KUAMINI MAJINA YA MWENYEZI MUNGU ALIE TUKUKA
Ni lazima kwa kila Muislamu aamini kuweko kwa Mwenyezi Mungu na kuamini kuwa Mwenyezi Mungu Ndie Aliyeumba kila kitu na yeye ndiye Anayeupeleka ulimwengu na anafanya atakalo. Pia ni wajibu kwa Muislamu kuamini kwamba Mwenyezi Mungu Ndiye anayestahiki kuabudiwa peke Yake kama ambavyo inatakiwa kwa Muislamu kuamini kwamba Mwenyezi Mungu hafanani na yoyote katika majina Yake na sifa Zake. Muislamu akiamini haya tuliyoyataja basi imani yake kwa Mwenyezi Mungu itakuwa imekamilika.
Hakika ni katika kumuamini Mwenyezi Mungu kuamini majina Yake mazuri na sifa zake tukufu bila ya kufananisha wala kuzipuuza, Mwenyezi mungu anasema:
{وَلِلَّهِ الْأَسْمَاءُ الْحُسْنَىٰ فَادْعُوهُ بِهَا} الأعراف:180
[Mwenyezi Mungu Ana majina mazuri, muombeni kwa majina hayo] [Al-Araaf : 180].
Katika maneno haya tunapata faida kwamba haifai kwa yoyote kubadilisha jina lolote au sifa yoyote ya Mwenyezi Mungu kwa sababu yoyote ile na pia haifai kufananisha jina au sifa ya Mwenyezi Mungu na jina au sifa ya mtu yoyote. Kwani kufanya hivyo ni kumfanya sawa Mwenyezi Mungu na kiumbe wake, Vilevile haifai kabisa kusema kwamba jina ambalo Mwenyezi Mungu Amelithibitisha au Mtume wake ﷺ jina hilo au sifa hiyo. Ni vyema kwa Muislamu ayajue majina ya Mwenyezi Mungu na amuombe kwa majina hayo.
Misingi Muhimu ya Majina na Sifa za Mwenyezi Mungu ﷻ.
Majina ya Mwenyezi Mungu yote ni mazuri tena yamefikia kilele katika uzuri kwa kule kukusanya kwake sifa zilizokamilika zisizo na upungufu ndani yake kwa namna yoyote.
Majina ya Mwenyezi Mungu ni yale aliyojiita kwa majina hayo au aliyomwita yeye Mtume ﷺ na haifai kwa mtu yoyote kutunga jina na kumpa Mwenyezi Mungu Mtukufu. Inavyotakiwa ni mtu kumwita Mwenyezi Mungu majina aliyojiita Mwenyewe katika kitabu chake na yale ambayo Mtume ﷺ katika hadithi zake tukufu, wala hafai mtu kuzungumza jambo bila ya ujuzi.Amesema Mwenyezi mungu Mtukufu:
{وَلَا تَقْفُ مَا لَيْسَ لَكَ بِهِ عِلْمٌ ۚ إِنَّ السَّمْعَ وَالْبَصَرَ وَالْفُؤَادَ كُلُّ أُولَٰئِكَ كَانَ عَنْهُ مَسْئُولًا} الإسراء:36
[Wala usizungumze jambo ambalo huna ujuzi nalo, hakika masikio na macho na moyo kutaulizwa kuhusiana navyo] [Al-Isra : 36].
IDADI YA MAJINA YA MWENYEZI MUNGU MTUKUFU.
Majina ya Mwenyezi Mungu hayana idadi maalumu. Muislamu atakiwa alijue hili vizuri kabisa, na hii ni kwa mujibu wa hadithi ya Mtume ﷺ aliposema:
[أسألك بكل اسم هو لك سميت به نفسك أو أنزلته في كتابك ، أو علمته أحداً من خلقك أو استأثرت به في علم الغيب عندك] رواه أحمد
[Ewe Mwenyezi Mungu na kuomba kwa kila jina ambalo liko kwenye kitabu chako, au ulilomfundisha yoyote katika viumbe vyako, au ulilolificha katika elimu isiyojulikana na yoyote kwako]. [Imepokewa na Ahmad].
Katika majina ambayo Mwenyezi Mungu hakuyataja wala hakuyafundisha viumbe nakuonesha kwamba majina yake hayana idadi maalumu.
Baada ya kutaja misingi muhimu ambayo yatakiwa kwa Muislamu aifahamu vizuri ili imani yake kwa Mwenyezi Mungu hususan katika majina yake na sifa zake iwe imekamilika vyema.
MAANA YA MAJINA YA MWENYEZI MUNGU MTUKUFU.
