0%

https://uongofu.com/wp-content/uploads/2021/06/services-head-1.png

MAISHA YA SAYYIDNA ALI KATIKA UHAI WA MTUME ﷺ

MAISHA YAKE KATIKA UHAI WA MTUME 

Mtume ﷺ alimuoza ‘Ali (r.a.) binti yake, Fatimah (r.a.), katika mwaka wa pili wa hijra. Akamtayarishia nguo laini na mto wa ngozi ambao uliwekwa majani ndani yake. Na yalikuwa maisha ya ‘Ali (r.a.) na mkewe ni ya kupa nyongo ulimwengu na niya kimaskini na ya kusubiri. [Al-Murtadha uk. 40]

Ali (r.a.) alikuwa pamoja na Mtume ﷺ katika vita vya Badri.Na mapambano yake na Al-Walid ibn ‘Utbah maarufu.

Pia alikuwa  pamoja na Mtume ﷺ katika vita vya Uhud. Na katika vita vya Khandaq, ‘Ali (r.a.) alipambana na ‘Amru ibn ‘Abdu-Wudd ambaye akilinganishwa na wapiganaji elfu moja kwa ushujaa wake. ‘Ali (r.a.) alimuua.Na katika vita vya Al-Hudaybiyyah, ‘Ali (r.a.) alikuwa mwandishi wa Waraka wa Sulhu. Na katika vita vya Khaybar, ‘Ali (r.a.) alishika bendera ya jeshi la Walslamu. Na akamuu wamwamba wa Wayahudi aitwaye Murahhab. Na ‘Ali (r.a.) aliwahi kuinua lango la ngome moja, ambalo huinuliwa na watu arubaini. [Al-Bidayah Wan-Nihayah Juz. 7 uk. 225]

Ali (r.a.) hakushiriki katika vita vya Tabuk kwa sababu alimwakilisha Mtume ﷺ kwa Ahli yake katika mji wa Madinah. ‘Ali (r.a.) akamshtakia Mtume ﷺ kuwa wanafiki wanasema maneno mengi kuhusu yeye. Mtume (s.a.w.) akamwambia kwa kumtuliza:

[ألا ترضى أن تكون مني بمنزلة هارون من موسى ، إلا أنه ليس نبي بعدي]

[Je, wewe huridhiki kuwa daraja yako kwangu mimi ni kama vile Harun kwa Musa, isipokuwa hakuna Mtume baada yangu.]     [AI- Bidayah Wan-Nihayah Juz. 7 uk. 225]

Mtume ﷺ alimpeleka Khalid ibn Al-Walid (r.a.) pamoja na Waislamu wengine kwa wakazi wa Yaman awalinganie katika Uislamu, wakakaa huko kwa muda wa miezi sita, ila Wayaman walikataa Kusilimu. Kisha Mtume ﷺ akampeleka ‘Ali (r.a.), akawasomea barua ya Mtume ﷺ . Wakasilimu watu wote wa kabila ya Hamadan. ‘Ali (r.a.) akamuandikia Mtume ﷺ kumjulisha kuhusu kusilimu kwao. Khabari hizo zilipomfikia Mtume (s.a.w.) akasujudu kwa furaha, kisha akainua kichwa chake akisema: “Amani iwe juu ya Hamadan, amani iwe juu ya Hamadan.” (Zad AI-Ma’ad Juz. 2 uk. 33)

Abu Bakr (r.a.) alipotumwa kuwa amiri wa Hijja na Mtume (s.a.w.) katika mwaka 9H, kisha baadaye akaenda ‘Ali (r.a.) na aya za Qur’ani kutoka Suratut-Taubah akawasomea watu siku ya kuchinja; basi Abu Bakar (r.a.) aliendelea kuwaongoza watu katika Hijja, ilipofika siku ya kuchinja alisimama ‘Ali (r.a.) akawasomea watu aya hizo. Kisha akatangaza kuwa kafiri hataingia Peponi, na baada ya mwaka huu si ruhusa kwa mshiriki yeyote kuhiji. Pia hairuhusiwi kutufu uchi kwenye Al-Ka’bah. Na mwenye mkataba wowote na Mtume (s.a.w.) basi utadumu mkataba wake mpaka umalizike muda wake. (Ibn Hisham Juz. 2 uk. 543)

Alipofariki Mtume (s.a.w.) ‘Ali (r.a.) alimuosha pamoja na ‘ammi yake ‘Abbas (r.a.) na watoto wa ‘Abbas: Al-Fadhl na Qutham, wakiwa pamoja na Shuqrah mtumwa wa Mtume (s.a.w.) na Usamah ibn Zaid, na ‘Aus ibn Khaulah. Na walisimamia mazishi ya Mtume (s.a.w.).

*Khulafaau Arrashidun 130-131

Toa maoni yako

Begin typing your search above and press return to search.