FADHLA ZA KUSOMA QUR’ANI TUKUFU
Ewe Muislamu ulipoumbwa na ukaletwa hapa Duniani uliwekewa katiba na mfumo wa kuishi na njia ya kupita mwanzo mpaka mwisho, nzuri na mbaya, yote hayo utayapata kwenye Qur’an ukifundishwa na Bwana Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam).
KUISOMA QUR’ANI NA ADABU ZAKE
Qur’ani Tukufu ni kitabu ambacho ndio msingi wa kufaulu kwenu, chenye kuwatoa watu kwenye giza,na kuwapeleka kwenye nuru, ndani yake kuna khabari ya waliokuja kabla yenu na watakaokuja baada yenu na hakimu kati yenu, chenye kupambanua baina ya haki na batili. Mwenye kukiacha ameumia, mwenye kutaka uongofu kwa hicho ataongoka, na mwenye kutaka kuongoza na kitabu kingine amepotea; ni kamba ya Allah ya kuaminika isiyokatika; ni utajo wa Mwenyezi Mungu ni njia iloyonyoka, mwenye kuifuata hapotei na mwenye kuifuata hachanganyikiwi. Hawashibi nayo wanavyuoni na maajabu yake hayapungui. Atakaye ukweli ataupata humo na mwenye kuhukumu nacho atahukumu kwa usawa.
Matakwa ya Allah ni tuisome Qur’ani ili atuongoze na atuingize peponi.
Ndugu Muislamu Tusomeni Qur’an na Tuwasomeshe watoto wetu ili waweze Kuinukia katika kuipenda Qur’ani,na Vile vile tuwahifadhishe watoto wetu wakiwa wadogo kwani kuhifadhi kwa udogoni ndio Wataweza kuhifadhi vizuri na kubaki ndani ya nyoyo zao. kwani kuhifadhi udogoni ni kama kuchonga kwenye jiwe.
Amesema Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala):
{إِنَّ الَّذِينَ يَتْلُونَ كِتَابَ اللَّهِ وَأَقَامُوا الصَّلَاةَ وَأَنفَقُوا مِمَّا رَزَقْنَاهُمْ سِرًّا وَعَلَانِيَةً يَرْجُونَ تِجَارَةً لَّن تَبُورَ لِيُوَفِّيَهُمْ أُجُورَهُمْ وَيَزِيدَهُم مِّن فَضْلِهِ ۚ إِنَّهُ غَفُورٌ شَكُورٌ فاطر:29-30
[Hakika wanaosoma hiki Kitabu cha Allah na wakasimamisha swala na wakatoa kwa mali yao tulizowapa kwa siri na dhahiri, wanatarajia biashara isiofilisika, na hakika Allah atawalipa awaongeze, kwani yeye mweyekusamehe saana na ni mwenye kushukuriwa ] [Faatir: 29-30]
Na mke wa Mtume ‘Aisha akazidi kutufafanulia akisema: ‘Kusoma kwa Qur’ani kunatafautiana, kuna anayesoma hodari. Hivyo, thawabu zake ni nyingi kiasi cha kutangamana na Malaika na anayesoma akigongagonga atapata malipo mara mbili. Vilevile Abi Umama akamwambia amemsikia Mtume akisema:
[اقرءوا القرآن فإنه يأتي يوم القيامة شفيعا لأصحابه] رواه مسلم
[Someni Qur’an, itakufaa siku ya Qiyama kuwaombea shufaa.] [Imepokewa na Muslim.]
Haya yote ni fadhila za Qur’an na fadhila za kusoma Qur’an.
Mtume wetu ﷺ alimuusia Abu Said akimwambia:
أُوصِيكَ بِتَقْوَى اللَّهِ ، فَإِنَّهُ رَأْسُ كُلِّ شَيْءٍ ، وَعَلَيْكَ بِالْجِهَادِ ، فَإِنَّهُ رَهْبَانِيَّةُ الْإِسْلَامِ ، وَعَلَيْكَ بِذِكْرِ اللَّهِ ، وَتِلَاوَةِ الْقُرْآنِ ، فَإِنَّهُ رَوْحُكَ فِي السَّمَاءِ ، وَذِكْرُكَ فِي الْأَرْضِ رواه أحمد
[Nakuusia umche Mwenyezi Mungu, kwani hilo ndio kichwa cha kila kitu, na utoke kwenda Jihad kwani hilo ndio daraja kuu la Uislamu na umtaje Mwenyezi Mungu Na kwa wingi, na usome Qur’an ukifanya hivyo roho yako itakuwa mahali pazuri mbinguni na utakuwa na utajo upo ardhini.] [Imepokewa na Ahmad]
ADABU ZA KUSOMA QUR’ANI
1. Kusoma kwa ajili ya Allah (Subhaanahu wa Taala)
Waja watalipwa kulingana na nia zao. Mtume anatutolea khabari kuwa watu watalipwa vibaya japokuwa tunawaona wakifanya mema, nao ni sampuli Tatu:-
Mtu anajishughulisha na Qur’an kuisoma vizuri, kuikusanya n.k
Mtu aliyeuliwa jihad fi sabilillahi.
Mtu tajiri anaye toa sana.
