DKT. TIMOTHY J. WINTER
Ni mzaliwa wa Uingereza mwaka 1960. Amesoma katika shule yenye hadhi Westminster, London na baadae akaingia Chuo Kikuu cha Cambridge ambapo alihitimu kwa alama za daraja lajuu kabisa mwaka 1983. Alichukua shahada yake ya pili katika chuo hicho hicho cha Cambridge, na baadae kwenda kujiendeleza kielimu huko Chuo Kikuu cha Azhar; moja ya vyuo vikuu vya zamani zaidi duniani. Akaishi Cairo kwa miaka 3 akiusoma Uislam kutoka kwa walimu wa kawaida tu wa kimisri. Dkt. Timothy alikuwa ni msaidizi wa utafiti wa Chuo Kikuu cha Oxford. Akaenda kuishi Jeddah, Saudi Arabia kwa miaka mitatu ambapo alianzisha ofisi ishughulikayo na mambo ya kufasiri. Baada ya kusilimu, alibadili jina na kuwa Abdul-Hakim Murad. Lakini ni vitu gani basi unafikri vimempelekea mtu mwerevu kama huyu kusilimu?! Sababu zitatolewa katika aya zifuatazo.
Katika umri wake wa ukijana, Timothy alilivalia njuga swala la kujua ipi dini ya kweli. Alikuwa ametambua kuwa mapadri hawaiamini imani ya Utatu. Alikuwa anawajua baadhi ya watu ambao ni maarufu na wenye heshima zao ambao walikuwa wanaimani ya Mungu mmoja pia. Timothy alikuwa ni mtu mwenye furaha kwa kuwa Mkristo anayeamini Mungu mmoja pia, akihusianisha akili na imani yake na mshairi maarufu wa kiengereza, John Locke, Isaack Newton, Charles Dickens na wengine wengi. Kusoma kwake vizuri kwa Agano La Kale la Biblia kulimfanya afanye maamuzi ya kujikita katika imani ya Mungu mmoja na kuikacha ile ya utatu. Na bila shaka maneno “Sikiza, Ee Israeli; Bwana, Mungu wetu, Bwana ndiye mmoja.” [Kumbukumbu la Torati 6:4] yanaonekana kueleweka kabisa hata yakichorwa katika mwamba au yakiandikwa katika karatasi. Ule ukuaji wa imani ya Mungu mmoja (na uislam ukiwepo) kwa wasomi wengi wa dini huko Ulaya kukawa ni sababu nyengine ya yeye kubadilika hivi. Katika kipindi kilichorushwa na kituo cha ABC, John Cleary alikuwa akizihoji sababu za Timothy kuwa Muislamu. “Kipi kilichokupelekea mpaka ukatoka katika Ukristo? Lipi jipya unalolipata katika uislam?” Cleary aliuliza. “Uwezo wangu wa imani” Winter alijibu, akaendelea “Haujaniruhusu kuamini akida au mafundisho ya kidini (doctrines) zisoweza kushikika au kueleweka (abstract). Mimi hata katika huu umri wangu bado niko na ule ‘kutaka-kujua’ ya mtoto mdogo [ambaye hupenda kuuliza maswali na haridhiki mpaka apate majibu halisi]. Sikuweza kuchukua mruko wa kiimani (kuamini kiupofu bila ya hoja za maana) na kukubali imani hizi za Kikristo kama ile ya Utatu (Trinity) na ati Yesu alikufa kwa dhambi zetu (Atonement).”
