0%

https://uongofu.com/wp-content/uploads/2021/06/services-head-1.png

DALILI ZA MWENYEZI MUNGU KATIKA VIUMBE VYAKE

DALILI ZA MWENYEZI MUNGU KATIKA VIUMBE VYAKE

Mwenyezi Mungu Ametuamrisha tuamini kwamba yeye yuko. Na Aya zinazozungumzia suala hili ni nyingi sana pia ameumba viumbe vinavyoonesha kwamba yeye yupo.Kwani kupatikana kwa viumbe ni kuonesha kuna alie umba
Hakika katika kila kitu alivyoviumba Mwenyezi Mungu Subhaanahu wa Taala ni dalili ya kuonesha kwamba yeye ni mmoja, na ndiye anayestahiki kuabudiwa kwa haki kabisa na haifai kushirikishwa na yoyote wala chochote.
Napenda nizitaje baadhi ya Aya ambazo zimetuamrisha kuzingatia katika ulimwengu.Amesema Allah Subhaanahu wa Taala:

{أَوَلَمْ يَنظُرُوا فِي مَلَكُوتِ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَمَا خَلَقَ اللَّهُ مِن شَيْءٍ وَأَنْ عَسَىٰ أَن يَكُونَ قَدِ اقْتَرَبَ أَجَلُهُمْ ۖ فَبِأَيِّ حَدِيثٍ بَعْدَهُ يُؤْمِنُونَ}

[Je hawaangalii ufalme katika mbingu na ardhi na alivyoumba Mwenyezi Mungu katika vitu, na huenda ikiwa umekaribia muda wao wa kuondoka duniani kumalizika. Basi ni maneno gani baada ya Qur’an watayamini ]  [Al-Araaf : 185].
Na Amesema tena Mwenyezi Mungu ﷻ:

أَفَلَمْ يَنظُرُوا إِلَى السَّمَاءِ فَوْقَهُمْ كَيْفَ بَنَيْنَاهَا وَزَيَّنَّاهَا وَمَا لَهَا مِن فُرُوجٍ  وَالْأَرْضَ مَدَدْنَاهَا وَأَلْقَيْنَا فِيهَا رَوَاسِيَ وَأَنبَتْنَا فِيهَا مِن كُلِّ زَوْجٍ بَهِيجٍ  تَبْصِرَةً وَذِكْرَىٰ لِكُلِّ عَبْدٍ مُّنِيبٍ       ق:6-8

[Je hawaangalii mbingu juu yao vipi tuliijenga na kuipamba na kuifanya kuwa haina nyufa. Na ardhi vipi tuliitandaza na kuiweka vigingi(isitikisike)na tukaotesha katika ardhi hiyo kila mimea mizuri hali ya kuwa ni kifumbua macho kwa kila mtu muelekevu]   [Qaaf : 6 – 8].

Amesema tena Mwenyezi Mungu Subhaanahu wa Taala:

أَفَلَا يَنظُرُونَ إِلَى الْإِبِلِ كَيْفَ خُلِقَتْ وَإِلَى السَّمَاءِ كَيْفَ رُفِعَتْ وَإِلَى الْجِبَالِ كَيْفَ نُصِبَتْ وَإِلَى الْأَرْضِ كَيْفَ سُطِحَتْ } الغاشية:17-20}

[Je hamwangalii Ngamia vipi ameumbwa, na mbingu vipi zimeinuliwa, na milima vipi imekitwa na ardhi vipi imetandikwa ]    [Al-Qaashiyah: 17- 20].

Hizi ni alama ambazo Mola anataka tuzingatie kuumbwa kwake.
Napenda sasa kutaja baadhi ya viumbe vingine vya Mwenyezi Mungu(Subhaanahu wa Taala). Navyo ni vinavyopatikana katika ardhi kama vile; Maji, Madini, Majabali, Mimea aina tofauti tofauti, kwani Mwenyezi Mungu ameidhalilisha ardhi hii kwa manufaa ya wanadamu na wanyama, wanadamu wanailima kwenye ardhi na kupanda mimea ili kujipatia chakula chao, wanatoa maji katika ardhi kwa matumizi yao na pia kuwanywesha wanyama wao. Mwenyezi Mungu amesema:

{وَفِي الْأَرْضِ آيَاتٌ لِّلْمُوقِنِينَ}  {الذاريات:20}

[Na katika ardhi kuna alama nyingi kwa wenye yakini ]   [Al-dhariyaat: 20.]

Tukiangalia mbinguni kuna nyota nyingi, jua, mwezi na sayari nyinginezo. Vilevile mbinguni kuna viumbe vya Mwenyezi Mungu ambao ni Malaika wanaotekeleza kazi alizowapa Mola aliyetukuka.
Na katika alama nyingine za kumjua Mwenyezi Mungu ni usiku na mchana. Mchana ni wakutafuta maisha na riziki na usiku ni kupumzika.Amesema Allah Subhaanahu wa Taala:

{وَجَعَلْنَا اللَّيْلَ لِبَاسًا  وَجَعَلْنَا النَّهَارَ مَعَاشًا}   النبأ:10-11

[Na tumeufanya usiku ni nguo na tukaufanya mchana ni wa kutafuta maisha ]  [Al-Nnaba 10-11].

