0%

https://uongofu.com/wp-content/uploads/2021/06/services-head-1.png

KUJIANDAA NA MWEZI MTUKUFU WA RAMADHANI

KUJIANDAA NA MWEZI MTUKUFU WA RAMADHANI

Mwenyezi Mungu Subhaanahu wa Taala Ametuwekea misimu mbali mbali na kwa minaajili ya kuipatiliza misimu hiyo kwa kurudi kwa Mwenyezi Mungu kwa kukufanya ibada, miongoni mwa misimu hiyo ni mwezi wa Ramadhani.

Mwenyezi Mungu mtakatifu ametuambia:

شَهْرُ رَمَضَانَ الَّذِي أُنزِلَ فِيهِ الْقُرْآنُ هُدًى لِّلنَّاسِ وَبَيِّنَاتٍ مِّنَ الْهُدَىٰ وَالْفُرْقَانِ ۚ فَمَن شَهِدَ مِنكُمُ الشَّهْرَ فَلْيَصُمْهُ ۖ وَمَن كَانَ مَرِيضًا أَوْ عَلَىٰ سَفَرٍ فَعِدَّةٌ مِّنْ أَيَّامٍ أُخَرَ ۗ يُرِيدُ اللَّهُ بِكُمُ الْيُسْرَ وَلَا يُرِيدُ بِكُمُ الْعُسْرَ وَلِتُكْمِلُوا الْعِدَّةَ وَلِتُكَبِّرُوا اللَّهَ عَلَىٰ مَا هَدَاكُمْ وَلَعَلَّكُمْ تَشْكُرُونَ

[Mwezi wa Ramadhani ambao umeteremshwa Qur’an ndani yake ambayo ni ubainifu na uongofu kwa watu na upambanuzi. Mwenye kuushuhudia Mwezi wa Ramadhani miongoni mwenu na afunge na atakayekuwa mgonjwa ama akawa safarini (na akala katika mwezi wa Ramadhani) basi ni juu yake kufunga katika siku nyengine, Mwenyezi Mungu awatakia wepesi na wala hawatakii uzito na ili mukamilishe hesabu ya masiku na mumtukuze Mweyezi Mungu, hakika mukifanya hivyo mutakuwa ni wenye shukrani]  [Al-Baqara:185]
Ndugu Muislamu mwezi mtukufu wa Ramadhani umetukabili inatupasa tuupokee kwa kumcha Mwenyezi Mungu na kufanya twaa na ibada kwa wingi na kukaa mbali na maovu kama tunavyo jua ya kuwa malipo ya amali njema huongezeka na vile vile malipo ya amali mbaya. Na mwezi huu mtukufu mwanzo ni kumi la rehma na kumi la maghfira na mwisho ni kuachwa huru na moto. Kufunga mchana ni wajibu na kusimama kwa ibada usiku ni sunna yenye kukamilisha faradhi. Ukifunga kwa imani na kutarajia malipo utasamehewa madhambi yaliyotanguliia. Ukifanya ‘umra ni kama uliye hijji. Milango ya pepo hufunguliwa na ya moto hufungwa. Na saumu ni ibada ya pekee ambayo Mola amejihusishia mwenyewe kama alivyosema Mtume ﷺ katika hadithi ya Bukhari aliyoipokea kutoka kwa Abu Huraira kuwa Mwenyezi Mungu amesema
[Amali zote za binaadamu ni zake ila saumu. Hakika ya saumu ni yangu na ni Mimi ndiye nitakaye ilipa na saumu ni kinga, ikiwa ni siku ya mmoja wenu kufunga basi asifanye machafu, wala asiseme maovu, basi atakapo tukanwa na yoyote au akataka kupigana naye basi amwambie mimi nimefunga. Naapa kwa Yule ambaye nafsi ya Muhammad iko mikononi mwake harufu ya kinywa cha mmoja wenu ni nzuri zaidi kuliko harufu ya miski, na mwenye kufunga ana furaha mbili, moja huipata akifungua saumu, na ya pili ni wakati akikutana na Mola wake].

