SOMO LA FIQHI
Kuoga janaba kuna namna mbili
1) Josho la Kutosheleza nalo ni lazima kupatikane Mambo mawili
A) Kutia Nia ya kuondosha Janaba.
B) Kueneza Maji mwili Mzima.
2) Josho la Ukamilifu
Nao ni kuoga kama alivyo oga bwana Mtume ﷺ kama ilivyoelezwa na Maimunah, Mama wa Waumini aliposema:
وَضَعْتُ لِرَسُولِ اللَّهِ – صلى الله عليه وسلم – وَضُوءَ الْجَنَابَةِ , فَأَكْفَأَ بِيَمِينِهِ عَلَى يَسَارِهِ مَرَّتَيْنِ – أَوْ ثَلاثاً – ثُمَّ غَسَلَ فَرْجَهُ , ثُمَّ ضَرَبَ يَدَهُ بِالأَرْضِ , أَوْ الْحَائِطِ , مَرَّتَيْنِ – أَوْ ثَلاثاً – ثُمَّ تَمَضْمَضَ وَاسْتَنْشَقَ , وَغَسَلَ وَجْهَهُ وَذِرَاعَيْهِ , ثُمَّ أَفَاضَ عَلَى رَأْسِهِ الْمَاءَ, ثُمَّ غَسَلَ جَسَدَهُ , ثُمَّ تَنَحَّى , فَغَسَلَ رِجْلَيْهِ , فَأَتَيْتُهُ بِخِرْقَةٍ فَلَمْ يُرِدْهَا, فَجَعَلَ يَنْفُضُ الْمَاءَ بِيَدِ
[Nilimuekea Mtume ﷺ chombo cha maji ya kujitwahirishia Janaba, akajimiminia maji kwenye kitanga cha mkono wa kushoto akitumia kitanga cha mkono wake wa kulia mara mbili au tatu, kisha akaosha tupu yake, kisha akapiga mkono wake kwenye ardhi au ukuta mara mbili au tatu, kisha akasukutua na akapaliza puani, akaosha uso wake na mikono yake, kisha akajimiminia maji kichwani mwake, kisha akaosha mwili wake, kisha akajiweka kando akaosha miguu yake] [Imepokewa na Bukhari].
Asema Maimunah: (Nikamletea kitambaa, hakukitaka, akawa ajifukuta kwa mkono wake).
Hivyo basi namna ya kuoga ni:
1. Aoshe vitanga vyake vya mikono, mara mbili au tatu.
2. Aoshe tupu yake.
3. Apige mkono wake kwenye ardhi au ukutani, mara mbili au tatu.
4. Atawadhe kama vile anavyotawadha kuswali, bila ya kupukusa kichwa chake na kuosha miguu yake.
5. Ajimiminie maji kichwani.
6. Aoshe mwili wake wote.
7. Ajiweke kando na aoshe miguu yake.