذِرْ}
[Ewe Mwenye kujifunika, simama uonye] … [74:1-2]
Hii ni kama vile kuambiwa yule ambaye anaishi kwa ajili ya nafsi yake au ni mwenye kupumzika tu: ‘Wewe ambaye umepewa mzigo huu mkubwa unanini wewe mpaka ulale? Una nini wewe mpaka utake mapumziko? Una nini wewe mpaka utake tandiko lenye Joto? Maisha ya utulivu? Starehe yenye kupumzisha?’ Simama kwa ajili ya jambo kubwa ambalo linakungojea; Simama kwa ajili ya mzigo mzito ambao umeandaliwa kwa ajili yako; Simama kwa ajili ya taabu na usumbufu; Simama kwa hakika wakati wa kulala na raha umepita kuanzia leo, kumebakia kwako kukesha kwa muda mrefu na jihadi ndefu iliyo ngumu; Simama ujiandae kwa ajili ya jambo hili na jitayarishe.’
Hakika haya ni maneno makubwa yenye kutisha yaliyomng’oa Mtume ﷺ kutoka katika joto la godoro, katika nyumba tulivu, ngome yenye joto na kumsukuma kwenye mkondo mkubwa wa kuvutana na kukaza dhamira za watu katika uhalisia sawa wa mambo ya maisha ya kila siku.
Baada ya aya hizi Mjumbe wa Mwenyezi Mungu ﷺ alisimama kwa zaidi ya miaka ishirini, akitekeleza jukumu alilopewa. Hakupurnzika na hakutulizana na hakuishi kwa ajili ya nafsi yake, wala watu wake wa nyumbani, alisimama na akaendelea wakati wote akiwalingania watu juu ya Mwenyezi Mungu ﷻ. Akaubeba mzigo mzito mabegani kwake, na wala hakuuona kuwa ni mzito, pamoja na kuwa ulikuwa ni mzigo wa amana kubwa kabisa katika ardhi hii. Mzigo wa kuwaongoza wanaadamu wote, mzigo wa itikadi yote, mzigo wa mapambano na Jihadi katika viwanja mbalimbali, aliishi katika vita vyenye kuendelea zaidi ya miaka ishirini, matukio makubwa makubwa yakawa yanafuatana. Hakupumzika kati ya tukio na jengine kwa kipindi cha muda mrefu, tokea aliposikia wito wa juu ulio Mtukufu, na akapokea kutoka katika wito huo majukumu
makubwa kabisa. Tunamwomba Mwenyezi Mungu ﷻ Amlipe malipo mema. (1)
Nyaraka zifuatazo hazikuwa, isipokuwa ni sura ndogo ya kawaida katika Jihadi hii ndefu iliyokuwa ngumu, ambayo aliishi nayo Mjumbe wa Mwenyezi Mungu ﷻ kwa muda mrefu katika maisha yake.
1) Fiy Dhilalil-Qur’an, Tafsiri ya sura mbili za Al-Murzammil na al-Mudatihir.
* Ar-Raheeq Al Makhtum 116