0%

https://uongofu.com/wp-content/uploads/2021/06/services-head-1.png

JE UNATAKA HUSNUL KHAATIMAH (MWISHO MWEMA)?

JE UNATAKA HUSNUL KHAATIMAH (MWISHO MWEMA)?

Je, unataka Husnul-Khaatimah (mwisho mwema )? Basi Ishi maisha mema!
Ee binaadamu! Mche Mwenyezi Mungu na jiandae kukutana na Mola wako kwa maandalizi ya waja wema. Hakika hali ya (kila) mwanadamu ni kama Anavyosema Mwenyezi Mungu ﷻ:

{يَا أَيُّهَا الْأِنْسَانُ إِنَّكَ كَادِحٌ إِلَى رَبِّكَ كَدْحاً فَمُلقِيهِ}

[Ewe mtu! Hakika wewe unajikusuru kwa juhudi kumwendea Mola wako Mlezi, basi utamkuta]   [Al-Inshiqaaq 84:6]
Ewe Muislamu, hakika binaadamu hajui wapi atafariki wala hajui lini atafariki kama Anavyosema Mwenyezi Munguﷻ 

{وَمَا تَدْرِي نَفْسٌ مَاذَا تَكْسِبُ غَداً وَمَا تَدْرِي نَفْسٌ بِأَيِّ أَرْضٍ تَمُوتُ إِنَّ اللَّهَ عَلِيمٌ خَبِيرٌ}

[Na haijui nafsi yoyote itachuma nini kesho. Wala nafsi yoyote haijui itafia nchi gani. Hakika Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye kujua, Mwenye khabari.]    [Luqmaan: 34]

Ikiwa hatujui tutakachokichuma kesho, jambo ambalo ni katika matendo yetu, basi hakika hatujui pia lini tutakufa kwani hilo ni katika matendo ya Mwenyezi Mungu. Na ikiwa hatujui nchi (au mahali) gani tutakufa juu ya kwamba mtu anakwenda nchi (au mahali) anayoichagua mwenyewe, basi hakika yeye hajui lini atakufa. Kwa hivyo basi, mahali pa kufariki na wakati wa kufariki haujulikani! Tunamuomba Mwenyezi Mungu Aturuzuku husnul-khaatimah (mwisho mwema)

Na si muhimu mtu kujua kufariki lini wala kufariki wapi. Hakika hakuna la muhimu isipokuwa jambo la muhimu ni katika hali gani mtu atafariki? Hili ndilo la muhimu; atafariki katika hali gani? Je, utafariki ukiwa katika Imani na ikhlaasw na Tawhiyd? Tunamuomba Mwenyezi Mungu Atujaalie hayo yote (kufariki katika hali hizo za Imani, ikhlaasw na Tawhiyd). Au je utafariki katika shaka na shirki na kufuru na ukanushaji? Hili ndilo muhimu, hili ndio! Lakini anayetaka kufariki kifo kizuri, basi afanye kheri kwani Mwenyezi Mungu ni Mkarimu mno na Mpaji mno Hatomwacha mja Wake katika dhiki ikiwa mja atakuwa ni mwenye kumkumbuka (na kumdhukuru) Mwenyezi Mungu wakati anapokuwa katika hali ya raha. Mtume ﷺ amesema:

[تَعَرَّفْ إلَى اللَّهِ فِي الرَّخَاءِ يَعْرِفُك فِي الشِّدَّةِ]      رواه أبو القاسم بن بشران في أماليه

[Mjue Mwenyezi Mungu katika (hali ya raha) Atakujua ukiwa katika shida (au dhiki)]   [Imepokewa na Abuul Qaasim bin Bishraan]