Ile hamasa ya kutaka kuijua fasihi ya dini ilikuwa ni sababu nyengine kwa Timothy kuipata nuru ya Uislamu. Kwa kusoma vitabu, Timothy aligundua makosa ya Biblia ambayo wafuasi wa kawaida wa kanisa bado hawajajuzwa. Vitabu alivyopitia ni pamoja na The Myth of God Incarnate (Uwongo wa Mungu Kuvaa Umbo la Binaadamu) na Life of Muhammed (Maisha ya Muhammad) cha Maxime Rodinson. Timothy anakubali kuwa aliathirika sana na visa vya Mtume alivyovikuta katika kitabu cha Rodinson. Kanuni yake ya kupingapinga ilimfanya aonekane kama mtu mgeni na wa kushangaza lakini mwenyewe anafurahi kwamba haijaweza kupigwa na mawimbi ya mithiolojia (kanuni na mafundisho ya kubuniwa tu na wala yasio na ukweli) zinazopatikana katika dini ya Kikristo. Mathalan, hakuweza kuimeza kabisa ile imani ya kusamehewa dhambi, akiita imani hii ya dini ni ya usaliti (blackmail) pale aliposhangazwa na Mungu asiyeweza kusamehe watu moja kwa moja mpaka ajitie katika umbo la binaadamu wamdhalilishe, wamtese, wamuabishe, na wamuadabishe eti ili ndio awasamehe. Vitabu vingine vilivyoacha athari kwake ni vile vya mtunzi mashuhuri wa kiengereza Ruqaiyyah Maqsood. Katika kitabu chake The Mysteries of Jesus: a Muslim study of the origins and doctrines of the Christian church. (Miujiza ya Yesu: Tafiti ya Kiislamu Katika Uhalisia na Imani ya Kanisa la Kikristo). Katika kitabu hiko, Maqsood alimuweka wazi Mungu mwengine kabisa, mwenye upendo mwenye huruma kwa kusema: “Mungu haitaji kafara ili aweze kusamehe watu. Kitendo cha kubadilika haraka kutoka katika Ukristo kuingia katika Uislam ni uthibitisho tosha wa ukweli kama ule wa Mwana Mpotevu (the Prodigal Son).”
Jambo jengine zito lililomvuta Timothy kuingia katika Uislam ni kuisoma Qur’an. Mazoezi ya kulinganisha na kutofautisha, Qur’an na Biblia yalimfanya Timothy kukiri haya: “Sehemu nyingi za Biblia zimejazwa na hadithi (visa) ambazo malengo yake bado ni tata au hata hamna kwa wakati mwengine; zilizomulikwa kwa mwanga wa kumwekuamwekua tu lakini Qur’an ilinipa mwanga kamili.” Katika mahojiano kwenye Sunday Nights na John Cleary katika kulijadili lililomuathiri katika uislam Timothy akaelezea athari ya Qur’an:
“Hata uislam una sauti zake nzuri pia, na ufunguo wa tuni za kiislamu si lengine bali ni huu usomaji mzuri wa Qur’an. Nilikuwa natembea mitaani asubuhi na mapema kipindi naishi Cairo. Nilishuhudia wenye maduka wakifungua maduka yao, na nilihesabu wauzaji maduka wapatao 38 ambao walikuwa wakisikiliza Qur’an masaa 24 kwa siku. Kwa hakika hiyo ndio sauti niipendayo zaidi, na ilikuwa moja ya sumaku zilizonivuta mimi kuuelekea uislam. Ni sanaa kubwa ya kiislamu, ambayo bado inanitetemesha kuliko sauti yoyote duniani.”
Sanjari na hilo, Timothy alivutiwa na kile alichokiita ‘msimamo wa ajabu wa uislam’. Hivyo ni sawa na kusema sheria na matendo ya ibada ya Kiislamu yanastaajabisha kwa kutobadilika kwake. Kuhusu hilo alisema:
“Msikitini, mtu hashikwi na tamaa wa kusema maneno yasiyo na maana, au ayatakayo, bali ni yale tuliyorithi kutoka zama za zamani za imani, maneno ambayo mtu atajishusha nayo pale anapohitaji kuongea na Mungu. Hakuna dini nyengine inayofanya kama mwanzilishi wao [yaani Mtume Muhammad] alivyofanya; na hakuna dini nyengine ambayo maneno yake ya ibada yako sawa dunia nzima na zama zote.”
Katika upande mwengine, amgundua katika ukristo, kuna sheria ambazo zimetungwa upya na watu wasio stahili jukumu hilo, wakisababisha mgawanyiko na chuki na aghalabu wakiaacha mkusanyiko ukiwa hautendi ipasavyo wanalotaka kufanya.” Upya huo wa sheria na ibada ndio unaoharibu ukweli wa dini. Ukiachana na yote, kubwa kabisa lililosababisha yeye kuwa Muislamu ni maombi yake kwa Mola mmoja na pekee. Timothy aliamini kuwa Mungu alikuwa akijibu dua zake.