Na katika alama hizi mbili za usiku na mchana amewafanyia watu mchana kwenda katika ardhi ya Allah na kutafuta fadhila zake na katika kutafuta fadhila hizo atazidi kubainikiwa mwanaadamu na kuzifahamu alama nyingine za Mwenyezi Mungu. Na katika usiku ni wakati wa kujipumzisha baada ya uchovu wa mchana katika hali ya kutafuta riziki na kutafuta maisha.
Tukigusia zaidi alama za Allah ni wanyama wengi wakubwa kwa wadogo na katika wadogo kuna wadogo zaidi, kuna wengine ametufanyia kuwatumia katika kazi zetu za kila siku, kama kubeba mizigo na kutupeleka sehemu nyingine Na dalili ya alama za Mwenyezi Mungu ni kuumbwa kwetu kwani kuna mazingatio makubwa sana. Mwemuezi Mungu Subhanahu wata’ala Amesema:

{وَفِي أَنفُسِكُمْ ۚ أَفَلَا تُبْصِرُونَ}   الذريات:21

[Na je katika nafsi zenu basi hamuoni ]   [Al-Dhariyaat: 21]

Aya hii inatueleza kuwa katika maumbile yetu wanadamu kuna mazingatio makubwa kumjua Mwenyezi Mungu. Lengo kuu la kumtambua ni kuzingatia katika viumbe vyako ni kumjua yeye ili kumthamini, kwani tukimthamini tutamuabudu haki ya kumuabudu na hilo ndio lengo kuu la kuumbwa majini na binadamu.Mwenyezi Mungu Subhanahu wa Ta’aala Asema:

{وَمَا خَلَقْتُ الْجِنَّ وَالْإِنسَ إِلَّا لِيَعْبُدُونِ}   الذريات:56

[Na sikuumba na majini na binaadamu isipokuwa waniabudu].   [Al-Dhariyaat 56]

Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala) ndiye aliyeumba ulimwengu wote na viumbe vyote bila usaidizi wa mtu yoyote na yeye ndiye anayeupeleka ulimwengu huu. Kwa hivyo, Yeye ndiye anayestahiki ibada kwa sababu hakuna yoyote aliyemsaidia katika uumbaji. Ametukuka Mwenyezi Mungu Mbora wa kuumba na anaupeleka ulimwengu aliomba anavyotaka na wala haulizwi kwa analofanya bali viumbe ndio watakaoulizwa katika vitendo vyao.
Ndugu katika imani! Jueni ya kwamba viumbe vyote ambavyo vinapatikana ulimwenguni havijileti vyenyewe bali Mwenyezi Mungu aliyetukuka ndiye aliyeviumba viumbe hivyo. Mwenyezi Mungu(Subhaanahu wa Taala)Amesema kwenye Kitabu Chake Kitukufu:

{أَمْ خُلِقُوا مِنْ غَيْرِ شَيْءٍ أَمْ هُمُ الْخَالِقُونَ  أَمْ خَلَقُوا السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ ۚ بَل لَّا يُوقِنُونَ}   الطور:35-36

[Au mumeumbwa kwa kisichokuwa kitu au nyinyi ndio waumbaji. Au nyinyi ndio mlioumba mbingu na ardhi bali wao hawana yakini]   [Al-Ttuur:35-36]

Kulingana na Aya hizi zinaonesha kwamba ulimwengu haukujiumba wenyewe na haukuwa kiumbe ambacho hakikumbwa wenyewe na kitu bali lazima tena kuna aliyeumba ulimwengu huu na akasimama kwa jambo lake(huo ulimwengu)naye si mwingine isipokuwa Mwenyezi Mungu ﷻ hakuna Muumba asiyekuwa Yeye wala Mola asiyekuwa Yeye.
Lau mtaambiwa kuna jumba kubwa la ghorofa lililokamilika, halina kasoro yoyote, ya kwamba limejijenga lenyewe mtaamini? Bila shaka hili ni jambo lisilowezekana kabisa.
Kwa hivyo, huu ulimwengu ulio mpana uliokwenda juu na chini. Haiwezekani kabisa kujileta wenyewe na haiwezekani kabisa kujitokeza ghafla bali ni lazima kuna aliyeuleta ulimwengu huu ambaye ni Mjuzi Muweza naye ni Mwenyezi Mungu ﷻ.
Tujue ya kwamba hatuna budi kumshukuru Mwenyezi Mungu ﷻ katika kutudhalilishia ardhi na vilivyomo humo. Kwa hivyo, ni lazima kwa kila Muislamu kushukuru neema kubwa za Mwenyezi Mungu Alizotuneemesha Allah Mola wa viumbe vyote.

KUUBWA BINGU NA ARDHI

Mwenyezi Mungu Aliyetuelimisha vipi alianza kuumba huu ulimwenguni, na ilimu hii huwezi kuipata mpaka kupitia Mtume rehma na amani zimfikie. Na yoyote atakayetaja chochote kuhusu jinsi ya kuumbwa mbingu na ardhi, hakika ni wajibu tulinganishe na mafunzo walio kuja nayo Mitume ikiafikiana na vile walivyotufundisha Mitume, basi itakubaliwa, na ikienda kinyume na maelezo ya Mitume haikubaliwi na ikiwa Mitume hawakubainisha basi sisi itabidi tulinyamazie suala hilo wala haifai kabisa kutia ufundi wetu mpaka itubainikie kuwa ni haki au ni batili.

SIKILIZA MADA HII NA SHEIKH SWADIQ ALI


Toa maoni yako

Begin typing your search above and press return to search.