Imetajwa kutoka kwa Salaf (Maswahaba na wema waliotangulia) kwamba binaadamu yanapomfikia mauti, Shetani humdhihirishia dini ya Kiyahudi, ya Kinaswara (Kikristo) na ya Kiislamu, na kwamba shetani hujifafanisha sura ya baba yake huyo mtu. Kisha husema: “Ee mwanangu! Usiache dini ya Kiyahudi, usiache dini ya Kinaswaara!” (Huendelea kumshawishi) mpaka mtu hufariki katika mojawapo wa dini hizo mbili batili, zilizofutwa ambazo Mwenyezi Mungu Hazikubali! Wa-Allaahi (naapa kwa Allaah!) hii hakika ni fitnah kubwa kabisa! Lakini kwa neema ya Allaah, na kama alivyosema Shaykhul-Islaami Ibn Taymiyyah  (Mungu amarahamu) kwamba dini hazidhihirishwi kwa kila anayefariki. Ikiwa anayefariki ni mwenye niyyah nzuri, na ni mtu aliyenyooka katika ‘ibaadah, basi Allaah humuokoa katika fitnah hii. Ndio maana Maulamaa wengi wamefasiri kuhusu fitnatul-mamaat (fitnah ya kifo) ambayo tunajikinga nayo katika kila Swala kuwa ni fitnah hii (ya Shetani kumjia mtu anapofariki na kumdhihirishia dini mbili. Mtume  ametuamrisha kuwa tunapomaliza tashahhud zetu za mwisho katika Swalaah tuseme:

[اللَّهُمَّ إِنِّي أَعُوذُ بِكَ مِنْ عَذَابِ جَهَنَّمَ وَمِنْ عَذَابِ الْقَبْرِ وَمِنْ فِتْنَةِ الْمَحْيَا وَالْمَمَاتِ وَمِنْ شَرِّ فِتْنَةِ الْمَسِيحِ الدَّجَّالِ]   رواه مسلم

Allaahumma inniy a’uwdhu Bika min ‘adhaabi jahannam wa min ‘adhaabil qabri, wamin fitnatil mahyaa wal mamaati, wamin sharri fitnatil-Masiyhid-dajjaal

[Ee Mwenyezi Mungu hakika mimi najikinga Kwako na adhabu ya (moto) na adhabu za Kaburi, na fitnah ya uhai, na (fitnah) ya kifo, na shari ya fitnah ya Masiyhi-Dajjaal]  [Imepokewa na Muslim]

Ulamaa wengi wakafasiri fitnatul-mamaat kwamba ni fitnah wakati wa mtu anapofariki kwa sababu ndio fitnah kubwa kabisa katika maisha ya mtu kwa vile kuna mzunguko na kugeuka:

[إِنَّ الرَّجُلَ لَيَعْمَلُ عَمَلَ أَهْلِ الْجَنَّةِ حَتَّى مَا يَكُوْنُ بَيْنَهُ وَبَيْنَهَا ِ إِلاَّ ذِرَاعٌ، فَيَسْبِقُ عَلَيْهِ الكِتَابُ فَيَعْمَلُ بِعَمَلِ أَهْلِ النَّارِ فَيَدْخُلُهَا]    رواه البخاري ومسلم

[…Hakika mtu hufanya ‘amali ya watu wa Peponi, mpaka ikawa hapana baina yake na Pepo ila dhiraa, akatanguliwa na aliloandikiwa (majaaliwa yake) akafanya ‘amali ya watu wa Motoni, akaingia Motoni]     [Imepokewa na Bukhari na Muslim]
Imehadithiwa kwamba Imaam Ahmad (Mungu amrahamu) alipokuwa anakaribia kufariki, akisema: “Bado, bado!” Akaulizwa: “Kwanini unasema bado bado?” Akasema: “Shetani yuko mbele yangu anajitafuna vidole vyake akiniambia: “Umenikwepa sijaweza kukupoteza ee Ahmad”. Ndio nikawa namjibu: Bado bado!” Ina maana; madamu roho ya binaadamu bado ipo mwilini mwake, basi hakika anaigopa fitnah.
Bali hakika Siku ya Qiyaamah itakapofika, itakuwa kama kwamba hawakuishi isipokuwa saa moja katika mchana (wa siku moja) kama Anavyosema Mwenyezi Mungu ﷻ:

{كَأَنَّهُمْ يَوْمَ يَرَوْنَ مَا يُوعَدُونَ لَمْ يَلْبَثُوا إِلَّا سَاعَةً مِنْ نَهَارٍ}    الأحقاف:35

[Siku watakayoyaona yale waliyoahidiwa itakuwa kama kwamba hawakukaa (duniani) isipokuwa saa moja (tu) ya mchana]    [Al-Ahqaaf 46: 35]

Allah Atujaalie Mwisho Mwema na tufe na Kalimatu Tawhiid

Imeandikwa na

Ustadh Yusuf Abubakar

☎+25422671024

Eldoret Kenya

Toa maoni yako

Begin typing your search above and press return to search.