Ufafanuzi wa baadhi ya majina ya Mwenyezi Mungu. katika majina hayo ni:-
[ALLAH] ni muabudiwa wa haki kwa mapenzi yote katika ibada hali ya kumtukuza.
Anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
{هُوَ اللَّهُ الَّذِي لَا إِلَٰهَ إِلَّا هُوَ} الحشر:23
[Yeye ndiye Mwenyezi Mungu ambaye hapana mungu isipo kuwa Yeye tu.] [Al Hashri:23]
[MWINGI WA REHMA MWENYE KUREHEMU] ni Ambaye anawahurumia zaidi waja wake kuliko mzazi kumhurumia mwanawe, kwani neema yoyote inayopatikana ni kwa huruma ya Mwenyezi Mungu na hakuna dhara lolote lililomuepuka mwanadamu, pia ni kwa rehma ya Mwenyezi Mungu,Allah anasema:
{وَمَا بِكُم مِّن نِّعْمَةٍ فَمِنَ اللَّهِ} النحل:53
[Na hakuna neema yoyote isipokuwa yatoka kwa Mwenyezi Mungu] [An-Nahal : 53].
[MFALME] Mwenye kumiliki ulimwengu wote juu yake na chini yake kiasi kwamba hakitikisiki chochote isipokuwa Anajua bali yeye Ndiye Aliyetaka kitikisike.
Mwenyezi mungu Mtukufu Anasema:
{مَالِكِ يَوْمِ الدِّينِ} الفاتحة:4
[Mfalme siku ya malipo] [Al-Faatiha : 3].
[MTAKATIFU] ni aliyetakasika na upungufu waliyonao viumbe vyake, kwani Mwenyezi Mungu hapatwi na uchovu wala maafa yoyote kinyume na mwanadamu hupatwa na machovu na pia maafa.Mwenyezi Mungu anasema:
{وَلَقَدْ خَلَقْنَا السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ وَمَا بَيْنَهُمَا فِي سِتَّةِ أَيَّامٍ وَمَا مَسَّنَا مِن لُّغُوبٍ} ق:38
[Na hakika si lingine tumeziumba mbingu na ardhi zilizo kati yake na hatukupatwa na uchovu] [Qaaf:38].
[MWENYE NGUVU MTENDESHA NGUVU] hakuna kiumbe chochote isipokuwa kiko chini ya uwezo Wake pia kinamyenyekea Yeye.Mwenyezi mungu (Subhaanahu wa Taala) Anasema:
{مَا قَدَرُوا اللَّهَ حَقَّ قَدْرِهِ إِنَّ اللَّهَ لَقَوِيٌّ عَزِيزٌ} الحج:74
[Hawakumuadhimisha Mwenyezi Mungu anavyo stahiki kuadhimishwa. Hakika Mwenyezi Mungu bila ya shaka ni Mwenye kushinda.] [ Al-Hajj : 74].
[MJUZI] ni Ambaye yuwajua siri na kilichodhihiri na anajua kilicho bara na baharini na anajua kila kitu Ametakasika Mwenyezi Mungu.
وَيَعْلَمُ مَا فِي الْبَرِّ وَالْبَحْرِ ۚ وَمَا تَسْقُطُ مِن وَرَقَةٍ إِلَّا يَعْلَمُهَا وَلَا حَبَّةٍ فِي ظُلُمَاتِ الْأَرْضِ وَلَا رَطْبٍ وَلَا يَابِسٍ إِلَّا فِي كِتَابٍ مُّبِينٍ} الأنعام:59
[Na Yeye anajua kilioko nchi kavu na baharini. Na halidondoki jani ila analijua. Wala punje katika giza la ardhi, wala kinyevu, wala kikavu ila kimo katika Kitabu kinacho bainisha.] [Al An’aam:59]
[MTUKUFU ALIYE JUU] Aliye juu kwa dhati Yake juu ya Arshi na pia ni Mtukufu kwa sifa zake.
Anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
{سَبِّحِ اسْمَ رَبِّكَ الْأَعْلَى} الأعلى:1
[Litakase jina la Mola wako Mlezi aliye juu kabisa,] [Al A’alaa:1]
[ANAFANYA ATAKALO] Mwenye uwezo wa hali ya juu wa kufanya lolote analolitaka.
