Nayo ni kukubali na kuamini imani mathubuti kuwa Allah pekee ndiye Mola wa kila kitu na mfalme wavyo na muumba wavyo, mwenye kufisha na kupeana uhai, mwenye kuleta manufaa na kudhuru, na mwenye kuendesha mambo yao wote, hana mshirika yeyote katika haya yote.
Baadhi ya mambo yanayoambatana na kukubali hii tauhidi:
1. Kuamini kuwa Allah yupo
2. Kuamini kwa vitendo vyake Allah kama kuumba, kuruzuku, kufisha na kuhuisha n.k.
3. Kuamini kwa (Qadhaa na Qadar yake Allah), yani makadirio yake ya kufanyika au kutofanyika vitu.
Dalili katika Qurani za hii aina ya tauhidi
1. Kauli yake Allah:
[ الْحَمْدُ لِلَّهِ رَبِّ الْعَالَمِين} [الفاتحة: 2]
[Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wa viumbe vyote;] [Suratul-Fatiha aya 2]
2. Na kauli yake Mwenyezi Mungu:
[ الْحَمْدُ لِلَّهِ الَّذِي خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ وَجَعَلَ الظُّلُمَاتِ وَالنُّورَ ثُمَّ الَّذِينَ كَفَرُوا بِرَبِّهِمْ يَعْدِلُونَ] [الأنعام :1]
[Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu aliye umba mbingu na ardhi, na akafanya giza na mwangaza. Tena baada ya haya walio kufuru wanawafanya wengine sawa na Mola wao Mlezi.] [Al-An`aam aya 1].
3. Na kauli yake Allah:
[ قُلْ مَنْ رَبُّ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ قُلِ اللَّهُ} [الرعد: 16}
[Sema: Ni nani Mola Mlezi wa mbingu na ardhi? Sema: Mwenyezi Mungu.] [Araad aya 16].
4. Na kauli yake Allah :
[ هَذَا خَلْقُ اللَّهِ فَأَرُونِي مَاذَا خَلَقَ الَّذِينَ مِنْ دُونِهِ بَلِ الظَّالِمُونَ فِي ضَلَالٍ مُبِينٍ ] [ لقمان: 11]
[Huu ni uumbaji wa Mwenyezi Mungu. Basi nionyesheni wameumba nini hao wasiokuwa Yeye! Lakini madhaalimu wamo katika upotovu uliyo dhaahiri.] [Luqman:11]
5. Na kauli yake
[إِنَّ اللَّهَ هُوَ الرَّزَّاقُ ذُو الْقُوَّةِ الْمَتِينُ] [الذاريات: 58]
[Hakika Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye kuruzuku, Mwenye nguvu, Madhubuti.] [Dhariyaat aya 58]
6. Na dalili nyingine ni kwamba, wale washirikina waliokuwa wakati wa mtume s.a.w walijua na kukiri hii aina ya tauhidi lakini jambo hili halikuwaingiza katika Wisilamu.Bali Mwenyezi Mungu aliwaita kuwa wao ni washirikina. Amesema Allah:
[ وَمَا يُؤْمِنُ أَكْثَرُهُمْ بِاللَّهِ إِلَّا وَهُمْ مُشْرِكُون] [يوسف: 106]
[Na wengi katika wao hawamuamini Mwenyezi Mungu pasina kuwa ni washirikina.]
[Suratul Yusuf aya 106].
Na maana ya kauli yake [Na wengi katika wao hawamuamini Mwenyezi Mungu]. Hapa, Mwenyezi Mungu amethibitisha kwamba wao wanaamini pamoja kwamba amewasifu kwamba wao ni washirikina. Imani hii aliyowasifu nayo ndiyo ya tauhidurububiyya. Kwani wao wanaamini kwamba Allah ndiye muumba wa vyote, mwenye kuruzuku,mwenye kufisha lakini pamoja na hii imani wanamshirikisha Allah katika ibada kwa kuabudu viumbe wengine pamoja na Mwenyezi Mungu.
Kuanzia Mwenyezi Mungu awaumbe viumbe, wote wamekuwa wakikiri na kuijua hii tauhidi ya rububiyya. Na mwenye kuipinga, hakika ndani ya kukanusha na kupinga kwake kuna uongo. Yeye anapinga tu kwa ulimi lakini moyo wake kwa ndani unakiri na kuamini kwamba Mwenyezi Mungu ndiye Mola Mlezi,Muumba wa vyote,Mwenye uwezo juu ya vyote na Mfalme wa wafalme. Na huu ndio uhakika wa tauhidi ya rububiyya. Hivyo mwenye kusema kwamba haamini kwa hii tauhidi, ni mwongo. Allah(Subhaanahu wa Ta´ala) Anasema kuhusu Fir´awn na watu wake waliopinga hii tauhidi :
[ وَجَحَدُوا بِهَا وَاسْتَيْقَنَتْهَا أَنفُسُهُمْ ظُلْمًا وَعُلُوًّا } [النمل : 14 }
[Wakazikanusha na hali kuwa nafsi zao zimeziyakinisha; kwa dhulma na majivuno.] [Suratul Naml aya 14]
JE, TAWHIDIRUBUBIYA YA MUINGIZA MTU KATIKA UISLAMU?
Tauhidurububuyah haimtoshelezi mtu wala haimwingizi katika Wisilamu. Ndiyo maana mtume ﷺ aliwapiga vita washirikina pamoja na kwmba walikuwa na tauhidurububiyya. Lakini kwa kuwa walikuwa wanawaomba viumbe wengine pamoja na Mwenyezi Mungu, mtume kawapiga vita hadi wamwabudu Mwenyzi Mungu pekee. Amesema mtume ﷺ:
أمرت أن أقاتل الناس حتى يشهدوا ألا إله إلا الله، وأن محمداً رسول الله] رواه البخاري ومسلم]
[Nimeamrishwa kuwa niwapige vita watu mpaka washuhudie kwamba hapana mola apasae kuabudiwa kwa haki illa Mwenyezi Mungu na kwamba Mohammad (Swala Allahu alaihi wasallam) ni mjumbe wa Mwenyezi Mungu….] [Imepokewa na Bukhari na Muslim.]
Nao wanaopigwa vita ni watu wote ambao hawajampwekeshea Mwenyezi Mungu ibada hata ingawa wanaamini katika tauhidurububiyya, haitawatosheleza,hadi wamuabudu Allah pekee kwa kutimiza tauhidul-uluhiyya kama itakavyokuja hapo mbeleni. (1)
(1) Chanzo: Tauhidi. Daktari Hajj Makokha Maulid