WAKATI WA KUFUNGA MWEZI WA RAMADHANI

Fungeni kwa kuuona mwezi na fungueni kwa kuuona mwezi, kwani Mtume Swalla Llahu ‘alayhi wasallam amekataza kutangulia kufunga Ramadhani kwa siku moja ama mbili ila ikiwa mtu ana ada ya funga yake kama vile jumatatu na Alkhamisi, na haifai kufunga siku ya shaka, Amesema Ammar bin Yaasir “Mwenye kufunga siku ya shaka basi amemuasi Abal Qaasim, yaani Mtume ﷺ.
Na amepokea Bukhari kutoka kwa Ibnu ‘Umar ya kuwa Mtume Swalla Llahu ‘alayhi wasallam amesema katika maana ya Aya: [Msifunge mpaka muuone mwezi wala msifunguwe mpaka muuone mwezi, na iwapo mtafinikwa na mawingu kamilisheni hesabu ya thalathini].
Na atakaye uona mwezi kwa yaqini na amjulishe kiongozi aliyewakilishwa wala asifiche.
Na utakapotangazwa mwezi katika vyombo vya habari, kuingia kwa Ramadhani fungeni na kutoka kwa Ramadhani fungueni, kwani kutangaza kwa kiongozi aliyewakilishwa ndio hukumu.
Kufunga Mwezi wa Ramadhani ni nguzo moja katika uislamu na mwenye kupinga huwa kafiri.
Kufunga ni nguzo iliothibiti katika Qur-ani na mwenye kupinga huwa amemkanusha Mungu na Mtume na maelewano ya Waislamu wote Allah atwambia:

{يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا كُتِبَ عَلَيْكُمُ الصِّيَامُ كَمَا كُتِبَ عَلَى الَّذِينَ مِن قَبْلِكُمْ لَعَلَّكُمْ تَتَّقُونَ}     البقرة:183

[Enyi mlio amini mmefaradhiwa swaumu kama walivyofaradhiwa waliotangulia ili mupate kumcha Mungu]    [Al-Baqara:183]
Na saumu ni wajibu kwa kila muislamu alio baleghe na akawa na akili na uwezo wa kufunga, na mwanamke asiyekuwa na hedhi. Kafiri si wajibu kufunga, lakini ataulizwa siku ya kiyama na akisilimu halazimishwi kulipa zilizopita ila akisilimu katikati ya huo mchana wa Ramadhani atalazimika akamilishe siku na mtoto mdogo si wajibu kufunga mpaka abaleghe lakini yafaa tuwafundishe kufunga kama walivyokuwa masahaba. Na kubaleghe kwa mtoto hujulikana kwa moja katika mambo matatu: Jambo la kwanza; ni kufikia miaka kumi na mitano. Jambo la pili; ni kutokwa na manii kwa kuota, ama jambo jingine. Jambo la tatu; ni kutokwa na nywele za kinena. Na mtoto wa kike huzidisha Jambo la nne nalo nikupatwa na hedhi. Mtoto akipatwa na mambo haya tuliyoyataja, humlazimu faradhi zote za Mwenyezi Mungu ikiwa ana akili.
Na mwendawazimu si wajibu kufunga wala faradhi yoyote nyingine. Na wala mwenye kushindwa kufunga kwa sababu ya utu zima ama ugonjwa ambao hautarajiwi kupona, itakuwa si lazima kufunga lakini atalisha maskini kila siku alioacha atalisha maskini mmoja, kila maskini robo ya pishi kwa pishi za Mtume na ni bora kumuongezea kitoweo.

HUKMU YA WENYE UDHURU

Mgonjwa anayetarajiwa kupona, ikiwa saumu haimsumbui wala kumdhuru, haifai kula kama mtu huyo hana udhuru wowote. Na ikwa saumu inamsumbua lakini haimdhuru na inafaa afungue na ni karaha kufunga na ikiwa saumu itamdhuru ni haramu kufunga na popote atakapopoa itamlazimu ailipe saumu na akifa kabla ya kupona hana madhambi.
Na mwanamke mwenye mimba akiwa ni dhaifu ama mimba itamletea uzito akashindwa kufunga mwanamke huyo anaruhusiwa asifunge lakini akihisi ya kuwa na uwezo wa kufunga, atafunga hata ikiwa ni kabla ya kujifungua na itakapokuwa haiwezekani atasubiri baada ya kujifungua na kutwahirika na nifasi. Na mwanamke mwenye kunyonyesha akiogopea kupunguka maziwa atakula kisha atalipa.
Na msafiri akikusudia kukimbia saumu haifai ni lazima afunge. Na ikiwa hakukusudia kukimbia kufunga basi ana hiari ya kufunga na kutofunga. Na ikiwa kufunga na kutofunga ni sawa basi ni bora afunge.
Na ikiwa safari itamsumbua ni karaha kufunga iwapo mashaka yatazidi na ni haramu kufunga. Kwani Mtumeﷺalitoka kwenda Makka mwaka wa fat-hi na huku amefunga akaambiwa kuna watu wameshindwa kufunga na wanakusubiri wewe utakavyofanya. Mtume ﷺ akaitisha maji akanywa na watu wanamwangalia kisha na watu wakanywa, kisha akaambiwa kuna watu hawakufungua akasema Mtume ﷺ : [Hayo ni maasi].