Mwenyezi Mungu anasema:
{فَعَّالٌ لِّمَا يُرِيدُ} البروج:16
[Atendaye ayatakayo.] [Al Buruuj:16]
Na amesema tena:
{لَا يُسْأَلُ عَمَّا يَفْعَلُ وَهُمْ يُسْأَلُونَ} الأنبياء:23
[Yeye hahojiwi kwa ayatendayo, na wao ndio wanao hojiwa kwa wayatendayo.] [Al Anbiyaa:23]
[MWENYE KUSAMEHE] Anayesamehe makosa yote aliyotendewa na anayesitiri aibu hata zikiwa nyingi kiasi gani.Mwenyezi Mungu anasema:
{رَبُّ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَمَا بَيْنَهُمَا الْعَزِيزُ الْغَفَّارُ} ص:66
[Mola Mlezi wa mbingu na ardhi na viliomo baina yake, Mwenye nguvu, Mwenye kusamehe] [Swaad:66]
Na amesema Mola katika Hadithi Qudsiy:
[يا ابن آدم ، إنك ما دعوتني ورجوتني غفرت لك ما كان منك ولا أبالي] رواه الترمذي
[Ewe mwanadamu, hakika yako wewe utakaponiomba na ukatarajia basi nitakusamehe dhambi zote wala sijali]. [Imepokewa na Al Ttirmidhiy]
[MWENYE HEKIMA] Anayeweka vitu pahali pake na anayekadiria vitu vizuri.
Asema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
{الر ۚ كِتَابٌ أُحْكِمَتْ آيَاتُهُ ثُمَّ فُصِّلَتْ مِن لَّدُنْ حَكِيمٍ خَبِيرٍ} هود:1
[Alif Lam Ra. Hiki ni Kitabu ambacho Aya zake zimewekwa wazi, kisha zikapambanuliwa, kilicho toka kwa Mwenye Hikima na Mwenye Khabari,] [Huud:1]
[MWENYE KUJITOSHELEZA] Anayejitosheleza mwenyewe asiyehitajia yoyote katika viumbe.
Asema Mwenyezi Mungu mtukufu:
{قُلْ هُوَ اللَّهُ أَحَدٌ اللَّهُ الصَّمَدُ} الإخلاص:1-2
[Sema: Yeye Mwenyezi Mungu ni wa pekee.Mwenyezi Mungu Mkusudiwa.] [Al Ikhlaas:1-2]
Haya ni baadhi ya Tafsiri ya Majina ya Mwenyezi Mungu Mtukufu.
Ewe ndugu Muislamu ! yamekuja mahimizo makubwa juu ya kuomba dua kwa majina ya Mwenyezi Mungu.Mwenyezi Mungu Mtukufu Anasema:
{وَلِلَّهِ الْأَسْمَاءُ الْحُسْنَى فَادْعُوهُ بِهَا} الأعراف:180
[Mwenyezi Mungu Ana majina mazuri, muombeni kwa majina hayo] [Al-Araaf : 180].
Na Mtume ﷺ amebainisha namna gani tutamuomba Mwenyezi Mungu kupitia majina yake matukufu. Katika hadithi Mtume ﷺ alimsikia mtu katika maswahaba akisema:[Ewe Mwenyezi Mungu, Nakuomba wewe kwani sifa na shukrani zote ni zako, hakuna mola apasaye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Wewe peke yako. Huna mshirika, Mwenye kusimulia unalofanya, Muumba wa mbingu na ardhi, Mwenye utukufu, na ukarimu, Ewe ulio hai Mwenye kusimamia kila kitu. Mtume ﷺ akasema: “ Hakika umemuomba Mwenyezi Mungu aliyetukuka kwa jina lake tukufu ambalo akiombwa kwa jina hilo hujibu na Akiombwa hutoa].
Kwa hivyo, ni juu yako mja wa Mwenyezi Mungu kuomba kwa majina yake.
Amesema Sheikh Muhammad Swaleh Uthaimin Allah Amrehemu katika kubainisha maana ya Neno lake Mwenyezi Mungu: “Muombeni kwa majina yake”. Amesema Sheikh: ‘Ni kuyafanya ni njia ya kupata unachotaka katika maombi, kwa hivyo, utachagua jina linalonasibiana na matakwa yako, kwa mfano ikiwa unaomba msamaha basi utasema: “Ewe Mwenye kusamehe nisamehe”. Na hainasibiani kusema: “ Ewe Mwenyezi Mungu Mkali wa kuadhibu nisamehe, bali hii ni kama kumcheza Mwenyezi Mungu shere, na inatakiwa useme «Ewe Mwenyezi Mungu Mkali wa adhabu niepushie adhabu Yako’.
Ndugu MUislamu, kinachotakiwa kwetu ni kukitegemea zaidi kitabu cha Mwenyezi Mungu na hadithi za Mtume ﷺ katika kuyajua majina ya Mwenyezi Mungu, kwani haifai kabisa kwa yoyote kumpa Mwenyezi Mungu jina ambalo hakujiita jina hilo wala hajamuita jina hilo Mtume wa Mwenyezi Mungu ﷺ.
KWA FAIDA ZAIDI SIKILA MADA HII NA SHEIKH SHADDAD ALI