0%

https://uongofu.com/wp-content/uploads/2021/06/services-head-1.png

JE NI KITU GANI KILICHOUMBWA KABLA YA VITU VYOTE

Suali : Je ni kitu gani kilichoumbwa kabla ya vitu vyote?

Jibu:  Kwanza kabisa msingi na marejeo ya kujua mambo yaliyotokea huko nyuma ni Qur’ani na sunnah (Hadithi za Mtume Muhammad (ﷺ) na pia ufuhamu wa wanavyuoni wakubwa kuhusu hizo Aya na hadithi za Mtume (ﷺ)
Kwa hivyo, kutokana na hali hiyo wanavyuoni wametafautiana pakubwa kuhusu suala hili la kitu kilichoumbwa mwanzo kabla ya vitu vyote.

Sababu ya kutafautiana :
Ni kutokamana na jinsi kila mmoja wao alivyozifahamu hizo dalili na kuzijengea hoja mbalimbali.

Kauli ya kwanza :  Ni Kalamu
Baadhi ya wanavyuoni wanasema kua kalamu ndiyo ya kwanza kuumbwa kati ya vitu vyote.

Dalili yao :
Hadithi ya U’baadah Ibnu Alswaamit iliyopokelewa na Al-imam Ahmad na Abuu Daawuud na Alturmidhiyy, anasema kuwa : alisema Mtume wa Allah rehma na amani zimshukie

إِنَّ أَوَّلَ مَا خَلَقَ اللَّهُ الْقَلَمَ فَقَالَ لَهُ : اكْتُبْ ، قَالَ : رَبِّ وَمَاذَا أَكْتُبُ ؟ قَالَ : اكْتُبْ مَقَادِيرَ كُلِّ شَيْءٍ حَتَّى تَقُومَ السَّاعَةُ

” Hakika kitu alichokiumba Allah kwanza ni kalamu, akiamrisha kua: andika, kukapitishwa kuanzia hapo kila kitu kitakachotokea mpaka siku ya Qiyama “

Hoja yao:
Hadithi hii inaonyesha kuwa kitu kilichoumbwa kwanza ni kalamu.

Kauli ya pili : Ni Arshi
Anasema Al-imam Ibnu Kathiyr:
Jamhuri ya wanavyuoni wamekubaliana kua A’rshi ndiyo iliyoumbwa mwanzo kabla ya vitu vyote .

Dalili yao:
Hadithi ya Abdullah Ibnu A’mr Ibnul-‘Aaswi, katika Swahiyh Muslim, alisema Mtume (ﷺ)

كَتَبَ اللَّهُ مَقَادِيرَ الْخَلَائِقِ قَبْلَ أَنْ يَخْلُقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ بِخَمْسِينَ أَلْفَ سَنَةٍ ، قَالَ : وَعَرْشُهُ عَلَى الْمَاءِ

” Mwenyezi Mungu aliandika na kupanga mipango ya viumbe vyote kabla hajaumba mbingu na ardhi kwa kipindi miaka elfu hamsini , na kiti chake cha enzi kilikuwa juu ya maji .”

Hoja yao :

Wanasema kua hii hadithi inamaanisha kua kuandikwa kwa mipangilio ya kila kitu kulitokea baada ya kuumbwa kwa A’rshi ..
Na wanaijibu hadithi ya kuumbwa kwa kalamu kwanza kwamba hiyo hadithi inamaanisha kua kalamu iliumbwa baada ya a’rshi na maji , Na Ibnu Hajar vilevile alikubaliana na hilo, pamoja na Ibnu Taymiyyah na IbnulQayyim.

Kauli ya tatu : Maji
Kauli ya tatu inasema kuwa maji ndiyo yaliyoumbwa kabla ya a’rshi na kalamu .

Dalili yao :
Hadithi marfuu’u kupitia kwa Abuu Raziyn Al-Uqayliyy: ” Maji ndiyo yaliyoumbwa kabla ya a’rshi ”

Na Al-imam Alssuddiy amepokea kwa riwaya nyingi kua: Mwenyezi Mungu hakuumba kitu chochote kabla ya kuumba maji.

Hoja yao :
Hizi hadithi zinaonyesha kuwa Mwenyezi Mungu aliumba maji kwanza kabla ya kuumba a’rshi.

Dalili nyingine :

Anasema Allah Mtukufu

وَهُوَ ٱلَّذِي خَلَقَ ٱلسَّمَٰوَٰتِ وَٱلۡأَرۡضَ فِي سِتَّةِ أَيَّامٖ وَكَانَ عَرۡشُهُۥ عَلَى ٱلۡمَآءِ لِيَبۡلُوَكُمۡ أَيُّكُمۡ أَحۡسَنُ عَمَلٗاۗ   سورة هود:7

[ Na Allah ndie aliye umba mbingu na ardhi na a’rshi yake ilikua juu ya maji, ili awape mtihani ni yupe kati yenu mwenye matendo mazuri zaidi]   Sura Huud: 7

Hoja yao :
Hii aya inamaanisha kua Allah aliumba maji kwanza kabla ya A’rshi , na arshi ilikua juu ya maji kabla hajaumba mbingu na ardhi…
Kwa hivyo wanasema kua yaliumbwa maji kwanza kisha a’rshi kisha kalamu na kisha mbingu na ardhi.

Kwa ufupi :
Wanavyuoni wengi wamekubaliana kua Mwenyezi Mungu aliumba A’rshi na maji kabla ya kuumba kila kitu.

Allah ndie anajua zaidi

Yametayarishwa na :
Abuu Yuusuf Sha’baan Abuuhurairah (Allah amuhifadhi)

Begin typing your search above and press return to search.