KUPEANA NASWAHA
Enyi Waislamu ! watukufu! Makala yetu ya leo ni kuhusu maudhui muhimu anayohitaji Muislamu katika maisha yake nayo ni nasaha, na nasaha ni kumtakia kheri apewaye nasaha. Tukijua ya kwamba nasaha ni msingi mkubwa wa dini, bali Mtume ﷺ amesema kwenye hadithi yake:
الدِّينُ النَّصِيحَةُ ] قُلْنَا لِمَنْ ؟ ، قال : [ لِلَّهِ وَلِكِتَابِهِ وَلِرَسُولِهِ وَلِأَئِمَّةِ الْمُسْلِمِينَ وَعَامَّتِهِمْ] رواه مسلم]
[Dini ni nasaha, Dini ni nasaha, Dini ni nasaha. wakamuuliza maswahaba: ‘Kwa nani ewe Mtume ﷺ
akasema : Kwa Mwenyezi Mungu na kitabu chake na Mtume wake na viongozi wa kiislamu na Waislamu kwa jumla] [Imepokewa na Muslim]
Faida tunazozipata katika hadithi hii ni kule kuonesha ya kwamba nasaha ina daraja ya juu kabisa, na faida nyingine kutajwa sehemu ambazo nasaha hupatikana. Sehemu hizo ni nasaha kwa Mwenyezi Mungu Aliyetukuka nayo ni kufanya ibada kwa ajili Yake pekee na kutaka radhi Zake. Ama nasaha kwa kitabu chake ni kukisoma na kufuata maamrisho yaliyomo na kujiepusha na makatazo yaliyokatazwa ndani ya Kitabu hicho na kuziamini khabari zilizomo ndani yake. Ama nasaha kwa Mtume wake ni kumpenda na kufuata maamrisho yake na kujiepusha na makatazo yake na kuitetea heshima yake akiwa hai au akiwa amekufa. Ama nasaha kwa viongozi kuwaunga mkono kidhati kuwapa nasaha kwa maslahi ya umma katika ulimwengu wao na akhera yao. Pia kuwasikiliza na kuwatii katika mambo mema na kuitakidi kwamba ni lazima kufuata maamrisho yao ikiwa hawakuamrisha maasi. Mola Subhaanahu wa Taala Amesema:
{يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا أَطِيعُوا اللَّهَ وَأَطِيعُوا الرَّسُولَ وَأُولِي الْأَمْرِ مِنكُمْ} النساء:59
[Enyi mlio amini mtiini Mwenyezi Mungu na mtiini Mtume na viongozi katika nyinyi”] [Al-Nnisa:59]
Ama nasaha kwa Waislamu wa kawaida ni kuwapendea kheri na kuwaepushia uovu vile vile kuyazungumza mazuri yao na kuyaficha maovu yao na kuishi nao kwa upendo na udugu. Pia kuwasaidia endapo wanadhulumiwa. La kusikitisha ni kwamba Waislamu wamepuuza suala zima la kupeana nasaha. Tukijua ya kwamba kulipuuza suala hili ni kwenda kinyume na maamrisho ya Mwenyezi Mungu na hasara yake ni kubwa duniani na kesho akhera.
SIFA ZA MTOAJI NASAHA
Kuna mambo yatakiwa yazingaziwe na yafuatwe katika kadhia nzima ya nasaha Kati ya mambo hayo ni kama yafuatayo:
1. Ni lazima nasaha iwe kwa ajili ya Mwenyezi Mungu Mtukufu, na isiwe kwa ajili ya kutaka sifa au kuonekana na watu. Mwenyezi Mungu Subhaanahu wa Taala, Amesema:
{وَمَا أُمِرُوا إِلَّا لِيَعْبُدُوا اللَّهَ مُخْلِصِينَ لَهُ الدِّينَ} البينة:5
[Na hawakuamrishwa isipokuwa wamuabudu Mwenyezi Mungu hali ya kumtakasia yeye ibada] [Al-Bayyinah:5]
2. Ni lazima awe mtoaji nasaha ni mjuzi wa yale anayoyazungumza.
3. Ni lazima mtoaji nasaha awe mwaminifu. Mwenyezi Mungu Subhaanahu wa Taala Amesema akizungumza kuhusu Mtume Huud:
{أُبَلِّغُكُمْ رِسَالَاتِ رَبِّي وَأَنَا لَكُمْ نَاصِحٌ أَمِينٌ} الأعراف:68
[Nafikisha ujumbe wa Mola wangu na mimi kwenu ni mtoaji nasaha mwaminifu] [Al-Aaraaf:69]
4. Nasaha iwe kwa njia ya siri kwa kiongozi na raia, lakini ikishindikana basi hakuna ubaya ikiwa wazi na khaswa ikiwa ni mambo yaliyo kinyume na sheria waliyo kubaliana wanachuoni wote kwamba ni haramu.
Haishurutishwi kwa mtoaji nasaha awe mwanachuoni mkubwa na wala si lazima awe mwadilifu zaidi kuliko anayepewa nasaha. Amesema Imam Is’haaq Ibn Ahmad katika Utangulizi wa nasaha kumwandikia Ibn Al-Jauzia Mwenyezi Mungu awarehemu: ‘Kama ingekuwa hakatazi ovu aliye na elimu chache kumkataza mwenye elimu nyingi ingekuwa watu hawakatazani maovu na tungekuwa kama Bani Israail pale Mwenyezi Mungu Aliposema: ”Walikuwa hawakatazani maovu waliyokuwa wakiyafanya’.
Ndugu Muislamu ! Lau atafuatilia Muislamu hali za wema waliotangulia ataona vipi walipigiwa mfano katika kutoa nasaha na kuzikubali. Napenda nitaje mifano miwili nadhani itatosha:
Amesema Abubakar Swiddiq, radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake: “Hana kheri katika sisi asiyekubali nasaha na hana kheri katika nyinyi asiyeitoa nasaha”.
Amesema ‘Umar ibn Khattwab radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake: “Mwenyezi Mungu amrehemu mtu aliyeniletea zawadi ya aibu zangu”.
Ndugu Muislamu ! Tujibidiisheni katika kutoa nasaha. Na tumtakasie Mwenyezi Mungu katika kadhia nzima ya kutoa nasaha.Tunamuomba Mwenyezi Mungu atujaalie miongoni mwa wanaosikiliza mema na wakawa ni wenye kuyafuata.
KWA FAIDA ZAIDI SIKILA MADA HII NA SHEIKH ABUU HAMZA