0%

https://uongofu.com/wp-content/uploads/2021/06/services-head-1.png

KUMTEGEMEA MWENYEZI MUNGU SUB’HANAHU WA TA’ALA

KUMTEGEMEA MWENYEZI MUNGU SUB’HANAHU WA TA’ALA

Namshukuru Mwenyezi Mungu ﷻ Ambae wanamtegemea yeye wenye kumtegemea, Aliyesema mwenye kumtegemea yeye anamtosha. Sala na Salamu zimshukie Mtume Muhammad, Mtume wa mwisho na Jamaa zake na Sahaba zake wote..
Kutegemea imechukuliwa katika neno (wakala) kama kusema fulani amelitegemeza jambo lake kwa fulani na akamtegemea yeye. Kwa hivyo, kutegemea ni tafsiri ya kutegemea kwa mwenye kutegemewa, na wala hamtegemei mwanadamu mtu mwingine ila anaitakidi kwake kupata jambo.
Kutafuta riziki ni maumbile ya kila mwanadamu. Utaona kukipambazuka mwanadamu anakwenda mbio, kwa sababu ya kutafuta riziki. Mkulima anajiandaa kwenda shambani. Mfanya biashara ajiandaa kwenda kwenye biashara yake. Kila mja hujiandaa kivyake. Na wote wanapata shida kwa sababu kila mmoja anataka kuhifadhi na kupata chakula cha yule anayemlazimu kumlisha; mke, watoto ama chakula cha familia yake.
Na hakika kuwa na himaya ya kutafuta cha kutosheleza au kutaka utajiri pamoja na kuwa njia yake ina vikwazo na safari ndefu. Yote hayo hupelekea lawama. Enyi Waja Dini ya kiislamu inakataa ya kwamba riziki inapatikana kwa njia ya udanganyifu. Na inakataza na kuchukia Muislamu kuitegemea njia hiyo ili apate riziki kutokana nayo. Na katika kuziba mlangu huu na njia hii. Amesema Mtume ﷺ:

[ولا يحملن أحدكم استبطاء رزقه أن يخرج إلى ما حرم الله عليه فإنه لا يدرك ما عند الله إلا بطاعته]    رواه عبدالرزاق والطبراني

[Isiwepelekeeni nyinyi uzito wa kupata riziki mukaingia katika kumuasi Mwenyezi Mungu. Hazipatikani zilizoko kwa Mwenyezi Mungu ila kwa Twaa yake].     [Imepokewa na Abdurazzaq na Al Twabraniy]
Kwa hivyo, ni yapi mapitio? Na nini suluhisho kutokana na maisha haya wanaoishi, watu wanatusiana, baadhi yao wanakula nguvu za wengine na baadhi yao kuwadhulumu baadhi. Na katika zama zetu hizi tunazoishi tunashuhudia hayo na kuna mifano mingi.
Ndugu Muislamu isome Hadithi hii inayotoka kwa Mtume wenu Muhammad, ikipokewa na ‘Umar Bin Khatwab (R.A) Akisema: “Nimemsikia Mtume ﷺ:

[لو أنكم تتوكلون على الله حق توكله لرزقكم كما يرزق الطير، تغدو خماصاً وتروح بطاناً]    رواه الترمذي

[Lau hakika nyinyi mungalikuwa munamtegemea Mwenyezi Mungu haki ya kumtegemea, Angaliwaruzuku nyinyi kama anavyowaruzuku ndege, anatoka asubuhi akiwa na njaa, na anarudi jioni akiwa ameshiba.]    [Imepokewa na Al-Ttirmidhi]
Kutokana na hadithi hii tunajifunza ya kwamba tukimtegemea Mwenyezi Mungu kikweli basi Mwenyezi Mungu atatupa tunalolitaka.
Ndugu Muislamu, zimekuja Aya nyingi na Hadithi nyingi zilizo sahihi kubainisha kumtegemea Mwenyezi Mungu kwa kila jambo letu na katika maisha yetu yote. Na hakika kumtegemea Mwenyezi Mungu ni jambo kubwa na ni amri kutoka kwa Mwenyezi Mungu akiwaamrisha waja wake Waislamu. Amewaamrisha hilo kwa hali zote. Amesema Mwenyezi Mungu ﷻ:

{وَلِلَّهِ غَيْبُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَإِلَيْهِ يُرْجَعُ الْأَمْرُ كُلُّهُ فَاعْبُدْهُ وَتَوَكَّلْ عَلَيْهِ ۚ وَمَا رَبُّكَ بِغَافِلٍ عَمَّا تَعْمَلُونَ}   هود:123 

