SWALA YA TAWBA
Suali: Swala ya toba? Inaswaliwa vipi? Na ina rakaa ngapi? Na jee naweza kuiswali baada ya Swala ya Al- Asiri?
Alhamdulillah:
Jawabu: Hakika ni katika rahma za Mwenyezi Mungu kwa umma huu ni kuwa ameufungulia mlango wa toba, na haufungwi mpaka roho ifike kwenye koo au mpaka jua lichomoze kutoka magharibi.
Na katika rahma za Mwenyezi Mungu pia kwa umma huu ni kuwaekea ibada ambayo ni katika ibada bora kabisa, kupitia kwa ibada hii anajikurubisha mja aliefanya dhambi kwa mola wake kwa matarajio ya kukubaliwa toba yake nao ni “Swala ya toba” na haya ni baadhi ya mambo yanayohusiana na swala hii.
1- kufaa kisheria kwa mtu kuswali swala ya toba.
Wamekubaliana wanazuoni kufaa kwa swala ya toba.amepokea Abuu dauud (1521) kutoka kwa Abubakar Aswiddiq radhi za Mwenyezi Mungu zimfikie yeye kwamba amesema: nimemsikia Mtume MUHAMMAD ﷺ akisema:
مَا مِنْ عَبْدٍ يُذْنِبُ ذَنْبًا فَيُحْسِنُ الطُّهُورَ ، ثُمَّ يَقُومُ فَيُصَلِّي رَكْعَتَيْنِ ، ثُمَّ يَسْتَغْفِرُ اللَّهَ إِلَّا غَفَرَ اللَّهُ لَهُ ، ثُمَّ قَرَأَ هَذِهِ الْآيَةَ : “وَالَّذِينَ إِذَا فَعَلُوا فَاحِشَةً أَوْ ظَلَمُوا أَنْفُسَهُمْ ذَكَرُوا اللَّهَ فَاسْتَغْفَرُوا لِذُنُوبِهِمْ وَمَنْ يَغْفِرُ الذُّنُوبَ إِلَّا اللَّهُ وَلَمْ يُصِرُّوا عَلَى مَا فَعَلُوا وَهُمْ يَعْلَمُونَ
[hakuna mja atafanya dhambi kisha akajitwahirisha vizuri,kisha akasimama akaswali rakaa mbili, kisha akamuomba Mwenyezi Mungu msamaha isipokua ALLAH atamsamehe kisha akasoma aya hii [Na ambao pindi wafanyapo uchafu au wakajidhulumu nafsi zao humkumbuka Mwenyezi Mungu na wakamwomba msamaha kwa dhambi zao – na nani anaye futa dhambi isipo kuwa Mwenyezi Mungu? – na wala hawaendelei na waliyo yafanya na hali wanajua.] Amesahihisha hadithi hii Albany katika sahihi ya Abii Dauud.
Na amepokea Imam Ahmad (26998) kutoka kwa Abii darda’a radhi za ALLAH ziwe juu yake amesema nimemsikia Mtume ﷺ akisema:
[مَنْ تَوَضَّأَ فَأَحْسَنَ وُضُوءَهُ ثُمَّ قَامَ فَصَلَّى رَكْعَتَيْنِ أَوْ أَرْبَعًا (شك أحد الرواة) يُحْسِنُ فِيهِمَا الذِّكْرَ وَالْخُشُوعَ ، ثُمَّ اسْتَغْفَرَ اللَّهَ عَزَّ وَجَلَّ ، غَفَرَ لَهُ]
[Mwenye kutawadha na akafanya uzuri katika udhu wake kisha akasimama akaswali rakaa mbili au nne (ametia shaka mmoja wa wapokezi) kisha akamtaja Mwenyezi Mungu na akanyenyekea vizuri ndani ya rakaa hizo,kisha akamuomba msamaha Mwenyezi Mungu alietukuka basi Mwenyezi Mungu atamsamehe]
Wanasema wenye kuhakikisha sanad za hadithi.Hadithi hii sanad yake ni sahihi na ameitaja hadithi hii Albany katika [Silisilatul Ahaadithi Sswahiihah] (3398)
2- Sababu ya Swala ya Toba:
Sababu ya swala ya toba ni Muislamu kufanya madhambi sawa yawe ni madhambi makubwa au madhambi madogo,hivyo basi ni wajibu wake kutubia haraka iwezekanavyo,na inapendekezwa kwake kuswali rakaa hizi mbili ili afanye wakati wa toba yake tendo zuri ambalo linamkurubisha zaidi kwa Mwenyezi Mungu nayo ni swala hii,anajikurubisha kwa ALLAH kupitia swala hii na kutarajia yakwamba Mwenyezi Mungu atakubali toba yake na atamsamehe madhambi yake.
3- Wakati wa Swala ya Tawba.
