0%

https://uongofu.com/wp-content/uploads/2021/06/services-head-1.png

ISRAI NA MI’RAJ


AR-RAHEEQ AL-MAKHTUM


Wakati Mtume () yupo katika hatua ambayo Da’awa ilikuwa ikipita katika kipindi cha mafanikio na matatizo, nyota za matumaini zilianza kuangaza katika maeneo ya mbali. Huo ndio wakati lilituka tukio la Israi na Mi raji, kuhusu tukio hili zipo kauli zinazotofautiana:-

1. Inasemekana Israi ilikuwa katika ule mwaka ambao Allah (ﷻ) Alimkirimu ndani yake Utume, ameichagua kauli hii Al-Tabary.

2. Inasemekana Israi ilikuwa baada ya kupewa Utume kwa miaka mitano, kauli hii imepewa nguvu na Al-Nawawy na Al- Qurtubi.

3. Inasemekana Israi ilikuwa usiku wa ishirini na saba kafika mwezi wa Rajab, mwaka wa kumi wa Utume, kauli hii imepewa nguvu na mwanachuoni mkubwa Al-Mansour Foury.

4. Inasemekana Israi ilikuwa kabla ya Hijra kwa miezi kumi na sita yaani katika mwezi wa Ramadhani mnamo mwaka wa kumi na mbili wa Utume.

5. Inasemekana Israi ilikuwa kabla ya Hijra kwa mwaka mmoja na miezi miwili yaani Muharram mnamo mwaka wa kumi na tatu wa Utume.

6. Inasemekana Israi ilikuwa kabla ya Hijra kwa mwaka mmoja yaani Rabiul Thani mnamo mwaka wa kumi na tatu wa Utume.

Kauli tatu za mwanzo zimepingwa kwa sababu Bi Khadija (Radhi za Allah ziwe juu yake) alifariki mwezi wa Ramadhani mwaka wa kumi wa Utume na kifo chake kilitokea kabla ya kufaradhishwa kwa Swala tano na hakuna tofauti kuwa Swala tano zilifaradhishwa katika usiku  wa lsrai‘

