Suali: Je Talaka ya mtu aliyelazimiswa inapita??
Jibu:
*Alhamdulillah.*
Maulamaa wengi wamekubaliana kwamba talaka ya mtu aliyelazimishwa haipiti , wakalitolea dalili jambo hili kwa Hadithi iliyopokewa na Ibn Majah (2043) kutoka kwa Abuu Dharr al-Ghifariy ( Radhi za Allah ziwe juu yake) amesema: Mtume wa Mwenyezi Mungu ﷺ amesema:
“Hakika Mwenyezi Mungu amewasamehe umma wangu makosa, kusahau, na kile walicholazimishwa kukifanya.”
Imehesabiwa kuwa sahihi na Shaykh Al-Albani katika Sahih Ibn Majah.
Al-Bayhaqiy amepokea katika as-Sunan al-Kubra (15499) kutoka kwa Ibn ‘Abbas ( Radhi za Allah ziwe juu yao) amesema: Mtume wa Mwenyezi Mungu ﷺ amesema: amesema:
*”Mtu aliyelazimishwa hana talaka -yaani talaka haipiti-“*
Ibn al-Qayyim aliihesabu kuwa sahihi katika I’lam al-Muwaqqi’in (3/38).
Na imekuja katika al-Mawsu’ah al-Fiqhiyyah (29/17-18):
“Maulamaa wengi wa fiqhi wamekubaliana kwamba talaka ya mtu aliyelazimishwa haipiti iwapo kulazimishwa huko ni kwa nguvu sana kama tishio la kuuwawa ,na kukatwa kiungo, na kupigwa vibaya, na kadhalika. Hii ni kwa mujibu wa Hadithi ya Mtume ﷺ:
‘Hakuna talaka wala kumuacha huru mtumwa katika hali ya kufungwa.’
Na Hadithi iliyotangulia:
‘Hakika Mwenyezi Mungu amewaondolea umma wangu makosa, kusahau, na kile walicholazimishwa.’
Na kwa sababu mtu huyo hana matakwa wala makusudio ya kufanya jambo , hivyo anakuwa kama mwendawazimu au mtu aliyelala.
Lakini ikiwa kulazimishwa huko ni kudhaifu au ikathibiti yakwamba mtu huyo aliyelazimishwa hakuathirika na jambo hilo , basi talaka yake itahesabiwa na kupita kwa sababu ana hiari .”
Shaykh al-Islam Ibn Taymiyyah ( Mungu amrahamu) amesema:
“Talaka ya mtu aliyelazimishwa haipiti. Na Kulazimishwa kunatokea ima kwa mtu kutishiwa au mtu kuamini kuwa talaka ile itamdhuru katika nafsi au mali yake hata kama hakuna tishio la moja kwa moja…”
(Al-Ikhtiyarat, uk. 366)
Ibn Juzayy katika al-Qawanin al-Fiqhiyyah (uk. 151) amesema:
“Ama mtu aliyelazimishwa kutoa talaka kwa kupigwa, kufungwa jela au kutishwa, basi talaka hiyo haijapita wala haimlazimu kwa mujibu wa Imamu Malik, Imamu Shafi’i na Ahmad bin Hanbal – kinyume na Abu Hanifa.”
Pili:
Wanazuoni wamebainisha masharti ya kulazimishwa ambayo kwayo Talaka haiswihi wala haipiti . Baadhi ya masharti hayo yameelezewa kwenye nukuu zilizopita, na kuwa kulazimishwa kudhaifu hakuhesabiwi kama ni kulazimishwa na hakuzuii kutokea na kupita kwa talaka.
Ibn Qudamah katika al-Mughni (10/351) amesema:
Masharti ya kulazimishwa ni matatu:
1. Awe anayetishia ana uwezo kwa mamlaka au nguvu, kama mwizi na mfano wake.
2. Mhusika aamini kuwa tishio litatekelezwa na litampata endapo hatatii matakwa yake.
3. Tishio liwe na madhara makubwa kama kuua, na kupigwa sana, na kufungiwa , au kutiwa jela kwa muda mrefu.
Lakini matusi, kashfa, au kuchukuliwa mali kidogo hayahesabiwi kama kulazimishwa.
Na Mwenyezi Mungu Anajua Zaidi.