MAELEZO KATIKA KUTAWADHA
1. Muislamu akiinuka kutoka usingizini na akataka kutawadha kwenye chombo, basi asichote humo kwa mikono yake mpaka aioshe mara tatu, kwa kauli yake Mtume ﷺ:
إذا استيقظ أحدكم من نومه فلا يغمس يده في وضوئه حتى يغسلها ثلاثاً، فإن أحدكم لا يدري أين باتت يده] رواه البخاري ومسلم]
[Akiamka mmoja wenu kutoka kwenye usingizi, basi na asiuvike mkono wake chomboni mpaka auoshe mara tatu, kwani hujui mkono wake ulilala wapi] [Imepokewa na Bukhari na Muslim.]
2. Inapasa mtu awe na pupa la kuyafikisha maji kwenye kila kiungo kinacholazimu kuoshwa, hasahasa kwenye sehemu za baina ya vidole vya mikono na miguu, na baina ya ndevu na mashikio, pia visukusuku, vifundo na visiginyo kwa kauli yake Mtume ﷺ:
[وَيْلٌ لِلأَعْقَابِ مِنَ النَّارِ] رواه البخاري ومسلم
[Ole wa motoni kwa visiginyo] [Imepokewa na Bukhari na Muslim.]
3. Asili ni kujengea yakini. Lau mtu alikuwa na yakini kuwa alitawadha kisha akafanya shaka kuwa udhu wake umetanguka, basi atajengea yakini yake nayo ni kuwa ana udhu. Na lau alikuwa na yakini kuwa hana udhu, kisha akafanya shaka: ametawadha au la? Basi yakini ni kuwa yeye hakuwa naudhu.
4. Muislamu anapotawadha, akaosha viungo vinavotakikana kuoshwa kwa mwenye kutawadha, mara mojamoja au mara mbilimbili, au vingine mara moja na vingine mara mbili au mara tatu, udhu wake ni sahihi.
5. Mtu akiswali bila ya udhu kwa kusahau, itamlazimu kurudia Swala anapokumbuka.
6. Mtu akitawadha kisha akaingiwa na njisi, basi ataiondoa najisi wala harudii kutawadha, kwa kuwa kuingiwa na najisi hakutangui udhu.