Ama kuhusu kauli tatu zilizobaki sikupata kile ambacho ningekitumia kutia nguvu moja katika kauli hizo isipokuwa mtiririko wa Surat Al-Israi, ambao unafahamisha kuwa Israi ilichelewa sana. Wanazuoni wa hadithi wamepokea ufafanuzi wa tukio hili na hapa chini tumauleta kwa ufupi katika maneno yafuatayo:- Ibnu Al- Qayyim amesema; ”Mjumbe wa Mwenyezi Mungu () , kwa kauli sahihi, alipelekwa kimwili akiwa amempanda Buraq, akifuatana na Jibril (rehema na amani ziwe juu yao), kutoka Msikiti Mtukufu mpaka Baytul Al-Muqaddas, akamfunga Buraq katika kikuku cha mlango wa Msikiti, na kisha Kusali pamoja na Mitume, yeye akiwa Imamu. Baada ya hapo, usiku huo huo kutoka Baytul Al-Muqaddas akapandishwa katika uwingu wa dunia akifuatana na jibril (Rehema na amani ziwe juu yae) aliyekuwa akibisha hodi kwa ajili yake, akafunguliwa na huko akamwona Adam (Rehema na amani ziwe juu yae) baba wa watu wote, akamsalimia, akamkaribisha na akamjibu salamu yake na akaukubali Utume wake. Mwenyezi Mungu (ﷻ) Akamuonesha roho za watu wema zikiwa upande wake wa kuume na roho za watu waovu zikiwa upande wake wa kushoto. Baada ya hapo, akapandishwa uwingu wa pili, Jibril (Rehema na amani ziwe juu yake) akaomba kuingia, akafunguliwa na hapo akamwona Yahya bin Zakaria na Isa bin Mariam (Rehema na amani ziwe juu yao), akakutana nao, akawasalimia, na wao wakamjibu salamu yake, wakamkaribisha na wakaukubali Utume wake. Kisha akapandishwa mpaka uwingu wa tatu, hapo akamwuona Yusuf (Rehema na amani ziwe juu yake), akamsalimia, naye akamjibu salamu yake, akamkaribisha na akaukubali Utume wake. Baada ya hapo akapandishwa uwingu wa nne ambako alimkuta Idrisa (Rehema na amani ziwe juu yake), akamsalimia, akamkaribisha na akaukubali Utume wake. Kisha akapandishwa uwingu wa tano, na hapo akamwuona Harun bin Imran (Rehema na amani ziwe juu yake), akamsalimia, nae akajibu salamu yake na kumkaribisha na akaukubali Utume wake. Baada ya hapo akapandishwa katika uwingu wa sita na akamkuta hapo Musa bin Imran (Rehema na amani ziwe juu yake) akamsalimia, naye akajibu salamu yake, akamkaribisha na akaukubali Utume wake. Alipompita, Musa (Rehema na amani ziwe juu yake) alilia na alipoulizwa ni jambo gani linalokuliza? Akajibu, ‘Ninalia kwa sababu Kijana amepewa Utume baada yangu, na katika umma wake wataingia peponi kuliko watakaoingia peponi kutoka katika umma wangu.” Kisha akapandishwa kwenye uwingu wa saba, ambako alikutana na Ibrahim (Rehema na amani ziwe juu yake), akamsalimia naye akajibu salamu yake, akamkaribisha na akaukubali Utume wake. Baada ya hapo ndio akanyanyuliwa na kupelekwa Sidratil-Muntaha, kisha akanyanyuliwa hadi Baytul Ma’amour, naye akapandishwa kupelekwa kwa Allah Mwingi wa Utukufu, akasogea (Mtume ()) mpaka umbali wa kiasi cha masafa ya Qausain (pinde mbili) au karibu zaidi kuliko hivyo, Allah (ﷻ) Akayafunua kwa Mja Wake yale Aliyoyafimua, na Akamfaradhishia Swala Mtume () akazipokea na kuanza kurejea mpaka alipofika mahala alipo Musa (Rehema na amani ziwe juu yake) ambaye alimwuliza; ”Umepewa amri ya jambo gani? Mtume () akamueleza, ”Ameniamrisha Swala khamsini”, Musa (Rehema na amani ziwe juu yake) akamwambia, ’Kwa hakika umma wako hawataweza kulitekeleza jambo hilo, rejea kwa Mola wako na umwombe Akupunguzie iwe takhfifu kwa umma wako.” Akageuza uso na kumwangalia Jibril (Rehema na amani ziwe juu yake), kwa jicho la kumtaka ushauri katika jambo hilo, naye akampa ishara kuwa ndiyo ukitaka Akapanda naye jibril (Rehema na amani ziwe juu yake) mpaka akafika kwa Mwenyezi Mungu (ﷻ) na hali ya kuwa Yeye yu Mahali Pake; (Tamko hili ni la Bukhari). Katika mapokezi mengine,  Akampunguzia Swala kumi kisha akateremshwa mpaka mahali alipokuwa Musa (Rehema na amani ziwe juu yake)” na akamweleza idadi ya Swala zilizopunguzwa. Musa (Rehema na amani ziwe juu yake) akamwambia, ’Rejea kwa Mola wako na umwuombe Akupunguzie tena.” Inasemwa kuwa hakuacha kwenda na kurudi kati ya Mus; (Rehema na amani ziwe juu yake) na Mwenyezi Mungu (ﷻ) mpaka Swala zilipobaki tano. Musa (Rehema na amani ziwe juu yake) akamtaka kurejea kwa Mwenyezi Mungu tena na kuomba kupunguziwa, Hapo Mtume akajibu; ”Kwa hakika ninamwonea haya Mola Wangu na sasa mimi ninaridhia na ninakubali Swala nilizopewa.” Alipokwenda umbali kidogo, alilingania mlinganiaji; ”Nimezipitisha faradhi Zangu na Nimewapunguzia waja Wangu (2)

Ibn Al-Qayyim amejadili kuhusu suala hili la Mtume () kumwona Mola Wake, Allah Aliyetukuka Mwenye Utukufu na kisha akayataja maneno ya Ibn Taymiya kuhusu suala hili. Matokeo ya utafiti ni kuwa, ”Kumwona Allah (ﷻ) kwa macho ni jambo ambalo halikuthibiti kabisa. Hiyo ni kauli ambayo haikusemwa na yeyote katika masahaba. Na kile tunachokisema kutoka kwa Bin Abbasi kuwa Mtume () alimwona Allah (ﷻ) moja kwa moja. Ni kuwa alimwona kwa moyo si kwa macho, kauli ya kwanza haipingani na ya pili.” Kisha anasema: ’Ama kuhusu kauli yake Mwenyezi_Mungu katika Suratu Al-Najm

ثُمَّ دَنَا فَتَدَلَّىٰ

Kisha akakaribia (kwa Mfume) na akateremka.”