[Na ni vya Mwenyezi Mungu tu vyote vilivyo fichikana katika ardhi na mbingu, na mambo yote yatarejezwa kwake. Basi muabudu Yeye na umtegemee Yeye. Na Mola wako Mlezi haghafiliki na yale mnayo yatenda.]   [Huud : 123]
Na Amesema Mwenyezi Mungu Subhaanahu wa Taala:

{وَتَوَكَّلْ عَلَى الْحَيِّ الَّذِي لَا يَمُوتُ وَسَبِّحْ بِحَمْدِهِ ۚ وَكَفَىٰ بِهِ بِذُنُوبِ عِبَادِهِ خَبِيرًا}      القرقان:58

[Na mtegemee Aliye Hai, ambaye hafi. Na umtukuze kwa sifa zake. Na yatosha kwake kuwa yeye ni Mwenye khabari za dhambi za waja wake.]    [Al-Furqan : 58].

Na Amesema tena Subhanahu wa Ta’aala:

{وَتَوَكَّلْ عَلَى الْعَزِيزِ الرَّحِيمِ }     الشعراء217

[Na umtegemee Mtukufu Mwenye nguvu Mwenye kurehemu.]   [Shuaraa : 217].

Na Amesema tena Mwenyezi Mungu Subhanahu waTa’aala:

{وَتَوَكَّلْ عَلَى اللَّهِ ۚ وَكَفَىٰ بِاللَّهِ وَكِيلًا}      الأحزاب:3

[Na mtegemee Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu anatosha kuwa ni wa kutegemewa.]     [Ahzaab : 3].
Na katika Hadithi ya Mtume ﷺ inatuelezea kuhusu kumtegemea Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala). Imetokana na Abu Hurayra radhi za Mwenyezi Mungu zimshukie Akipokea kwa Mtume ﷺ:

[يدخل الجنة أقوام أفئدتُهم مثل أفئدة الطير]    رواه مسلم

[Wataingia peponi watu nyoyo zao ni mfano wa nyoyo za ndege.]  [Imepokewa na Muslim]
Maana yake wanaomtegemea Mwenyezi Mungu na kumesemwa nyoyo zao ni laini.Ewe Ndugu, Muislamu Hakika kutegemea ni kusadikisha kutegemea moyo kwa Mwenyezi Mungu katika kuleta mambo mema na kuondosha madhara. Vilevile kumtegemea Mwenyezi Mungu ni ukweli na imani na utulivu na kua na mafungamano baina ya mja na Mola wake.

Amesema Ibnul-Qayyim Mwenyezi Mungu Amrehemu : “Kutegemea ni nusu ya imani na ni nusu ya pili ya kurudi kwa Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu amewaahidi wenye kumtegemea malipo makubwa na malipo mengi “Katika Hadithi iliyoko katika sahihi mbili hadithi ya watu sabini elfu wataingia peponi bila hisabu, nao ni wale ambao hawataki kuzunguliwa, wala hawajichomi, wala hawatabiri ndege wanamtegemea Mola wao”.
Na hakukuwa kutegemea Mwenyezi Mungu kunakanusha kuchukua sababu za sheria zilizo halali. Mfano mtu akisema mimi sitafuti riziki wala siendei mbio, ikiwa imeandikwa kwangu niwe tajiri nitakuwa tajiri bila kutaabika wala shida, ikiwa Sikuandikiwa basi siwi hakuna haja nisumbuke wala nipate taabu. Kwahivyo, linalotakiwa ni kumtegemea Mwenyezi Mungu pamoja na kufuata sababu.
Na Mtume ﷺ Amewasifu wenye kumtegemea Mwenyezi Mungu kwa sifa mbili:
1. Kwenda kutafuta riziki.
2. kutegemea sababu za kisheria.
Mwenye kukosa moja wa sifa mbili hizi hakika ameangukia patupu na amefanya shirki. Na mwenye kwenda kwa sababu zilizo halali na akamtegemea mola wake na akamshukuru mola kwa kila yanayopendeza na akasubiri hukumu ya Mwenyezi Mungu wakati anapopata msiba na machukivu amefaulu na amefadhilisha ukamilifu wote.

SIKILIZA MADA HII NA SHEIKH SHADDAD ALI 

Toa maoni yako

Begin typing your search above and press return to search.