0%

https://uongofu.com/wp-content/uploads/2021/06/services-head-1.png

MICHAEL WOLFE

Michael Wolfe

Pamoja na kuwa Rais na prodyuza mkuu wa mfuko wa Unity Productions, Michael Wolfe (aliyezaliwa 3 Aprili 1945, Marekani) ni mtunzi wa vitabu vya kishairi, hadithi za kubuni, za masafa na historia. Pia ni mhadhiri wa masuala ya kiislamu katika vyuo vikuu nchini Marekani, vikiwemo kile cha Harvard, Georgetown, Stanford, SUNY Buffalo, na cha Princeton. Ana shahada ya fani ya fasihi (sanaa) kutoka Chuo Kikuu cha Wesleyan.

Ana asili ya dini mbili, Uyahudi kutoka kwa baba na Ukristo kutoka mama yake. Hivyo alikuwa na fursa ya kusherehekea sikukuu zote Hanukkah na Krismasi. Anaandika:

“Baba yangu ni Myahudi, mama ni ni Mkristo. kutokana na uchotara wangu, mguu mmoja upo katika Uyahudi na mwengine upo katika Ukristo. Imani zote zilikuwa hazina mashaka kwangu. Hata hivyo, ile iliyokuwa inahamasisha ‘wao wao tu’ (waliobarikiwa) [Uyahudi] niliiona haiungani mkono nami, na ile nyengine iliyojaa mafumbo [Ukristo] haikunifurahisha”

Kutembea kwake kwingi na kupenda vitabu kulimfanya kuufahamu Uislamu ambao kani (nguvu ya uvutano) yake ilishindwa kuzuiliwa na Michael. Moja ya sababu iliyomfanya akubaliane na Uislamu ni kukuta katika Uislamu mambo yanayoendana na matakwa yake. Hivyo anasema:

“Sikuweza kuorodhesha mahitajio yangu yote, lakini angalau nilikuwa najua kipi nikifatacho. Dini niitakayo mimi ni dini itakayoweza nieleza kuhusu metafizikia (falsafa ya kuchunguza chanzo cha uhai na maarifa) kwani metafizikia ndiyo sayansi. Sitaki ile inayopongeza utumizi duni wa akili, au iliyojaa mafumbo ili kuwaridhisha wachungaji. Isiyokuwa na wachungaji (viongozi), isiyokuwa na tofauti kati ya uasili na vitu vyake vilivyobarikiwa. Ambapo kutakuwa hakuna vita na nyama. Tendo la ndoa liwe ni la asili tu na sio eti kutokana na laana waliyopewa viumbe. Mwishowe, nilitaka ibada ya kila siku itakayoongoza nidhamu yangu. Zaidi ya yote, nilitaka jambo lililo wazi na uhuru wa kweli. Sikutaka niwe katika mkumbo wa kufata vitu kibubusa.* Na kila nilivyokua nausoma Uislamu, ndivyo ulivyokuwa ukiafikiana na matakwa yangu.”

Michael wolfe amekuwa Muislamu akiwa na miaka 40, baada ya kushindana na imani tofauti tofauti kwa miaka 20. Ingawa inatosha kwa mtu kufanya Hijja mara moja tu katika maisha, Bw. Wolfe katika kugombania kwake kupata radhi za Mwenyezi Mungu, amehiji si chini ya mara tatu, Hijja yake ya mwanzo ikiwa mwaka 1991. Akiuona ukweli wa Uislamu na ujinga wa baadhi ya watu katika faida ya Uislamu, Michael aliona haja ya kuandika haya:

“Rafiki zangu walioathiriwa na siasa hawakuridhishwa na chaguo langu jipya. Wote walichanganya Uislamu na viongozi madhalimu wa Mashariki ya Kati waliodhaniwa kutaka kufanya mapinduzi ili watawale. Vitabu walivyosoma, habari walizotazama vyote vilichukulia dini hii kama mpango wa kisiasa tu. Halikuwapo linalosemwa kuhusu ibada zake. Napenda kumkariri Mae West kwao pale alivyosema: “Muda wowote utakaochukulia dini mzaha, basi wewe ndio utakayechekwa.” Kihistoria, Muislamu anaiona dini kama ni hitimisho, mmea uliopevuka ambalo ulipandwa tangu wakati wa Adam. Imejengwa kwa msingi wa kuabudu Mungu mmoja kama Uyahudi, ambayo mitume wake Uislamu unawachukulia kama ni ndugu waliotoka kumoja na kilele chao kikiwa Yesu na Muhammad. kusema kweli, Uislamu umefanya kazi kubwa katika hatua ya kuirudisha ladha ya maisha kwa mamilioni ya watu. Kitabu chake, Qur’an kilimfanya Goethe kusema, “Mnaiona hii, mafundisho yake hayashindwi abadan; pamoja na mifumo yetu yote ya kibinaadam, hatuwezi kufika, na huo ndio ukweli hakuna mfumo wa kibinaadamu utakaofanikiwa”.

Akiongea na mtangazaji Bob Faw kuhusu imani yake mpya. Faw ‘alimpiga’ bwana Wolfe kwa swali hili: “Kwa kuwa ushakuwa muislamu, je kuna tofauti yoyote kwako labda!?” Wolfe akajibu: “Bila shaka ipo, umbile nilokuwa nalikosa zamani maishani mwangu lipo sasa nami. nalihisi kabisa.” Wolfe alivutiwa sana na mafundisho ya Uislamu kuwa kila mtu azungumze na Mungu mwenyewe, bila kuwa na kizuizi katikati:

“Hili jambo la kufanya mazungumzo na Mola wako mtukufu bila kuwa na balozi katikati, kusikohitaji jengo fulani au mtu maalum, kunanipendeza mno.”