Huko siko kule kukaribia ambako kumetajwa katika kisa cha Al-Israi, kwani kukaribia ambako kumo katika Suratu Al- Nnajm, ‘Ni kukaribia kwa Jibril (Rehema na amani ziwe juu yake) na kusogea zaidi kama alivyosema Aisha na Ibn Masoud (Radhi za Allah ziwe juu yao). Mtiriko wa maneno unafahamisha juu ya maana haya; ”Amekukaribia na kusogea sana.” katika hadithi ya Al-Israi, kuna maana kuwa kukaribia huko ni kukafibia kwa Mola Mtukufu Aliyetukuka na kuwa karibu kwake zaidi. Hakuna kupingana katika Surat Al-Nnajm. Lakini kutajwa huko ndani yake ni kuwa yeye alimwuona mara nyingine mbele ya Sidratil – Muntaha, na huyo ni Jibril (Rehema na amani ziwe juu yake). Mtume Muhanunad () alimwuona Jibril (Radhi za Allah ziwe juu yao) katika sura yake halisi mara mbili; ya kwanza hapa duniani na mara nyingine katika Sidratil-Muntaha (3) na Mwenyezi Mungu (ﷻ) Ndiye Mjuzi zaidi.

Lilituka lile tukio la Mtume () kupasuliwa tena kifua chake kwa mara ya pili. Kwa ujumla katika safari hii aliona mambo mengi; Miongoni mwa hayo ni kule kuletewa maziwa na pombe na kuchagua maziwa badala ya pombe, na pakasemwa, ”Umeongozwa katika fitrah na umechagua na kupata fitra, ama kwa hakika laiti ungechukua pombe umma wako wote ungepotea.” Katika safari hiyo alionyeshwa mito minne huko peponi, mito miwili iko nje na mito miwili iko ndani. Mito iliyo nje ni mto Nail (Nile) na Furat (Euphrates), na maana ya mambo hayo ni kuwa ujumbe wake utafanya makazi yake katika majangwa yenye rutuba katika Nail na Furat na watu wake ndio watakao kuwa wasimamizi  wa Da’wa ya Kiislamu, kizazi baada ya kizazi, na si kuwa maji ya mito miwili hiyo yanachimbuka kutoka peponi.

Alionyeshwa Malaika mwangalizi wa Moto wa jahannam ambaye hacheki, mwenye uso usio na furaha wala bashasha. Alionyeshwa pepo na moto. Alionyeshwa’ walaji wa mali za yatima kwa dhulma, waliokuwa na midomo kama ya ngamia, wanatupiwa midomoni mwao vipande vya moto kama mawe na kisha kutokea katika tupu zao za nyuma.

Alionyeshwa walaji wa riba waliokuwa na matumbo makubwa yaliyowafanya wasiweze hata kuondoka mahala walipokuwapo. Alipita na kuwaona watu wa Firauni wakionyeshwa moto na hali wakipita wakiukanyaga.

Alionyeshwa wazinifu, mbele yao kukiwa na nyama iliyonona vizuri na pembeni mwao kukiwa na nyama duni iliyooza yenye uvundo. Wakawa wanakula. ile nyama duni iliyooza yenye uvundo, na wanaiacha ile nzuri iliyonona. Alionyeshwa wanawake wanaonasibisha waume zao watoto ambao si wao (watoto wa zinaa) hawa walikuwa wametundikwa kwa matiti yao.

Na aliuona msafara wa kibiashara wa watu wa Makka wakati wa kwenda na wakati wa kurudi kwake, na aliwafahamisha watu hao juu ya ngamia aliyewatoroka na alikunywa maji yao yaliyokuwa yamefunikwa na hali ya kuwa wao wamelala na kisha akakiacha chombo kikiwa kimefunikwa na jambo hilo ndio likaja kuwa dalili (hoja) ya ukweli wa madai yake asubuhi ya usiku wa Israi. (4)

Ibn al~Qayyim alisema, “Kulipo pambazuka Mtume wa Mwenyezi Mungu () akiwa kwa jamaa zake aliwaeleza yote aliyoonyeshwa na Mwenyezi Mungu Mtukufu Mwenye Kushinda, miongoni mwa miujiza Yake mikubwa. Makuraishi walipinga na hawakutaka kabisa kuamini khabari hizo.

Katika kutafuta ukweli wa maelezo yake walimtaka awaelezee ulivyo msikiti wa Baytul Al-Muqaddas. Kwa Uwezo Wake Mwenyezi Mungu (ﷻ) akamdhihirishia hiyo Baytul Al-Muqaddas machoni mwake, akawa anawaeleza alama zake moja baada ya nyingine na wakashindwa kukanusha kwa vile alikuwa akiwaambia ukweli.

