AR-RAHEEQ AL-MAKHTUM
Sauti ya ukweli haikuacha kuvuma katika pande zote za Makka, mpaka ilipoteremka kauli ya Mwenyezi Mungu ﷻ Aliye Mtukufu:
{فَاصْدَعْ بِمَا تُؤْمَرُ وَأَعْرِضْ عَنِ الْمُشْرِكِينَ}
[Basi (wewe) yatangaze uliyoamrishwa (wafa usijali upinzani wao) na ujitenge Mbali na (Vitendo ‘Vya) hao washirikina.] [15:94]
Mjumbe wa Mwenyezi Mungu ﷺ akasimama na kuwaonya dhidi ya mambo ya ovyo ya kishirikina na upuuzi wake. Akawa anawabainishia ubaya wa masanamu na udhaifu wake, akawa akitoa mifano mingi, kuonyesha udhaifu wa hayo masanamu. Akawawekea wazi, kwa kuzitumia dalili zilizowazi, kuwa mwenye kuyaabudu masanamu, na akayafanya kuwa ni kiungo kati yake na Mwenyezi Mungu ﷻ kwa hakika mtu huyo atakuwa katika upotevu ulio wazi.
Watu wa Makka walighadhibishwa, walishangaa na kugutuka wakati waliposikia sauti inayodhihirisha ukweli, kuwakhofisha na upotevu, ushirikina na watu waliokuwa wakiabudu masanamu. Sauti yake ilifanana na sauti ya radi iliyoyavunja mawingu, ikatoa mweko na kulitetemesha anga lililokuwa tulivu.
Makuraishi walisimama na kujiandaa kuyazima mageuzi na mapinduzi haya yaliyochomoza ghafla, kwa vile walipata khofu kuwa mageuzi haya yangeondosha mambo yao ya kuiga na yale ambayo waliyarithi.
Makuraishi walisimama imara katika msimamo wao kwa sababu waliamini kuwa maana ya kuamini ni kuukanusha Uungu kwa asiyekuwa Mwenyezi Mungu ﷻ, na maana ya kuuamini Utume na siku ya mwisho ni kujisalimisha kikamilifu na kutegemeza mambo yote moja kwa moja kwa Mwenyewe Mwenyezi Mungu ﷻ na kuwa haingebaki kwao khiyari (uhuru) katika nafsi zao au mali zao, sembuse kwa watu wengine.