HUKUMU YA ANAE FANYA KAZI YA DREVA

Na safari ni ya aina yoyote ile, kama madereva wa malori wakati wowote wanapoacha miji yao wanaruhusiwa kufungua kama vile wanavyoruhusiwa kupunguza swala za rakaa nne na kuzikusanya swala mbili mbili ikiwa mtu amesafiri katikati ya mchana ni vizuri akamilishe saumu ya siku ile ya kwanza ya safari.
Na haifai kufunga kwa mwenye hedhi na nifasi na wala haiswihi. Wakati wakitwahirika na hedhi ni lazima wafunge hata kama hawajaoga kisha watalipa siku walizokula.

KUHIMIZA KUSIMAMA USIKU WA RAMADHANI

Ndugu Muislamu Mtume ﷺ amehimiza kusimama kufanya ibada katika masiku ya Ramadhanii. Na mtu akiendelea na imamu kuswali mpaka akamaliza huandikiwa thawabu za mtu aliyesimama usiku kucha.
Na ni juu ya maimamu kumcha Mwenyezi Mungu katika kuswalisha tarawehe. Inafaa awachunge wanaomfuata asiwaendeshe mbio bila ya utulivu katika kusimama, kurukuu na kusujudu. Kwani Mwenyezi Mungu Amesema Subhaanahu wa Taala:

{لِيَبْلُوَكُمْ أَيُّكُمْ أَحْسَنُ عَمَلًا } [هود:7

[Ili akufanyieni mtihani ajuulikane ni nani miongoni mwenu mzuri zaidi wa vitendo.] [Huud:7]
Na Mtume alikuwa ni mwenye kupenda kheri zaidi na ni kielelezo chema lakini hakuzidisha zaidi ya rakaa kumi na moja sio katika Ramadhanii wala masiku mengine. Na Mtume ﷺ aliswali na jamaa katika Ramadhani kisha akaacha kwa kuogopea isifaradhishwe.
Na iliyo swahihi kutoka kwa Amirul muuminiina ‘Umar ibnul Khatwb ni kuwa alimuamrisha ‘Ubai ibn Ka’ab na Tamimi Daar waswalishe watu kwa rakaa kumi na moja na hii ndio idadi aliodumu nayo Mtumeﷺ na akafuata khalifa muongofu ‘Umar Ibnul khatwab ndio bora zaidi, na ikiwa mtu atazidisha kwa mapenzi yake sio kufuata sunna hapingwi lakini asifanye haraka kama wanavyofanya maimamu wengi waleo

Mungu atuafikie kupaliza nyakati za twaa na atuhifadhi na maovu na atuongoze njia iliyonyooka na atuepushe na njia ya motoni na atufanye wenye kufunga Ramadhani na wenye kusimama usiku kwa ibada kwa imani na kutarajia malipo na thawabu za Mwenyezi Mungu, hakika Mwenyyezi Mungu ni Mpaji na ni Mkarimu.
Namaliza maneno yangu kwa kumuomba Mwenyezi Mungu msamaha na kuwaombea Waislamu wote msamaha kutokana na madhambi yote.

FAIDA ZA KUFUNGA

Miongoni mwa faida ni kuivunja nafsi, kwani shibe ya maji na chakula na kuvaana na wanawake inapelekea kughafilika.
Faida nyingine ni moyo kukaa faragha kwa kumfikiria Mwenyezi Mungu na kuleta dhikri, kwani tumbo likiwa tupu husababisha moyo kunawirika.
Na faida nyingine ni kwa mtu tajiri hujua neema ya Mola juu yake. Kwa sababu ya kujinyima kwa muda fulani na hupelekea kumkumbuka ndugu yake aliyenyimwa neema ile moja kwa moja humsikitikia mwenzake maskini.
Na saumu hufanya mapitio ya damu kuwa membamba ambayo ndio mapitio ya shetani, kwani shetani anatembea katika mwili kama inavyotembea damu basi Mtume amesema “Fungeni mapito ya shetani kwa njaa.”
Saumu ya Mja haiwezi kutimia ila akiepuka yaliyo haramishwa katika hali zote.
Kwani Mtume ﷺ Amesema:

[من لم يدع قول الزور والعمل به فليس لله حاجة في إن يدع طعامه وشرابه]

[Ambaye haachi maneno ya uongo na kutumia uongo, Mwenyezi Mungu hana haja aache chakula chake na kinywaji chake]. Na watu wema ilikuwa wakifunga hukaa Msikitini ili kuepukana na kusengenya.

Sikiliza Mada hii na Sheikh Yusuf Abdi

Toa maoni yako

Begin typing your search above and press return to search.