Michael Wolfe anajulikana zaidi kwa filamu yake katika kipindi cha Nightline cha ABC iliyorushwa Aprili 18, 1997 ikijulikana kama An American in Mecca (Mmarekani Akiwa Makkah). Kipindi hiko kikateuliwa kuwemo katika tuzo za Peabody, Emmy, George Polk na National Press Club. Filamu ilishinda tuzo ya mwaka kutoka katika Baraza la Waislamu (Muslim Public Affairs Council). Michael Wolfe alishiriki kutengeneza, na kusimamia uhariri wa filamu ya masaa mawili iliyohusu maisha ya Mtume Muhammad iliyoitwa Muhammad: Legacy of a Prophet. Filamu hiyo ilioneshwa nchi nzima na PBS na baadae kuonyeshwa kimataifa na National Geograpghic International. Filamu ilituzwa na Cine Special Jury Award kwa filamu bora izungumziayo watu au mahali. Wakati wakutengeneza filamu hiyo, washiriki walihitaji kuperuzi kwingi katika maisha ya Mtume. Michael Wolfe mwenyewe anakiri kusoma Ibn Kathir na vitabu vyengine vya seerah (mwenendo wa Mtume). Kiukweli, kukawa na Wamarekani wengi ambao walisilimu baada ya kuona filamu hii. Katika mahojiano, Islam Online walimuuliza alichovuna baada ya zoezi hili kubwa la kuandaa filamu hii ya Muhammad na alijibu kama ifuatavyo:

“Nimemjua Mtume vyema zaidi kuliko mwanzo kabla hatujaanza kutengeneza filamu hii japokuwa kumsoma kwangu ndio kwanza kulianza. Kuna mengi ya kujifunza. Wakati tunatengeza filamu hii, niliweza kuona na kufahamu hali ya Waislamu wa Marekani. Najua sasa wepi ni Waislamu na vipi tunafanya. Ni kifungua jicho kwangu mimi kama Mmarekani niliyezaliwa hapa, ni jambo la faraja sana kukutana na watu kutoka sehemu mbalimbali, watu wenye lugha tofauti na mengineyo. Ni moja ya hazina za kuwa Muislamu.”

Katika mahojiano tofauti, Michael Wolfe kama mmoja wa waandaaji wa filamu ya Muhammad: The Legacy of a Prophet, alisema:

“Kwa Wamarekani wengi kutokuwa na uelewa wa imani yangu kunanishangaza sana. Japokuwa Uislamu ni dini inayokua kwa kasi zaidi, bado tabia nyingi za Wamarekani kuhusu Uislamu zimekuwa zikitawaliwa na chuki, kuelewa vibaya na hata wakati mwengine uhasama wa wazi. Wana uelewa mdogo tu kuhusu Mtume aliyefundisha dini hii na ipi ni misingi ya ibada zetu. Siasa na mila za watu wa mashariki ya Kati, gumzo la ugaidi vyote vimeshiriki kukandamiza uelewa wao mzuri wa dini. Ukichukulia kwamba kundi kubwa la Waislamu haliko hata Mashariki ya Kati bali Indonesia, utambuzi huu nasema kweli unapotosha.”

Filamu nyengine alizoshiriki Wolfe katika uandaaji ni Cities of Light: The Rise and Fall of Islamic Spain (Miji ya Muangaza: Kupanda na Kuporomoka Kwa Dola ya Kiislamu Hispania) na Prince Among Slaves (Mfalme Miongoni Mwa Watumwa). Sanjari na hilo, Wolfe ameshiriki katika vipindi mbalimbali vya redio. Anaandika makala maalumu iitwayo “From A Western Minaret” kwa ajili ya jarida la mtandaoni Beliefnet.com.

Kazi zilizochapishwa za Wolfe ni pamoja na The Hadj: An American’s Pilgrimage to Mecca. (New York: Atlantic Monthly Press, 1993. Kina kurasa 352); One Thousand Roads to Mecca: Ten Centuries of Travelers Writing about the Muslim Pilgrimage, (New York: Grove Press, 1997. Kina kurasa 656) ; na Taking Back Islam: American Muslims Reclaim their Faith, (Rodale Press, Pennsylvania, 2003. Kina kurasa 256). Baadhi ya tuzo alizopokea ni pamoja na Lowell Thomas Award, “Best Cultural Tourism Article, 1998”; Marin County Arts Council Writers Award, 1990, na 1983; California State Arts Council Writers Award, 1985. Michael Wolfe alitangazwa mshindi wa Tuzo ya 2003 ya Wilbur Award kwa kitabu bora cha mwaka kuhusu dini. Anaishi mwishoni mwa mtaa salama, uliofungwa, huko Santa Cruz.**

** Hii ilikuwa ni Dondoo (excerpt) ya kitabu cha Salim Boss kiitwacho“Wao Ima ni Waerevu Mno au Wajinga Mno” chenye kurasa 672 zote zimechapishwa kwa rangi (full colour). Ni tarjama ya kitabu kilichouzika sana kiitwacho “They are Either Extremely Smart or Extremely Ignorant”  Kwa usomaji wa ziada tembelea www.extremelysmart.org au www.facebook.com/muerevumno “**


Toa maoni yako

Begin typing your search above and press return to search.