Mwisho akawaeleza kuhusu ule msafara wa wafanyabiashara aliokutana nao wakati wa kwenda na kurudi; akawaeleza ni lini msafara huo unategemea kufika; akawaeleza kuhusu ngamia anayeuongoza msafara huo, na mambo yakatokea kama alivyowaeleza. Hata baada ya kujulishwa yote hayo Makuraish walizidi kukanusha na kukufuru. Abubakar (Radhi za Allah ziwe juu yake) ameitwa ”Swiddiq” ’Msadikishaji’ kwa sababu ya kulisadikisha tukio hili (5)

Yapo maelezo mafupi na marefu yaliyokuja katika kuelezea sababu ya safari Ipo pia Kauli ya Mwenyezi Mungu (ﷻ) Mwenyewe inayotosha kabisa kueleza sababu ya safari hii, pale Anaposema;

(لِنُرِيَهُ مِنْ آيَاتِنَا ۚ)

[Ili Tumuonyeshe baadhi ya alama zetu.] (17:1)

Na huu ni utaratibu wa Allah (ﷻ) kwa Mitume, pahala pengine ndani ya Qur’an Anasema:

وَكَذَٰلِكَ نُرِي إِبْرَاهِيمَ مَلَكُوتَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَلِيَكُونَ مِنَ الْمُوقِنِينَ

”Na namna hivi Tulimuonyesha Ibrahim Ufalme wa mbingu na ardhi (kuwa ni wa Mungu), na ili awe miongoni mwa wenye yaqini’.” (6: 75).

Na Alisema kumwambia Musa (a.s):

لِنُرِيَكَ مِنْ آيَاتِنَا الْكُبْرَى

”Ili Tukuonyeshe miujiza (mingine) mikubwa mikubwa.” (20:23).

Na Ameweka wazi makusudi ya huko kuonyeshwa, “ili awe ni miangoni mwa wenye yaqini.” Kwa hivyo ni wazi basi kuwa elimu ya Mitume katika Kumjua Mola Wao inatokana na kuiona kwa macho miujiza Yake na kwa njia hiyo kuwa na yaqini na Allah (ﷻ) kwa kiasi kisichokuwa na mfano. Ni ukweli ulio wazi kuwa jambo la kujionea si sawa na la kusikia, na hii ndiyo sababu Mitume (Rehema na amani ziwe juu yao) walivumilia mengi katika njia ya Mwenyezi Mungu (ﷻ) mambo ambayo si rahisi kuvumiliwa na watu wa kawaida. Nguvu zote za kidunia mbele ya Mitume ni kama ubawa wa mbu hawatishiki nazo hata chembe, hata wanapofanyiwa vitimbi na wakati mwingine kuteswa.

Kwa hakika utafiti wa hekima na siri zilizojificha nyuma ya sehemu ndogo ndogo za safari hii, vipo katika vitabu vya siri za sheria, hapa sisi tutajihusisha na hakika za kawaida zinazochimbuka kutoka kwenye chemchemu ya safari hii yenye kubarikiwa, na zinazomiminika kutoka kwenye bustani ya maua ya Sira za Mtume (), zimfikie mwenye Sira hii, Rehma na Amani za Mwenyezi Mungu (ﷻ) na maamkizi mema. Ninaona ni bora nikaandika baadhi ya hayo niliyotaja kwa muhtasari: –

Bila shaka msomaji ataona kuwa katika Suratul Israa Mwenyezi Mungu (ﷻ) Amekitaja kisa cha Al-Israa katika aya moja tu,‘ kisha akaingia katika kutaja fedheha za  Mayahudi na maovu yao, na kisha akawazindua kwa kuwaeleza kuwa hii Qur’an inaongoza kwenye mambo yanayohitaji misimamo madhubuti kabisa. Inawezekana msomaji akadhania kuwa hizo aya mbili hazina uhusiano wowote, jambo hilo si kweli, maana kwa maneno haya Mwenyezi Mungu Mtukufu Anaashiria kuwa kwa hakika Israa ni tukio lililotokea Baytul Al-Muqaddas na kuwa Mayahudi watanyang’anywa cheo cha kuwaongoza wanaadarnu kutokana na matendo yao maovu ambayo wameyafanya. Matendo ambayo hayakubakisha nafasi ya wao kubakia katika cheo hicho na kuwa Mwenyezi Mungu (ﷻ) Atakihamisha cheo hicho kwa vitendo na kumkabidhi Mtume Wake Muhammad () ambaye Atamkusanyia vituo viwili vikuu vya Da’wa ya Ibrahim (Rehema na amani ziwe juu yake). Wakati umefika wa kuhamishwa kwa uongozi wa kiroho kutoka umma ulioijaza historia yake kwa udanganyifu, khiana, madhambi na uadui kwenda katika umma mwingine utakaoaminika kwa wema na kheri. Mtume wa umma huo hakuacha kuwa anayesifika na wahyi wa Qur’an inayoongoza kwenye msimamo ulio sahihi.