Kumbe wote hawa watatu, wanafanya riya, Allah atamwambia msomaji Qur’an: Si nilikufundisha Qur’ani ? Atajibu: Ndio ewe Mola; baadaye ulifanya nini? atajibu nilikua nikiisoma usiku na mchana, Mwenyezi Mungu atasema: ‘Umesema urongo, na Malaika watazidi kumkaripia ‘muongo we, na watasema Ewe Mola: huyu bwana, alikuwa akisoma kwa ajili ya watu, na tukaachia watu wamlipe kule kule duniani. Mungu atawaamrisha Malaika wamtie motoni Mwenyezi Mungu atulinde na hayo
2. Kusoma hali akiwa na utwahara
Hapana shaka kuyasoma maneno ya Allah ukiwa msafi, ndio bora kama vile kupiga mswaki, kutawadha n.k. Kwa sababu Mtume ﷺ Amesema:
[إن أفواهكم طرق للقرآن فطيبوها بالسواك] رواه إبن ماجة
[Hakika midomo yenu, ndiyo njia za kusoma Qur’an, isafisheni kwa miswaki]. [Imepokewa na Ibnu Maajah]
Mtume ﷺ akasema tena:
[إِنَّ الْعَبْدَ إِذَا قَامَ يُصَلِّي ، أَتَاهُ الْمَلَكُ فَقَامَ خَلْفَهُ يَسْتَمِعُ الْقُرْآنَ وَيَدْنُو] رواه البيهقي
[Ikiwa mja anaswali, Malaika humjia, na wakamsimamia nyuma yake wakimsikiliza Qur’ani na wanamkurubia.] [Imepokewa na Al-Bayhaqiy]
Na je ikiwa mja kinywa chake chanuka? Malaika watakaa kando.
3. Kusoma kisawasawa
Mola wetu anatuamrisha kuisoma Qur’an na Mtume wetu anatushinikiza hivyo, na maswahaba wakisoma Aya Aya, mmoja wao ni Anas bin Malik Anatuambia Mtume akiwafundisha hata kuvuta Bismillahi na kadhalika. “Abdallah bin Masuud amesema”
[لا تهذوا بالقرآن هذا الشعر] رواه إبن أبي شيبة
[Musiisome Qur’ani haraka haraka kama Mashairi] . [Imepokewa na Ibnu Abiishayba].
Albara amesema: ‘Nimemsikia Mtume akisoma Wattini Wazzaytuni kwenye Swala ya Ishaa. Sijawahi kusikia sauti nzuri kama hiyo. Mtume ﷺ amesema:
[زَيِّنُوا الْقُرْآنَ بِأَصْوَاتِكُمْ] رواه الحاكم
[Tengenezeni sauti zenu mnaposoma Qur’an]. [Imepokewa na Haakim]
Na hizo hadithi ni swahihi. Ni vizuri asome kwa sauti ya kuimbia ya kughani, imepokewa kutoka kwa Mtume ﷺ amesema:
[لَيْسَ مِنَّا مَنْ لَمْ يَتَغَنَّ بِالْقُرْآنِ] رواه البخاري
[Si katika sisi yule mtu atasoma Qur’aan na haghani]. [Imepokewa na Bukhari].
Na kughani kwenyewe ni mume kwa sauti ya kiume na mke ajikaze, sio sauti kuwavutia wengine, na asome asimame kwenye mwisho wa kila Aya kama anavyotueleza mke wa Mtume Ummu Salama.
4. Kusoma kwa Sauti ya chini
Mtume ﷺ alitufundisha, tusisome kwa sauti ya juu, mpaka tukawaudhi wengine. Kwa mfano, wengine wanaswali na majirani wamelala, soma kwa kiasi.
Mtume ﷺ anatuambia katika maana ya hadithi: “Nyote mtaitwa na mola wenu, msiudhiane wala msipandishiane sauti nyingi na kama mtu anasinzia aache kusoma alale, asije akasoma makosa makosa asijijue, na asiache sura zile fadhila zaidi kama suratul-Ikhlas, ambayo ni theluthi ya Qur’an.
Na katika riwaya kadhaa Mtume amekuwa akisema: [Suratul-Ikhlas, ni theluthul ya Qur’an.]
Na alikuwa akisoma Suratul Sajdah na Suratul Insaan katika Sala ya Alfajiri, na Tabaraka na Surat Al-Falaq na An-Nisa kabla ya kulala. Na vile vile akisoma Surat Al-Falaq na An-Nisa na Ayatul-Kursiyu baada ya kila swala].
5. Kukatazwa kusoma Qur’an katika rukuu na Sijida.
Mtume ﷺ mwenyewe ametukataza hilo kwenye hadithi swahihi akisema:
أَلا وَإِنِّي نهيت أَن أَقرَأ الْقُرْآن رَاكِعا أَو سَاجِدا ، فَأَما الرُّكُوع فَعَظمُوا فِيهِ الرب ، وَأما السُّجُود فاجتهدوا فِي الدُّعَاء ، فقمن أَن يُسْتَجَاب لكم رواه مسلم
[Jueni ya kuwa, nimekatazwa kusoma Qur’an kwenye Rukuu na sijida. Ama katika Rukuu Mtukuzeni Allah na ama katika sijda mjitah idi kwa dua huenda mukakubliwa maombi yenu ]. [Imepokewa na Muslim]
Na sababu yake ametaja Sheikhul-Islam, kukaa rukuu na sijida ni pahali pa kujidhalilisha Muislam kwa Mola wake.
KWA FAIDA ZAIDI SIKILIZA MADA HII NA SHEIKH MAHAMMAD RAJAB