HUKMU YA KUKARIRI SURA MAALUM BAADA YA SURATUL FATIHA KATIKA RAKAA YA KWANZA NA YA PILI
Suali : Jee yafaa kusoma sura maalum baada ya Suratul fatihah kisha kusoma sura ile ile baada ya fatihah katika rakaa ya pili. Na jee yafaa kudumu kusoma sura maalum baada ya faatihah katika kila swala na katika kila rakaa, na jee swala inaswihi pamoja na kudumu na jambo hilo??
Jawabu :
Kwanza : Yafaa mwenye kuswali kusoma sura maalum baada ya Suratul Faatihah katika Rakaa ya kwanza, kisha akasoma sura ile ile katika Rakaa ya pili.
Na linaloonesha kufaa kwa jambo hilo ni Hadithi iliyopokelewa na Abu Daud (816) kutoka kwa Mtu mmoja kutoka katika kabila la Juhainah yakwamba
سَمِعَ النَّبِيَّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ : يَقْرَأُ فِي الصُّبْحِ ( إِذَا زُلْزِلَتْ الْأَرْضُ ) فِي الرَّكْعَتَيْنِ كِلْتَيْهِمَا ، فَلَا أَدْرِي أَنَسِيَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ أَمْ قَرَأَ ذَلِكَ عَمْدًا “
[Alimsikia Mtume MUHAMMAD ﷺ akisoma katika Swala ya subhi sura ya (Idha zulzilatil ardhu) katika Rakaa zote mbili sasa sijui kama Mtume ﷺ alisahau ama alisoma hivyo kwa makusudi]
Hadithi hii amesema Sheikh Albany Mungu amrehemu yakwamba ni nzuri katika kitabu cha [Swahihu Sunani Abii Daud].
Amesema Sheikh Albany Mwenyezi Mungu amrehemu katika kitabu chake “Swala” [ukurasa wa 90]
“Na udhahiri wa hadithi hii ni kwamba mtume MUHAMMAD ﷺ alifanya vile kwa makusudi ili iwe sheria” .
Na amepokea Imamu Bukhary (7375) na Imamu Muslim (813) Imepokelewa kutoka kwa Aisha radhi za ALLAH ziwe juu yake yakwamba Mtume MUHAMMAD ﷺ:
أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ بَعَثَ رَجُلًا عَلَى سَرِيَّةٍ وَكَانَ يَقْرَأُ لِأَصْحَابِهِ فِي صَلَاتِهِمْ فَيَخْتِمُ بِقُلْ هُوَ اللَّهُ أَحَدٌ …. إلخ الحديث
[Alimtuma mtu kama kiongozi wa kundi la jeshi na alikua akiwasomea watu wake katika Swala zao na alikua akimalizia na (Qul huwa llahu ahad)…. Mpaka mwisho wa hadith.
Amesema Ibnul Araby Mwenyezi Mungu amrehemu akisherehesha hadithi ya Imamu Bukhary:-
“Na likawa hili ni dalili yakwamba yafaa kukariri sura katika kila rakaa” imeisha kutoka katika kitabu cha ” [Ahkaamul Qur’an] (4/468)
Pili :Kudumu na kusoma sura maalum baada ya fatihah katika kila Rakaa, na katika kila Swala inafaa na ndio madhehabi ya Wanazuoni wengi.
Imekuja katika kitabu cha [Mausuuatul fiqhiyyah] (25/290):
“Wameenda wanazuoni wengi katika madhehebu ya Hanafi na Shafii na Hanbal yakwamba “Hakuna tatizo kwa mwenye kuswali kukariri sura katika Qur’aan aliyoisoma katika rakka ya kwanza” .
Isipokua hata kama jambo hili linafaa,na Swala inaswihi kwalo, na halibatwilishi Swala ila Jambo hili ni kinyume na Sunna, na muongozo uliopangika wa Bwana Mtume MUHAMMAD ﷺ na hivyo basi inapendeza na ni bora kwake asome Sura tofauti tofauti kwa kumuiga Bwana Mtume MUHAMMAD ﷺ.
Anasema Sheikh Ibnu Uthaymeen ALLAH amrehemu:
“Na mkabala wa jambo hili ni kwamba jambo linaweza kua linafaa lakini haliwi sheria:
Kisa cha mtu ambae mtume alimtuma kama kiongozi wa jeshi , basi alikua akiwaswalisha watu wake na katika kusoma kwake alikua akmalizia na (Qul huwa llahu ahad) , waliporudi wakamuelezea Mtume ﷺ kuhusu jambo hilo Mtume ﷺ akasema “Muulizeni kwanini alikua akifanya hivyo”? Akasema : Hakika sura hii ni sifa ya Al Rahmaan na mimi napenda kuisoma sura hii Mtume ﷺ akasema ” Mwambieni yakwamba ALLAH anampenda” kwahivyo mtume akalikiri tendo lake hili , nalo ni yeye kumalizia kisomo chake katika swala na (Qul huwa llahu ahad) Lakini Mtume ﷺ hakulifanya jambo hili kwamba ni sheria ; kwani hata yeye Mtume ﷺ alikua hamalizi kisomo chake katika swala na Qul huwa llahu ahad na wala hakuamrisha umma wake kufanya hivyo.”
Inabainika kutokana na jambo hili yakwamba kuna matendo ambayo inafaa kuyafanya lakini sio sheria ,kwa maana yakwamba mwanadamu akikifanya kitendo hicho hakemewi , na pia hawezi kuambrishwa kukifanya kitendo hicho ”
Imeisha kutoka katika kitabu cha [Majmu’u Fataawa Ibni Uthaymeen] (17/252)
Na ALLAH ndio mjuzi zaidi.
Kwa kifupi : inafaa kwa mwenye kiswalia kusoma sura maalum baada ya Faatihah katika Rakaa ya kwanza na kusoma sura ile ile katika Rakaa ya pili na hivyo hivyo kudumu na kusoma sura maalum baada ya Faatihah katika kila Rakaa , na katika swala zote lakini linalopendeza na lililo bora kwake : ni kusoma sura tofauti tofauti , kwa kumuiga bwana Mtume MUHAMMAD ﷺ.
Chanzo ni Fatwa ya Sheikh Swaleh Al Munajjid*
Na kufanya Tarjam na Ustadh Fadhil Muhammad