Kwa vipi utahama uongozi huu hali ya kuwa Mtume () anazunguka katika majabali ya Makka hali ya kuwa ni mwenye kufukuzwa na kupingwa na watu wa kabila lake?. Suala hili linaibua ukweli mwingine ambao ni kuwa mzunguko wa kwanza katika Da’awa hii ya Kiislamu umekaribia kufika mwisho na kukamilika, na baada ya hapo utaanza mzunguko mwingine ambao unatofautiana na mzunguko wa kwanza katika mapito yake. Kwa sababu hiyo ndio maana tunaona kuwa baadhi ya aya zinakusanya mambo yanayohusu makhofisho ya wazi na makamio ya kutisha dhidi ya Mushirikina;

وَإِذَا أَرَدْنَا أَن نُّهْلِكَ قَرْيَةً أَمَرْنَا مُتْرَفِيهَا فَفَسَقُوا فِيهَا فَحَقَّ عَلَيْهَا الْقَوْلُ فَدَمَّرْنَاهَا تَدْمِيرًا (16) وَكَمْ أَهْلَكْنَا مِنَ الْقُرُونِ مِن بَعْدِ نُوحٍ ۗ وَكَفَىٰ بِرَبِّكَ بِذُنُوبِ عِبَادِهِ خَبِيرًا بَصِيرًا

 [ Na pindi tukitaka kuuteketeza mji huwaamrisha wale wenye starehe na taanusi, lakini wao huendelea kutenda maovu humo. Basi hapo kauli huthibiti juu ya mji huo, nasi tukauangamiza kwa maangamizo makubwa. Na kaumu ngapi tumeziangamiza baada ya Nuhu! Na Mola wako Mlezi anatosha kabisa kuwa ni Mwenye kuzijua na kuziona dhambi za waja wake.]  (17: 16-17)

Pamoja na aya hizi zipo aya nyingine zilizowawekea wazi Waislamu na zinazoendelea kuwawekea misingi ya maendeleo na kanuni zake na vyanzo vyake ambavyo hujenga jamii ya Kiislamu. Kama vile tayari wamekwisha fika kwenye ardhi iliyo tayari, waliyapanga vizuri mambo yao kwa pande zote na wakaunda umoja wenye mshikamano madhubuti.

Katika jamii yao, hali kadhalika kulikuwepo na ishara ya kuwa Mtume () atapata makimbilio na mahali pa amani ambako yatatulizana mambo yake na makimbilio hayo ndiyo yangekuwa kituo cha wito wake katika pande zote za dunia. Hii ni moja ya siri miongoni mwa siri. za safari hii yenye kubarikiwa ambayo inahusiana na utafiti wetu huu (wa kitabu hiki), tumeona tuipe kipaumbele kwa kuitaja, na kwa ajili ya hekima hii na mifano yake tunaona kuwa kwa hakika hakuna shaka Israa ilituka nyuma kidogo ya mkataba wa Aqabah wa kwanza au wa pili na Allah Ndiye Mjuzi zaidi.


1) Zaad Ma’ud, Iuzuu 2, Uk. 149. Mukhtusar Simti Rrasul, Uk. 148-149. Rahmatun Lil ’Alamin,]uzuu 1, Uk. 76. Tarikhul Islam, Juzuu 1, Uk. 124. 249.
2) Zaad Ma’ad, Juzuu 2, Uk. 47-48
3) Zaad M’ad, Juzuu 2, Uk. 47-48. Sahihil Bukhari, Juzuu 1, Uk. 50, 455-456, 470-471, 481, 548-550; Juzuu 2, Uk. 684. Sahihil Muslim, Juzuu 1, Uk. 91-96. 252
4) Ibn Hisham, juzuu 1, Uk. 397, 402-406
5) Zaad Ma’ad, Iuzuu 1, Uk. 48. Suhihil Bukhari, Iuzuu 2, Uk. 684. Sahihil Muslim, Iuzuu 1, Uk. 96. Ibn Hisham, ]uzuu 1, Uk. 402-403. 755 Ibid. Iuzuu 1, Uk. 399. 254
*) Arrahiq Al-Makhtuum Uk -247-257

Begin typing your search above and press return to search.