SOMO LA FIQHI
MAANA YA NUSUK
Nusuk Kilugha: Ni Ibada
Nusuk kisheria: Ni maneno yanayosemwa na vitendo vinavofanywa na Mwenye kuhiji au kufanya Umra.
NIA YA IBADA YA HIJJA (NUSUK)
Anapomaliza kuoga na kujinadhifisha yule anayetaka kuhirimia, akavaa nguo za ihramu, na mwanamume akatoa nguo za mzunguko, atanuilia kuingia kwenye ibada ya Hijja au Umra.
Na inapendekezwa aitamke aina ya ibada anayoikusudia. Aseme akikusudia Umra kisha kujistarehesha mpaka Hijja:
[لبيك اللهم عُمْرَة متمتعًا بها إلى الحج]
LABBAYKA ALLAHUMMA UMRATAN MUTAMATIAN ILAA-L HAJJI
Nakuitikia, ewe Mola, kwa kufanya Umra hali ya kujipumzisha nayo mpaka nifanye ibada ya Hijja
au aseme:
[لبيك اللهم عُمْرَة]
LABBAYKA ALLAHUMMA UMRATAN
Nakuitikia kwa kufanya Umra kisha wakati wa Hijja aseme:
[لبيك اللهم حجًّا]
LABBAYKA ALLAHUMMA HAJJA
Nakuitikia kwa kuhiji. Na mwenye kuzishikanisha pamoja Hijja na Umra atasema:
[لبيك اللهم حجًّا وعُمْرَة]
LABBAYKA ALLAHUMMA HAJJAN WA UMRAH
Nakuitikia kwa Hijja na Umra.
Kwa hadithi ya Anas Radhi za Allah ziwe juu yake kuwa alisema: Nilimsikia Mtume wa Mwenyezi Mungu ﷺ akisema:
[لَبَّيْكَ عُمْرَةً وَحَجًّا]
[Nakuitikia Kwa kuhiji na kufanya Umra] [Imepokewa na Bukhari na Muslim.].
Na asipotamka chochote nia ya moyoni inamtosheleza.