Inapendekezwa kuswali Swala hii pindi tu Muislamu anapoazimia kufanya toba kutokana na dhambi alilolifanya,sawa toba hii iwe baada ya kufanya maasi pale pale, au akachelewesha toba.Na ni lazima kwa mwenye kufanya dhambi kuharakisha kufanya toba lakini akiichelewesha itakubaliwa,kwani toba inakubaliwa ikiwa hakutapatikana vizuizi vifwatavyo:
1- Roho ikishafika kwenye koo anasema Mtume ﷺ:
[إِنَّ اللَّهَ يَقْبَلُ تَوْبَةَ الْعَبْدِ مَا لَمْ يُغَرْغِرْ] رواه الترمذي وحسنه الألباني
[hakika Mwenyezi Mungu anakubali toba ya mja kabla hajatokwa na roho] Imam Albany ameifanya hadithi hii ni nzuri katika (swahih al tirmidhy) (3537)
2- Jua likichomoza kutoka upande wa magharibi Mtume ﷺ anasema :
[مَنْ تَابَ قَبْلَ أَنْ تَطْلُعَ الشَّمْسُ مِنْ مَغْرِبِهَا تَابَ اللَّهُ عَلَيْهِ] رواه مسلم
[Atakaetubu kabla ya jua kuchomoza kutoka magharibi Mwenyezi Mungu atakubali toba yake] [Imepokelewa na Imamu Muslim (2703)].
Na Swala hii inaswaliwa kila wakati hata katika zile nyakati ambazo imekatazwa kuswali ndani yake kama vile (baada ya al asiri) kwa sababu swala hii ni katika swala zilizo na sababu hivyo basi inaswaliwa pale inapopatikana sababu yake.
Anasema Sheikhul Islam ibnu Taymiyah Mungu amrahamu. “Swala zote zenye sababu zinaswaliwa ikiwa zitacheleweshwa mpaka mda wa makatazo kama vile sijda ya tilawa,tahiyyatul masjid,swala ya kupatwa kwa jua,na mfano wa swala baada ya tohara, kama ilivyokuja katika hadithi ya bilal r.a na vile vile swala ya istikhaara na vile vile swala ya toba, mtu anapofanya dhambi ni wajibu wake atubu kwa haraka, nayo ni sunna mpaka atakaposwali rakaa mbili na kutubu kama ilivyokuja katika hadithi ya abubakar swiddiq”
[Majmuul fataawa 215/23]
3- Sifa ya Swala ya Tawba:
Swala ya tawba ni rakaa mbili kama ilivyo katika hadithi ya Abubakar radhi za ALLAH ziwe juu yake na inapendeza kwa mwenye kutubu aiswali peke yake kwa sababu swala hii ni katika Sunna ambazo haifai kuziswali kwa jamaa,na ni sunna baada ya swala afanye istighfaar na amuombe Mwenyezi Mungu msamaha kwa hadithi iliyopokelewa na Abubakar radhi za Allah ziwe juu yake.
Na haijathibiti kutoka kwa Mtume ﷺ kuhusisha swala hii na sura maalum bali mwenye kuswali atasoma sura yeyote anayoitaka.
Na inapendeza mtu ajitahidi kufanya matendo mema pamoja na Swala hii kwani Mwenyezi Mungu anasema:
{وَإِنِّي لَغَفَّارٌ لِمَنْ تَابَ وَآمَنَ وَعَمِلَ صَالِحاً ثُمَّ اهْتَدَى} طه:82
[Na hakika yangu mimi ni mwingi wa msamaha kwa yule atakaetubu na akaamini na kufanya matendo mema kisha akaongoka] [Twaha:82.]
Na katika bora ya matendo mema atakayoyafanya mwenye kutubu ni kutoa Sadaka.
hakika mtu kutoa sadaka ni katika sababu kubwa za kufutiwa Madhambi Mwenyezi Mungu anasema:
{إِنْ تُبْدُوا الصَّدَقَاتِ فَنِعِمَّا هِيَ وَإِنْ تُخْفُوهَا وَتُؤْتُوهَا الْفُقَرَاءَ فَهُوَ خَيْرٌ لَكُمْ وَيُكَفِّرُ عَنْكُمْ مِنْ سَيِّئَاتِكُمْ}
[Mkizidhihirisha sadaka ni vizuri; na mkizificha mkawapa mafakiri kwa siri basi hivyo ni kheri kwenu, na yatakuondoleeni baadhi ya maovu yenu] [Al-Baqara:271]
Na imethubutu kutoka kwa Ka’ab bin Malik alimwambia Mtume baada ya Mwenyezi Mungu kukubali Tawba yake : Ewe mtume wa Mwenyezi Mungu ni katika tawba yangu nizitoe na mali zangu zote ziwe ni sadaka kwa ajili ya Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Mtume akasema:
[أمسك عليك بعض مالك فهو خير لك]
[Zuia baadhi ya Mali zako hilo ni kheri kwako] Ka’ab akasema mimi nabaki na fungu langu la ngawira za vita vya kheibar.
[Imepokelewa na Bukhari na Muslim.]
KWA UFUPI:
1. Swala hii ya Tawba imethibiti kutoka kwa Mtume ﷺ.
2. Swala hii inafaa kuswaliwa baada ya muislamu kufanya dhambi sawa liwe dhambi kubwa au dogo, sawa iwe ni baada ya kufanya madhambi hapo hapo ama baada ya mda.
3. Swala hii inaswaliwa kila wakati hata katika zile nyakati ambazo imekatazwa kuswali.
4- yakwamba inapendeza kwa mwenye kutubu pamoja na swala hii kufanya baadhi ya matendo mema kama vile kutoa sadaka na mengineyo.
** Chanzo: Hii ni Fatwa ya Sheikh Mahammad Swaleh Al Munajid