0%

https://uongofu.com/wp-content/uploads/2021/06/services-head-1.png

UKOO WA BWANA MTUME ﷺ

UKOO WA BWANA MTUME ﷺ


UKOO WA MTUME ﷺ.

Ukoo wa Mtume wa Allaah  unajulikana kwa jina la Ukoo wa Haashim (Bani Haashim), na Haashim huyu ni babu yake Mtume wa Mwenyezi Mungu  aliyekuwa mtu mkarimu sana mwenye kuheshimika miongoni mwa watu wa kabila lake, na kwa ajili hii alipewa yeye jukumu la kuwanywisha na kuwalisha mahujaji waliokuwa wakija kutufu Al-Ka’aba, na hili lilikuwa ni jukumu adhimu sana analopewa mtu mwenye kuheshimika sana katika watu wa Makkah wakati ule.

Haashim alikuwa mtu wa mwanzo kuwalisha mahujaji chakula maarufu kinachoitwa ‘Thariyd’, nacho ni mikate mikavu inayokatwakatwa na kuchanganywa na mchuzi wa nyama. Heshima ya chakula hiki katika kuwakaribisha wageni ni mfano wa heshima ya biriani katika jamii yetu.

Jina lake hasa lilikuwa ni ‘Amru, lakini alipewa jina hili la Haashim kwa sababu yeye mwenyewe ndiye aliyekuwa akiikatakata mikate mikavu kwa ajili ya kutayarisha chakula hicho cha ‘Thariyd’.

Na neno ‘Haashim’ katika lugha ya Kiarabu maana yake ni kitu kikavu kilichokatikakatika.

Allaah Anasema juu ya mimea ya ardhi:

{فَأَصْبَحَ هَشِيمًا تَذْرُوهُ الرِّيَاحُ}

[Mimea Ikawa majani makavu yaliyokatikatika ambayo upepo huyarusha huku na kule].

Al-Kahf – 45

Imepokelewa kuwa Haashim alipokuwa akienda nchi ya Sham katika safari zake za kibiashara alipita Madina na alipokuwa hapo alimuoa Bibi mmoja aitwae Salma binti ‘Amru anayetokana na kabila la bani Najjar, akakaa naye muda wa siku chache kabla ya kuendelea na safari yake kwenda Sham na kumuacha Bibi Salma kwa wazee wake akiwa na mimba ya “Abdul-Muttwallib” bila watu wake waliopo Makkah kujua.

Wakati Haashim alipokuwa safarini, Salma alimzaa “Abdul-Muttwallib”, lakini Haashim hakuweza kurudi kwani alifariki dunia akiwa Gaza nchi ya Palastina.

“Abdul-Muttwallib” alizaliwa katika mwaka wa 497 baada ya Nabii ‘Isa (Alayhis Salaam) na akapewa jina la Shaybatul Hamd kutokana na unywele mmoja wa mvi aliokuwa nao kichwani, kwa sababu neno ‘Shaybah’ katika lugha ya Kiarabu maana yake ni mvi.

Bibi Salma aliyekuwa akiishi nyumbani kwa baba yake huko Madina alimlea mwanawe ‘Abdul-Muttwallib malezi bora.

Haashim alikuwa na watoto wa kiume wanne, watatu walikuwa Makkah na mmoja ambaye ni “Abdul-Muttwallib aliyekuwa Madina kwa mama yake, na majina yao ni; Asad na Abu Sayf na Nadhlah na “Abdul-Muttwallib, na alikuwa na watoto wa kike watano nao ni Ash-Shifaa na Khaalidah na Dhaifah na Ruqayyah na Jannah.

Jamaa zake walioko Makkah hawakuwa na habari zozote juu ya ndugu yao ‘Abdul-Muttwallib aliyekuwepo Madina, lakini habari zilimfikia Al Muttwallib ndugu yake Haashim ambaye ni ami yake ‘Abdul-Muttwallib aliyeifunga safari ya kwenda Madina kumchukua mtoto wa ndugu yake.

Al-Muttwallib alilia sana alipomuona ‘Abdul-Muttwallib, akambeba na kumbusu na kumkumbatia huku akilia kwa furaha, kisha akamtaka ende naye Makkah, lakini ‘Abdul-Muttwallib alikataa na kumwambia kuwa hawezi kuondoka bila ya ruhusa ya mama yake.

Mama yake alikubali baada ya kuombwa sana na kushikiliwa, lakini alipotakiwa na yeye afuatane nao Makkah alikataa na akachagua kubaki kwa wazee wake hapo Madina.

Al-Muttwallib aliingia Makkah akiwa amempakia ‘Abdul-Muttwallib juu ya ngamia na watu walipomuona walikuwa wakisema:

“Huyu hapa ‘Abdul-Muttwallib!”

Al-Muttwallib akawa anasema:

“Ole wenu! Huyu ni mwana wa ndugu yangu Haashim.”

Akamlea nyumbani kwake mpaka alipokuwa mkubwa, na Al-Muttwallib alipofariki akiwa safarini katika nchi ya Yemen mji wa Radman, watu wakamchagua ‘Abdul-Muttwallib kuwa kiongozi wao, akawa anatenda yale wazee wake waliyokuwa wakitenda katika heshima ya kuwalisha na kuwanywisha mahujaji. Alikuwa mkarimu sana na watu wake wakampa jina la “Al-Fayaadh” na maana yake ni “Mkarimu sana” akapata heshima kubwa sana asiyowahi kupata yeyote katika wazee wake waliotangulia na watu wake wakampenda sana na kumtukuza. [1]


[1] Ar-Rahiyq Al-Makhtuum – uk.40


Toa maoni yako

Begin typing your search above and press return to search.