AR-RAHEEQ AL-MAKHTUM
Makuraishi walibaini kuwa kwa mafundisho hayo nafasi ya baadhi ya watu kujiona kuwa ni bora kuliko wengine, au kwa msemo mwingine, kuondolewa kwa ubwana na utwana, tabia iliyokuwa imezoeleka sana na Waarabu wakati huo, lilikuwa ni jambo gumu kukubalika. Walitakiwa kufuata muundo wa Dini mpya na kutekeleza mambo yanayoridhiwa na Mwenyezi Mungu ﷻ na Mtume Wake. Walitakiwa pia kujizuia na mambo ya dhulma, kwa namna yoyote ile, na maovu mengine waliyokuwa wakiyatenda asubuhi na jioni. Walikuwa wameelewa vizuri athari ya mafundisho hayo, lakini nafsi zao zilikuwa zinakataa kuikubali hali hiyo na kwa mtizamo wao waliona kuwa ni hali inayoondosha utukufu wao kwa sababu hapakuwa na kheri yoyote kwao.
{بَلْ يُرِيدُ الْإِنسَانُ لِيَفْجُرَ أَمَامَهُ}
[Lakini mtu anataka tu kuyakataa yaliyo mbele yake (ili ajipe moyo kuuia hakuna kitu huko Akhera, azidi kufanya maovu).] [75:5.]
Waliyaelewa yote hayo vizuri sana isipokuwa walikosa jambo la kufanya mbele ya mtu waliyekwisha mpa sifa ya kuwa mkweli mwaminifu, aliyekuwa mfano wa hali ya juu kabisa katika maadili ya kibinaadamu, na katika kuwa na tabia nzuri hawajawahikuona mfano wake kwa kipindi kirefu katika historia za mababa zao na mataifa mbalimbali waliyokuwa wakiyajua. Walikuwa hawajui la kufanya. Wafanye nini sasa? Walikwama katika hilo na walikuwa na haki ya kukwama.
Baada ya majadiliano marefu, hawakuona njia isipokuwa kwenda kwa ammi yake Abu Twalib na kumwomba arnzuie mtoto wa ndugu yake kueneza yale aliyokuwa akiyaeneza. Ili maombi yao yakubalike na kuonekana kuwa yanafaa, ya ukweli na uhakika waliona ni bora wakaseme maneno yafuatayo: ‘Kwa hakika mafunzo anayoyatoa kwa watu ili waiache miungu ye tu, na kusema kwake kuwa miungu hiyo haina manufaa na haina uwezo wowote ni matusi makubwa na ni udhalilishaji mkubwa wa miungu ye tu, na maana yake ni kuwafanya baba na babu zetu kuwa ni wapumbavu na kwamba kwa kufuata imani hiyo, tumepotea.’ Hii ndio njia waliyoiona inafaa kufuatwa na maneno ya kusemwa.*
*Arraheeq Al Makhtum 131-132