Katika mahojiano naye, John Cleary aliuliza swali lamsingi sana kuhusu maisha ya Timothy katika Uislamu: “Ni kipi kwako kinachokuashiria mwanga sahihi wa Uislamu, kile kinachoangaza njia ambayo maisha yako yanapaswa kuyafata?” Na jibu lilifupisha ule uzuri wa Uislamu kama alivyosema mwenyewe Timothy Winter:
“Mwenyezi Mungu mmoja,na ukweli ni mmoja, usiochanganywa, usiofanywa mgumu na usiobadilika…mtiririko mzuri wa njia za kuabudu ambao mtu anatumia kuufikia ukweli huo muhimu. Moja ya utajiri wa Uislamu kwangu mie ni hizi liturujia na vitendo za ibada na hata pia vile watu wanafunga Saum na kutoa Zakkah; yote haya yako sawa ulimwenguni kote na hayajabadilishwa hata kidogo. Hakuna waliyotokea wakasema njooni tubadilishe kidogo mfumo wa swala zetu. Labda tulete magitaa na imamu wa kisasa avalie mabuti na jinzi akijaribu kuimba hapo mbele. Naenda msikitini na najua kitu nachoenda kupata kikiwa hakibadiliki, kizuri, kikiwa kishakamilika tangu zama hizo. Jambo kubwa sana kwangu kuona ibada zetu hazibadiliki na bila shaka hazitabadilka. Na la tatu ni huku kufata mila ya Ibrahim. Silihisi jambo hili eti kwa kuwa mimi ni Muingereza au labda ni mtu fulani, najua ni tofauti lakini moyoni nahisi ni sehemu kutoka katika maandiko ya Kiyahudi na Kikristo, jamii za kiimani za Mashariki ya Kati pia. Bado nampenda Yesu, Ibrahim, Musa, Yaqub, Ismail na Is’haq kwani wote wameheshimiwa katika Qur’an, walikuwa watu wakubwa utotoni mwangu na bado nawaheshimu hadi leo. Hivyo sihisi kuwatenga hata kidogo.”
Kwa sasa ni mhadhiri wa chuo kikuu akifundisha masomo ya dini ya kiislamu katika kitivo cha masuala ya dini, Chuo Kikuu cha Cambridge, Uingereza. Na pia ni mkurugenzi wa masomo ya Teolojia katika Chuo cha Wolfson. Pamoja na kuwa imam wa msikiti wa Cambridge, Sheikh Murad pia ni katibu wa mfuko wa Waislamu; Muslim Academic Trust (London) na pia ni mkurugenzi wa Sunnah Project katika kituo cha masomo yahusuyo mashariki ya kati hapo Chuo Kikuu cha Cambridge, ambacho kinatoa matoleo ya mwanzo kabisa ya mkusanyiko wa Hadithi kwa Kiarabu.
Winter amekuwa akitokea katika idhaa ya BBC na amekuwa mwandishi mkubwa katika magazeti mbalimbali kama The Independent; Q-News International, jarida la Waislamu la Waingereza (Britain’s premier Muslim Magazine); na Seasons jarida la kitaaluma la Taasisi ya Zaytuna. Timothy alinukuliwa akisema:
“…Pamoja na asili yake ya karne ya 7 ya Uarabuni, Uislamu unakubalika mazingira yote, na hii ni dalili ya asili njema na ya kimaajabu ya dini hii…tukiuzoea Uislamu na kutulia nao vizuri, utaona ndio imani pekee inayostahili watu wa Uingereza. Mila zake ndio bora kwetu. Mtindo wake wa huruma ya wastani, maji yaliyotulia yana kina kirefu; msisitizo wake katika staha na msisitizo wake katika maarifa ya kawaida na katika nadharia ya vitendo, na usisitizo wake wa kutumia akili, vinaungana kutupatia dini bora na asili zaidi kwa ajili ya watu wetu…Uislamu ndio dini yenye udugu wa kweli wa waumini katika Mungu mmoja wa kweli, muunganiko wa kweli kwa wale wanaopenda kubaki na malengo mazuri ya kufata ubinaadamu katika hizi zama za kijinga na kusikistisha. Uislamu ni mkarimu na unajumuisha wote.” **
** Hii ilikuwa ni Dondoo (excerpt) ya kitabu cha Salim Boss kiitwacho“Wao Ima ni Waerevu Mno au Wajinga Mno” chenye kurasa 672 zote zimechapishwa kwa rangi (full colour). Ni tarjama ya kitabu kilichouzika sana kiitwacho “They are Either Extremely Smart or Extremely Ignorant” Kwa usomaji wa ziada tembelea www.extremelysmart.org au www.facebook.com/muerevumno “**